Vijana shikamaneni katika: Imani, Sakramenti, Maadili na Sala! Vijana shikamaneni katika: Imani, Sakramenti, Maadili na Sala! 

Vijana shikamaneni katika: Imani, Sakramenti, Maadili na Sala!

Kanisa ni Jumuiya ya waamini wanaotembea pamoja katika: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na Sala. Hii ni Jumuiya inayofumbatwa katika misingi ya: imani, matumaini na mapendo kwa kuambata mshikamano na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hawa ndiyo wakimbizi na wahamiaji; maskini, wazee na wagonjwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Twende pamoja, ni kilio cha vijana tangu wakati wa utangulizi na hatimaye, maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana iliyofanyika mwaka 2018. Kanisa ni Jumuiya ya waamini wanaotembea pamoja katika: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na Sala. Hii ni Jumuiya inayofumbatwa katika misingi ya: imani, matumaini na mapendo kwa kuambata mshikamano na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hawa ndiyo wakimbizi na wahamiaji; maskini, wazee na wagonjwa ambao wanaonekana kana kwamba si mali kitu katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia!

Huu ni muhtasari wa mahubiri yaliyotolewa, Jumatano, tarehe 23 Januari 2019 na Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kwa vijana wanaohudhuria maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani huko Panama. Maadhimisho haya ni muda muafaka wa kujenga na kudumisha urafiki wa dhati, upendo na mshikamano unaosimikwa katika umoja na udugu wa watoto wa Mungu. Ni fursa ya kutoka katika ubinafsi, uchoyo na unafiki, tayari kumfungulia Kristo Yesu, malango ya maisha, ili kupata maisha katika utimilifu wake.

Vijana wawe ni vyombo na mashuhuda wa uinjilishaji; faraja na matumaini kwa wale wanaotoka katika nchi ambazo zinaendelea kuogelea katika vita, kinzani na mipasuko ya kijamii: Wawe ni faraja kwa wale wote wanaoteseka kwa njaa, magonja na umaskini wa hali na kipato! Imani kwa Kristo Yesu, iwawezeshe kujenga ari ya kimisionari na Injili ya huduma ya upendo. Maadhimisho haya, yawe ni sehemu ya uponyaji wa ukoma wa maisha ya kiroho na kimwili, unaowaandama vijana katika hija yao ya maisha, ili kweli waweze kupenda kwa dhati na kuwajibika katika upendo huo! Ni muda wa kutoa na kupokea; kusamehe na kusahau; kuganga na kuponya majeraha ya ndani kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini! Kimsingi, maisha ya binadamu yanafumbatwa katika upendo kwa Mungu na jirani!

Kwa upande wake, Askofu mkuu Josè Domingo Ulloa Mendieta wa Jimbo kuu la Panama anasema, vijana wa kizazi kipya ndio walengwa wakuu wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa sababu Kanisa lina imani na matumaini kwa vijana. Kwa njia uwepo na ushiriki wao, vijana wanaweza kuleta mageuzi makubwa katika maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Anawahamasisha vijana kuwa wasikivu kwa mpango wa Mungu katika maisha yao, tayari kuumwilisha katika uhalisia wa maisha na vipaumbele vyao. Vijana wawe mstari wa mbele kufuata mifano bora ya maisha kutoka kwa watakatifu na wafiadini, waliosadaka maisha yao kwa ajili ya Mungu, Kanisa na jirani! Watakatifu ni wadhambi waliotubu na kumwongokea Mungu; wakasimama kidete: Kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu, utu na heshima yake. Ni watu waliokuwa na furaha ya kweli iliyokuwa inabubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Vijana wanahamasishwa na Mama Kanisa kujikita katika malezi ya awali na endelevu kwa kutumia mwongozo uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko: DOCAT: Yaani “Kitabu cha Mkusanyiko wa Mafundisho Jamii ya Kanisa, tayari kuyatangaza na kuyashuhudia katika vipaumbele vya maisha na utume wao! Huu ni muhtasari wa mafundisho Jamii ya Kanisa kutoka kwa Papa Leo XIII “Rerum Novarum” yaani “Mambo Mapya” msingi wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayofumbatwa katika: Haki msingi, utu na heshima ya binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, hadi katika Mafundisho ya Papa Francisko: “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” na “Amoris laetitia” yaani “Furaha katika upendo ndani ya familia”.

Baba Mtakatifu anasema, muhtasari huu ni nyenzo muhimu katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa mwanga wa Injili na Mafundisho Jamii ya Kanisa. Ni nyenzo ya toba na wongofu wa ndani, ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili na kwa nguvu na jeuri ya Injili, vijana wanaweza kuleta mabadiliko makubwa katika ulimwengu mamboleo kwa kuendelea kujikita katika upendo, haki, amani na mshikamano wa dhati!

Kardinali: Vijana Panama
24 January 2019, 13:24