Tafuta

Neno la Mungu ni muhimu katika kujenga Jumuiya ya waamini na Kristo yesu ni ufunuo hai wa Neno la Mungu na ni Yeye hasa aliye Neno wa Mungu. Neno la Mungu ni muhimu katika kujenga Jumuiya ya waamini na Kristo yesu ni ufunuo hai wa Neno la Mungu na ni Yeye hasa aliye Neno wa Mungu. 

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili III ya Mwaka C: Ufunuo!

Leo tunatafakari Masomo ya dominika ya 3 ya Mwaka C wa Kanisa. Ni masomo ambayo kwa namna ya pekee kabisa yanazungumzia nafasi ya Neno la Mungu katika kuunda jumuiya ya waamini na katika kuunda imani ya mwamini na hapo hapo kutuonesha kuwa Kristo ndiye ufunuo hai wa Neno hilo la Mungu na ni Yeye hasa aliye Neno la Mungu.

Na Padre william Bahitwa, - Vatican.

Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunatafakari Masomo ya dominika ya 3 ya Mwaka C wa Kanisa. Ni masomo ambayo kwa namna ya pekee kabisa yanazungumzia nafasi ya Neno la Mungu katika kuunda jumuiya ya waamini na katika kuunda imani ya mwamini na hapo hapo kutuonesha kuwa Kristo ndiye ufunuo hai wa Neno hilo la Mungu na ni Yeye hasa aliye Neno la Mungu.

Ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza (Neh 8: 2-4, 5-6. 8-10) ni kutoka katika kitabu cha Nehemia. Kitabu hiki cha Nehemia pamoja na kitabu vya Mambo ya Nyakati na kile cha Ezra ni vitabu vinavyotoa mfululizo wa pili wa vitabu vya Agano la Kale vinavyosimulia Historia ya Israeli. Kwa ujumla vitabu hivi vitatu vinarudia historia ile ile inayoelezwa kutoka kitabu cha Yoshua hadi kitabu cha pili cha Wafalme lakini pia vinaongeza matukio mapya hasa historia ya waisraeli baada ya kurudi kutoka utumwani Babeli. Kitabu cha Nehemia chenyewe kinaonesha jitihada za kuliunda upya taifa la Israeli kama taifa teule la Mungu na taifa linaloshika torati kama msingi na kiini cha utaifa wao.

Somo la leo linaonesha namna Torati ilivyokuwa ikipewa heshima na nafasi ya kwanza. Ezra kuhani aliileta mbele ya kusanyiko la watu na akaisoma na kuifafanua katika siku hiyo maalum na takatifu kwa Bwana. Torati iliposomwa iliwachoma watu mioyo wakalia na kuomboleza hata Nehemia na walawi wakawaambia watu “siku hii ni takatifu kwa Bwana Mungu wenu, msiomboleze wala msilie”. Torati ni kanuni na maagizo ya Mungu kwa watu wake, ni Neno la Mungu ni  na kwa wayahudi ndiyo Biblia hasa. Somo hili linaonesha namna ambavyo wayahudi waliliheshimu Neno la Mungu na kulipa nafasi ya juu kabisa katika utaifa wao. Ni somo linaloonesha pia mwanzo wa huduma za hekaluni ambazo kiini chake kilikuwa ni kulisikiliza Neno la Mungu, kulifafanua na kulitafakari kwa kuwa ndilo hasa taa ya miguu yao na mwanga katika njia zao, rej Zab 119:105

Somo la pili (1Kor 12:12-30) ni waraka kwa kwanza wa mtume Paulo kwa wakorinto. Mtume Paulo anaiandikia jumuiya ya wakristo wa Korinto, jumuiya iliyokuwa na tatizo la mgawanyiko. Katika somo la leo anawaalika kujenga umoja kati yao kwa kuangalia sura ya kanisa kama mwili wa fumbo wa Kristo ambao ni kama mwili wa kawaida wa mtu. Ni mwili ulio na viungo vingi: kuna mkono, mguu, pua, macho, sikio na kadhalika. Kila kiungo kina nafasi yake, kila kiungo kina thamani yake na kila kiungo kina kazi yake. Hakuna kiungo kinachoweza kusimama peke yake nje ya mwili kumbe vyote vinategemeana kwa jinsi vinavyounda mwili mmoja.

Hoja za mtume Paulo ni mbili. Ya kwanza wale wanaojiona wadogo, wanajidharau na kuona mchango wao hauna thamani katika jumuiya hawapaswi kufanya hivyo kwa sababukila mwanajumuiya ana thamani yake ya pekee. Anasema “Mguu ukisema kwa kuwa mimi si mkono mimi si wa mwili’ je si wa mwili kwa sababu hiyo” Hoja ya pili ni kuwa wale katika jumuiya wanaojikuza na kuwadharau wengine kulingana na nafasi zao hawapaswi nao kufanya hivyo kwa sababu wanajumuiya wote wanategemeana. Anasema Mtume Paulo “jicho haliwezi kuuambia mkono ‘sina haja na wewe’ wala tena kichwa hakiwezi kuiambia miguu ‘sina haja na ninyi’” Ni mwili mmoja.

Fundisho hili Mtume Paulo halitoi kama nadharia, yeye mwenyewe ni mfano hai. Kabla ya wongofu wake aliwatesa na kuwaua wafuasi wengi wa Kristo. Na siku Kristo anamtokea katika njia ile ielekeayo Damasko alimwambia moja kwa moja “Saulo kwa nini wanitesa” na tena “Mimi ndimi Yesu unayenitesa” (Rej. Mate 9:5.) Kristo ameungana moja kwa moja na watu wake katika mwili wake wa fumbo. Mateso kwa mmojawapo wao ni mateso kwa mwili mzima wa Kristo. Hili ni somo linalotupatia taalimungu kubwa iliyoficha si tu katika umoja wa wakrito bali ule umoja unaoounganisha ubinadamu mzima.

Injili (Lk 1:1-4, 14-21) Katika mwaka huu C wa kanisa tuliouanza, masomo ya dominika ni yale kutoka kwa mwinjili Luka. Na katika liturujia ya leo tunaanza na sura ya kwanza na aya za kwanza zinayotoa utangulizi wa injili yote. Luka anaeleza ameiandika injili yake kwa Theofilo. Inawezekana alikuwa ni mmojawapo wa wanafunzi wake au kiongozi fulani. Lakini kwa kuangalia maana ya Theofilo – mtu anayempenda Mungu -  tunaweza kusema kuwa Luka ameiandika si kwa mtu mmoja bali ni kwa wote wanaompenda Mungu. Na moja kwa moja somo letu linatupeleka katika sura ya nne ambapo Yesu anaanza utume wake wa hadharani. Anauanza akiwa amejaa Roho Mtakatifu na ni kwa Roho Mtakatifu ataufanya utume wake hadi mwisho. Anauanza kwa kuyafungua Maandiko na kuyasoma mbele ya watu kama alivyofanya Ezra katika somo la kwanza.

Kisha kusoma anatangaza kuwa “Leo Maandiko haya yametimia masikioni mwenu”.  Maandiko yametimia kwa sababu ni yeye aliyekuwa akizungumziwa katika utabiri huo: ni yeye aliyejazwa Roho Mtakatifu, ni yeye aliyepakwa mafuta, yaani kuwa Kristo (mpakwa mafuta), ni yeye anayekuja kutangaza Habari Njema na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa. Lakini kwa namna ya pekee zaidi maneno yametimia kwa sababu Maandiko hayo yaliyokuwa yakisomwa tangu enzi za Agano la Kale, sasa kwa njia yake yamepata kuwa hai. Kristo ndiye ufunuo hai wa Maandiko Matakatifu na ni yeye aliye Maandiko hai, ndiye Habari Njema.

tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News masomo yetu ya leo yanajikita katika kuonesha nafasi na thamani ya Neno la Mungu. Neno la Mungu ni Neno linalobeba historia ya wokovu - kumbukumbu ya historia ya mahusiano ya Mungu na watu wake, Ni Neno linaloshuhudia namna ambavyo Mungu aliingia katika maisha ya watu na akaongoza maisha yao kuufikia mwisho alioukusudia mwenyewe, ni Neno linaloshuhudia kazi za wajumbe mbalimbali wa Mungu na utume wao kwa watu wa Mungu. Lakini hapo hapo Neno la Mungu linakuwa ni Neno linalounda taifa jipya la watu wa Mungu kila wakati na kila mara linapotangazwa. Ndiyo maana Neno la Mungu ni Neno hai daima na ni neno lenye nguvu daima na ni Neno jipya daima.

Tunaalikwa leo kulitambua Neno la Mungu kama mojawapo ya mihimili inayounda imani na mojawapo ya mihimili inayounda na kukuza jumuiya ya waamini. Desturi ya kusoma Neno la Mungu binafsi, katika familia au katika jumuiya ni desturi inayomkutanisha mtu na Neno hai lenye uzima. Tunaweza kuliona Neno kama masimulizi ya kawaida ya Biblia na huenda yale tuliyoyazoea kwa sababu tumekwishayasikiliza na kuyasoma mara nyingi, lakini ni katika ukawaida huo huo tunajipatia mang’amuzi mapya ya imani, tunaikuza imani na tunakutana na yule ambaye ni Neno hai yaani Kristo Bwana wetu. Kila mara Neno la Mungu linaposomwa kama Neno la Mungu, hata ubobee namna gani katika Biblia lazima utatoka na kitu kipya.

Kulisikiliza Neno la Mungu kwa uchaji na kulitangaza kwa tumaini thabiti kama tuvyoalikwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican (Dei verbum n 1) ni kuiendeleza kazi ile ile ya wokovu ambayo Mungu aliitambulisha kwa Neno lake. Tulipende Neno la Mungu, tulibebe Neno la Mungu, tulisome Neno la Mungu na tujivunie Neno la Mungu kama hazina kubwa ya wokovu wetu.

liturujia 3 J Mwaka C wa Kanisa
25 January 2019, 16:26