Tafuta

Zambia: Mpango Mkakati wa Mwezi wa Kimisionari Oktoba 2019: Sala, Sakramenti, Tafakati, Ushuhuda na Matendo ya huruma Zambia: Mpango Mkakati wa Mwezi wa Kimisionari Oktoba 2019: Sala, Sakramenti, Tafakati, Ushuhuda na Matendo ya huruma 

Zambia: Mpango Mkakati wa Mwezi wa Kimisionari Oktoba 2019

Ni wakati wa ushuhuda wa wamisionari na wafiadini waliosadaka maisha yao kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Ni muda wa majiundo makini katika Maandiko Matakatifu na Katekesi; Maisha ya kiroho pamoja na upendo wa kimisionari. Haya ndiyo mambo msingi yanayopaswa kumwilishwa kama sehemu ya utekelezaji wa Mwezi Oktoba 2019.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mwezi Oktoba 2019 kitakuwa ni kipindi maalum sana kwa maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Huu ni muda wa kusali na kutafakari utume kama msingi wa mchakato mzima wa uinjilishaji mpya unaotekelezwa na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Ni kipindi cha ushuhuda wa  huruma na upendo Mungu unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Mwezi Oktoba 2019 Kanisa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume"Maximum Illud" yaani “Kuhusu Shughuli za Kimisionari.” Ni muda wa: sala, katakesi, tafakari na matendo ya huruma!

Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 unaongozwa na kauli mbiu “Mmebatizwa na kutumwa: Kanisa la Kristo katika utume”.  Kanisa linataka kuendeleza wito na utume wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, agizo kutoka kwa Kristo mwenyewe kwa wafuasi wake. Hiki ni kipindi maalum sana kwa maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Huu ni muda wa kutangaza furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa; Kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa ari na ushiriki mkamilifu na hatimaye, Kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Ni wakati muafaka kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanatelekeza vyema dhamana na wajibu waliojitwalia kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo inayowashirikisha: Unabii, Ukuhani na Ufalme wa Kristo. Waamini wakiwa wamezaliwa upya kwa “Maji, Roho Mtakatifu na Neno”, wana wajibu wa kukiri na kutangaza imani ambayo wameipokea kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kanisa na hivyo kushiriki katika utendaji wa kitume na wa kimisionari wa Taifa la Mungu. Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia, ZCCB, tayari limeanza maandalizi ya maadhimisho ya Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 utakaoyashirikisha majimbo yote nchini humo pamoja na kuongozwa na Waraka wa Kichungaji kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia kwa Familia ya Mungu nchini humo kwa mwaka 2016.

Pamoja na mambo mengine, Waraka huu uligusia: hali ya kisiasa nchini Zambia; hali ya uchumi na athari zake kijamii; umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote; ushauri kwa vyama vya kisiasa na wanasiasa wenyewe pamoja na makundi mbali mbali nchini humo, ili kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha mafao ya wengi, haki, amani na umoja wa kitaifa. Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia linasema, hii ni dhamana ya: Kikuhani, Kifalme na Kinabii wanayoshirikishwa watu wa Mungu kadiri ya miito na utume wao ndani ya Kanisa.

Padre Cleophas Lungu, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia anasema, kwa familia ya Mungu nchini Zambia, Mwezi Oktoba, 2019 itakuwa ni fursa ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya wamisionari waliojisadaka na wale wote wanaoendelea kujitosa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili ndani na nje ya Zambia. Ni watu walioguswa na kutikiswa kwa magonjwa, hali ngumu ya maisha pamoja na vifo katika ujana wao, lakini wakathubutu kupiga moyo mkonde na kutoka kimasomaso kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kumbe, kwa sasa Wakristo wote wanahimizwa kushiriki kwa hali na mali kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kuanzia ndani ya familia zao. Huu ni wakati kwa majimbo na parokia zote nchini Zambia luhakikisha kwamba, zinatekeleza kwa dhati kabisa Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 kwa kujikita zaidi katika jitihada binafsi za kukutana na Kristo Yesu kwa njia ya Neno na Sakramenti za Kanisa.

Ni wakati wa ushuhuda wa wamisionari na wafiadini waliosadaka maisha yao kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Ni muda wa majiundo makini katika Maandiko Matakatifu na Katekesi; Maisha ya kiroho pamoja na upendo wa kimisionari. Haya ndiyo mambo msingi yanayopaswa kumwilishwa kama sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019, ambalo kimsingi ni tukio la kimataifa!

WARAKA WA KICHUNGAJI WA BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI ZAMBIA KWA MWAKA 2016

Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia katika Waraka wake wa kichungaji kwa Familia ya Mungu nchini Zambia kwa mwaka 2016 pamoja na mambo mengine, linagusia hali ya kisiasa nchini Zambia; hali ya uchumi na athari zake kijamii; umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote; ushauri kwa vyama vya kisiasa na wanasiasa wenyewe pamoja na makundi mbali mbali nchini Zambia, ili kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha mafao ya wengi, haki, amani na umoja wa kitaifa. Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia unaongozwa na kauli mbiu “Tazama, nitamwelekezea amani kama mto…”  Isaya 66:12.

Maaskofu wanaialika Familia ya Mungu nchini Zambia kusimama kidete kulinda na kudumisha mafao ya wengi, kuchunguza dhamiri ili kuangalia ni watu Wazambia wameteleza na kuanguka na ni mahali gani walipofanikiwa Zaidi, ili kuanza mwaka 2016 kwa ari na matumaini makubwa wakati huu Zambia inapojiandaa kwa uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika tarehe 11 Agosti, 2016. Hiki kiwe ni kipindi cha kuonesha ukomavu wa kisiasa kwa kudumisha demokrasia ya kweli, haki, amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa.

Vyombo vya ulinzi na usalama vihakikishe kwamba vinalinda na kudumisha amani na utulivu. Vyama vya kisiasa na wanasiasa wenyewe wajenge utamaduni wa kuvumiliana kwa kufanya kampeni za kistaarabu. Maaskofu wanapongeza hatua ya Serikali iliyoko madarakati kwa kuridhia marekebisho ya Katiba ya Zambia, lakini wanasema, kuna haja ya kuwa na dira na mwelekeo wa kupata Katiba Mpya. Marekebisho ya Katiba yawafikie walengwa, yaani wananchi wengi wa Zambia. Maaskofu bado wanaendelea kukazia umuhimu wa Kura ya Maoni, itakatosaidia mchakato wa maboresho ya utu, heshima na maisha ya wananchi wengi wa Zambia.

Jeshi la Polisi linapaswa kuwa ni kwa ajili ya mafao ya wananchi wa Zambia na wala si kwa ajili ya Chama tawala. Umajimbo na Ukabila ni mambo ambayo kwa sasa ni hatari sana kwa mshikamano na mafungamano ya Wazambia ambao wanapaswa kukumbuka kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; umoja na utofauti wao ni utajiri mkubwa kwa ustawi na maendeleo ya nchi. Wanasiasa wakijikita katika ukabila ili kuwagawa wananchi, watambue kwamba, wanajipalia makaa ya moto, hawatakuwa na watu wa kuwaongoza!

Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia linasikitika kusema kwamba, hali ya uchumi ni mbaya kiasi kwamba, waathirika wakuu ni wananchi wanaoishi vijijini. Kilio cha maskini kinapaswa kusikilizwa na kupatia majibu muafaka. Serikali inapaswa kutumia rasilimali ya nchi kwa umakini mkubwa, kwa kuzingatia ukweli, haki na usawa. Serikali iwe mstari wa mbele kulinda ajira za wananchi wake dhidi ya makampuni yanayotaka kuchuma faida kubwa kwa gharama ya maisha ya Wazambia. Maaskofu wanawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema nchini Zambia, kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha mazingira bora, nyumba ya wote kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kichungaji juu ya utunzaji bora wa mazingira, "Laudato si". Serikali iwe makini na wawekezaji wa ndani na nje, ili kulinda na kudumisha mazingira kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Maaskofu wanavishauri vyama vya siasa kujikita katika misingi ya haki, amani na demokrasia pamoja na kuhakikisha kwamba, vinawachagua wagombea wenye sifa na ambao watakuwa kweli mstari wa mbele katika kudumisha mafao ya wengi. Serikali iwahakikishie wananchi wake ulinzi na usalama wa maisha na mali zao; iwe ni chombo cha haki, amani, upatanisho na umoja wa kitaifa. Wakuu wa wilaya wawe makini katika kufanikisha mchakato mzima wa uchaguzi mkuu nchini Zambia.

Maaskofu wanawataka vijana wa kizazi kipya, kamwe wasikubali kutumiwa na wanasiasa kwa ajili ya kusababisha fujo na vurugu sanjari na kujenga utamaduni wa kuvumiliana na kuheshimu wengine. Vyombo vya mawasiliano ya jamii, vitekeleze dhamana na wajibu wake kwa kuzingatia sharia, kanuni, maadili, ukweli na uwazi. Kanisa kwa upande wake litaendelea kusimama kidete kulinda na kutetea umoja na mshikamano wa kitaifa na kamwe halitakubali nyumba zake za Ibada kutumiwa na wanasiasa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu. Wanakanisa wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika mchakato wa kukuza na kudumisha tunu msingi za Injili, upendo, haki, amani, upatanisho; haki jamii, mafao ya wengi na usawa katika  masuala ya kisiasa na kiuchumi. Viongozi wa Kanisa wasikubali kutumiwa na wanasiasa kwa ajili ya mafao yao binafsi. Wanasiasa wanahamasishwa kuhudhuria Ibada za Misa Takatifu, lakini wasiruhusiwe kupewa nafasi ya kufanya kampeni Makanisani.

Lengo ni kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa, haki, amani na ustawi wa wananchi wengi wa Zambia. Familia ya Mungu iwe ni vyombo vya haki, amani, upendo na mshikamano; ili kukuza na kudumisha toba, wongofu, msamaha na upatanisho. Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia, umetolewa Lusaka, Zambia, na kupigwa mkwaju na Maaskofu Katoliki wa Zambia, tarehe 23 Januari 2016.

Zambia: Oktoba 2019
14 January 2019, 07:30