Tafuta

Vatican News
Mkutano wa 42 wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè kwa mwaka 2019-2020 utaadhimishwa Wroclaw, Poland Mkutano wa 42 wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè kwa mwaka 2019-2020 utaadhimishwa Wroclaw, Poland  (AFP or licensors)

Mkutano wa Vijana wa Taizè 2019-2020 kufanyika Poland

Siku ya 41 ya Vijana wa Kiekumene kwa Mwaka 2018 yameongozwa na kauli mbiu “Kamwe hatuwezi kusahau ukarimu”. Katika mkutano huo Baba Mtakatifu Francisko amewataka vijana kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema karama na mapaji yao kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya maisha, ili ulimwengu uweze kuwa ni mahali bora zaidi pa kuishi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

 

Fra Alois, Mkuu wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè ametangaza kwamba, Siku ya 42 ya Vijana wa Kiekumene itaanza kuadhimishwa tarehe 28 Desemba 2019 hadi tarehe Mosi, Januari 2020 huko mjini Wroclaw, nchini Poland. Na hii itakuwa ni mara ya tatu kwa Poland kuwa mwenyeji wa Siku ya Vijana wa Kiekumene Barani Ulaya. Hizi ni nyakati muhimu sana za maisha na utume wa Kanisa kwa vijana, zinazofumbatwa katika maisha ya sala, tafakari pamoja na ujenzi wa madaraja ya vijana kukutana, ili kuaminiana na kuthaminiana katika maisha yao, licha ya tofauti zao msingi katika maisha.

Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè katika tamko lake kwa vyombo vya habari inasema, mchakato wa ujenzi wa umoja na mshikamano ni muhimu sana kwa wakati huu Barani Ulaya, ambako uchoyo na ubinafsi unaonekana kutaka kushika kasi ya ajabu. Mkutano wa Poland utawapatia vijana fursa ya kuweza kukutana ili kujenga hali ya kuaminiana na kuthaminiana kama ndugu! Itakumbukwa kwamba, Maadhimisho ya Siku ya 41 ya Vijana wa Kiekumene kwa Mwaka 2018 yameongozwa na kauli mbiu “Kamwe hatuwezi kusahau ukarimu”.

Katika mkutano huo Baba Mtakatifu Francisko amewataka vijana kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema karama na mapaji yao kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya maisha, ili ulimwengu uweze kuwa ni mahali bora zaidi pa kuishi. Utamaduni wa ukarimu, uwawezeshe vijana kumfungulia Kristo Yesu, malango ya maisha yao, ili kuweza kusikiliza Neno lake na kulimwilisha katika uhalisia wa maisha yao.

Taizè 2019 Poland

 

 

03 January 2019, 08:56