Tafuta

Vatican News
Masista Wakarmeli wa Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu, Tanzania: Mbinu Mkakati wa Miaka 3. Umisionari na Utakatifu wa maisha! Masista Wakarmeli wa Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu, Tanzania: Mbinu Mkakati wa Miaka 3. Umisionari na Utakatifu wa maisha!  (ANSA)

Masista Wakarmeli Tanzania: Umisionari & Utakatifu wa maisha!

“Kuwa mmisionari kila mahali kwa utakatifu wa maisha, upendo wa kidugu, utajiri wa changamoto za tamaduni na ari ya kumpeleka Kristo hasa pembezoni kadiri ya roho ya waanzilishi”. Ndiyo mada iliyochanguliwa kuongoza Mkutano na mipango yote ya Shirika nchini Tanzania kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo. Ikizingatia mwito wa Baba mtakatifu Francisko kuhusu utakatifu wa maisha.

Na Sr. Vestina V. Tibenda, CMTBG. Roma.

Baada ya miaka thelathini na minne ya uwepo wao Barani Afrika hususani nchini Tanzania, Masista Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu wameadhimisha mkutano wao mkuu wa tisa.  Mkutano huu ambao huadhimishwa kila baada ya miaka mitatu, ulifanyika mnamo tarehe 9 – 15 Desemba 2018 katika kituo cha mafungo ya kiroho “St. Therese of Avilla Spritual Centre” Boko, Jimbo kuu la Dar es Salaam, chini ya uenyekiti wa Mama Mkuu wa Shirika SR. Donatella Cappello pamoja na Mshauri Mkuu Sr. Vestina Tibenda.

Mkutano ulihudhuliwa na Masista wote wa nadhiri za daima wanaofanya utume katika jumuiya saba za kitawa pamoja na masista wanne wa nadhiri za muda waliyochaguliwa kwa kura za wenzao ili kuwawakilisha katika mkutano huo.  Mkutano mkuu ni fursa ya kutathamini safari ya Shirika kwa miaka mitatu, ili kuhuhisha na kupyaisha ufahamu wa utambulisho wa kikarama na hatimaye kuweka malengo, mikakati na njia mahususi ambazo zitawasaidia wanashirika kuishi kwa ubunifu na uaminifu kwa karama na utume katika kukabiliana na mahitaji ya Kanisa na ulimwengu mamboleo.

Ili kuweza kuyafikia hayo malengo, ni muhimu kuyasoma maisha ya Shirika katika maeneo yake mengi kwa macho ya imani na ya kitaamuli yenye uwezo wa kutambua mapito ya Mungu katika historia ya kila mtawa binafsi na ya Shirika nchini Tanzania katika ujumla wake. “Kuwa mmisionari kila mahali kwa utakatifu wa maisha, upendo wa kidugu, utajiri wa changamoto za tamaduni na ari ya kumpeleka Kristo hasa pembezoni kadiri ya roho ya waanzilishi”. Ndiyo mada iliyochanguliwa kuongoza Mkutano na mipango yote ya Shirika nchini Tanzania kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo. Ikizingatia mwito wa Baba mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo”. Anasema, utakatifu ni mwaliko kwa waamini wote na wala si kwa watu wachache tu ndani ya Kanisa!

Huu ni mwaliko wa kuongeza jitihada za kukutana na Kristo Yesu katika maisha kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata: huruma na upendo wa Mungu katika maisha. Watakatifu ni watu wa kawaida kabisa, ni wadhambi waliotubu na kumwongokea Mungu, leo hii wamekuwa ni marafiki zake wa karibu! Watakatifu ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao! Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Wakristo wote wamejichukulia dhamana ya kuanza safari ya utakatifu wa maisha! Waraka huu unamhimiza kila Sista mkarmeli mmisionari kujikita katika safari ya utakatifu kadiri ya roho ya kikarmeli, yaani: roho ya sala na udugu, ili hatimaye, kumpeleka Kristo kwa watu. Sambamba na mipango mipya katika mkutano huo wameteuliwa pia viongozi watakao liongoza Shirika la Wakarmeli Wamisionari inchini Tanzania kwa kipindi kipya cha miaka mitatu (2018-2021).

Katika uteuzi huo Sr. Maria Lilian Kapongo ameteuliwa kuwa mwakilishi wa Mama Mkuu wa Shirika akisaidiwa na washauri watatu: Sr. M. Flora Mashughuli, Sr. M. Hildegalda Mbonde na Sr. M. Jovitha Kagemulo. Wakishirikiana na Masista wenzao, viongozi hao wanajukumu la kulinda  karama ya Shirika ili iendelee kuwa hai zaidi, kusimamia na kutekeleza mipango na maazimiom yaliyofikiwa wakati wa Mkutano Mkuu na kuwasaidia masista wenzao kuiishhi katika umoja na furaha ya maisha ya kindugu

Shirika la Masista Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu ni Shirika la kimataifa lenye hadhi ya kipapa, lililoanzishwa kunako mwaka 1925 na Mwenye heri M. Crocifissa Curcio pamoja na Padre Lorenzo Van Den Eerenbeemt katika mji wa Santa Marinella – Roma Italia. Linafanya utume wake katika mabara yote matano ya dunia. Masista waliingia nchini Tanzania kunako mwaka 1984 kufuatia mwaliko kutoka kwa Hayati Mwadhama Kardianli Laurian Rugambwa na hadi sasa kuna jumla ya watawa 76 Wazalendo wa kutoka: Tanzania, Kenya, Uganda na DRC wanaotekeleza dhamana na utume wao sehemu mbali mbali za Tanzania katika: Jimbo kuu la Dar es Salaam, Jimbo kuu teule la Mbeya, Jimbo la Tanga, Jimbo la Musoma, Jimbo la Bunda na katika jimbo Katoliki la Kahama.

Umisionari ni kipengele cha msingi kikarama, ambacho watawa hawa wanaitwa kuishi na kukimwilisha upya katika nyakati hizi za mageuzi makubwa kijamii, kisiasa na kiuchumi. Kadiri ya Mwenye heri M. Crocifissa “misioni” ni jambo lolote linalotuwezesha kumtangaza Kristo na upendo wake kwa kila mwanadamu, na hasa wale “wote waliyo wadogo wa dunia”; yaani kumfanya Kristo ajulikane, pia upendo wake na wa Baba yake upate kusikika kwenye maisha ya watu. Hii ndiyo tabia maalum ya karama halisi ya umisionari ambayo wanashirika wanaitwa kuiishi mahali popote, katika hali na nyakati zote: kuzileta roho za watu kwa Mungu; “kupyaisha ubinadamu” kwa njia ya malipizi yawe ya kiroho au kwa njia ya utume.

Kipengele kingine muhimu cha Karama yetu kinatokana na elimuroho ya Mt. Teresia wa mtoto Yesu na tunaweza kukiandika hivi: "kuweka saruji ya upendo duniani".  Ni upendo mkuu wa Mungu mwenye huruma unao "shuka kati ya watu na kuwavutia kwake ili kuwaongoza kuelekea mbinguni, kuwabadilisha kiundani na kuwaponya majeraha kwa faraja ya msamaha. Mtakatifu Teresia wa mtoto Yesu aliiishi kwa kina huruma hii na anasema hivi: “Mungu mwema amenijalia huruma yake isiyo na mipaka na kwa njia ya huruma hii naweza kutafakari na kuuabudu ukamilifu wote wa kimungu!  Hivyo, mambo yote nayaona yakiwa na miali ya upendo, hata haki nadhani imevishwa upendo. Ni furaha iliyoje kufahamu kwamba Mungu mwema ni Mungu wa haki anayeelewa mapungufu yetu na anaye fahamu udhaifu wa asili yetu ya kibinadamu"

 

Kwa kifupi huo ndiyo utambulisho wa karama wa Masista Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu, watawa wanaoishi kidugu katika maisha ya tafakari, kwa nia ya kuufanya ukarmeli ushamiri katika kila sehemu ya dunia, kwa njia ya kukarabati ubinadamu. Ninapo watakia heri na baraka tele kwa mwaka mpya 2019, nawakabidhi katika ulinzi wa Mwenye Heri Bikira Maria wa Mlima Karmeli, Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu msimamizi wa Shirika nchini Tanzania, pamoja na maombezi ya Waanzilishi wa Shirika: Mwenye Heri Maria Crocifissa na Padre Lorenzo, ili kwa maombezi yao tudumu sote katika mapendo kamili tukimtumikia Mungu na watu wake hasa kwa utakatifu wa maisha.

Masista Wakarmeli Tanzania

 

07 January 2019, 08:29