Tafuta

Muziki ni chombo cha imani, amana na utajiri katika maisha na utume wa Kanisa. Muziki ni chombo cha imani, amana na utajiri katika maisha na utume wa Kanisa. 

Kwaya ya Mt. Paulo wa Msalaba, Dodoma, Jubilei miaka 25 ya utume

Baba Mtakatifu Francisko anasema, nyimbo na muziki mtakatifu katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa zinawasaidia waamini kuzamisha Neno la Mungu katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Kimsingi anasema Baba Mtakatifu Francisko, muziki ni chombo cha imani, amana na utajiri mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa!

Na Rodrick Minja, - Dodoma & Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Muziki mtakatifu ni chombo cha ibada na uinjilishaji; ni amana na utajiri wa Kanisa; dhamana inayopaswa kutekelezwa kwa ibada, unyenyekevu na unyofu wa moyo! Hii inatokana na ukweli kwamba, nyimbo na muziki mtakatifu katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa zinawasaidia waamini kuzamisha Neno la Mungu katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Kimsingi anasema Baba Mtakatifu Francisko, muziki ni chombo cha imani, amana na utajiri mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa!

Dokta Alex Mshewe amewataka wanakwaya kote nchini Tanzania kutumia karama walizojaliwa na Mwenyezi Mungu katika kuinjilisha watu wa Mungu, ili kweli Mwenyezi Mungu aweze kupewa sifa na utukufu na mwanadamu aweze kutakaswa na kutakatifuzwa! Hayo ameyaeleza kwenye sherehe ya kutimiza miaka 25 ya Jubilei ya Kwaya ya Mtakatifu Paulo wa Msalaba Jimbo Kuu Katoliki Dodoma na uzinduzi wa Albamu ya nyimbo za Injili ijulikanayo kama “Mungu ni mwema”. Amesema kuwa kazi ya kuinjilisha ni ngumu sana kwani huwezi kuhubiri bila ya waimbaji. “Hubirini bila kuchoka kwa kutumia vipaji vyenu vya uimbaji na katu msikate tamaa kwani mwenyezi mungu aliyewapa tunu hizo laiwapa bure nanyi mnatakiwa kuzitumia na kuzitoa bure” aliongeza Dokta Mshewe.

Kwa leo hii ndugu zangu ambao umeona na kusherehekea miaka hii 25 ya Jubilei ya Kwaya ya Mtakatifu Paulo wa msalaba mnapaswa kujiuliza ni wapi mlikotoka na ni wapi mnakoenda na niwapi mlipo na baada ya kujiuliza hayo mtapaswa tena kujiuliza ni wapi mlipokosea, mlipofanikiwa ndipo muanze kujitafakari kwa kina ni nini  mnachopaswa kufanya. “Miaka 25 si haba kama kiatu cha raba  wengi walitamani kufikia siku hii lakini hawakuifikia kwa hiyo sisi tuliofanikiwa kuiona na kuishereheka Jubilei hii tunayo kila sababu ya kumshukuru mwenyezi mungu.” Aliongeza.

Kwa upande wake mgeni rasmi katika sherehe hiyo ya Jubilei ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa kwaya hiyo mwaka 1993 Padre Robert Kaiza, Mkuu wa Shirika la Marian Hills, Kanda Afrika Mashariki, aliwataka wanakwaya kote nchini Tanzania kujenga tabia ya kuwatembelea wagonjwa na kuwapa faraja na sio kuishia kuimba kwenye ibada tu. Padre Kaiza aliwataka kuhakikisha kuwa talanta walizojaliwa na mwenyezi Mungu wanazitumia kwa nguvu zote na vema na sio kuzitumia visivyo. Aliwataka kuhakikisha kuwa wanaondokana na makandokando ya dunia hususani ya migomo katika uimbaji.

“Mtakapofanya migomo hiyo migomo mnamgomea nani? Ni Padre au Mwenyezi Mungu? Mnapaswa kulitambua hilo na kulitafakari kabla ya kulitenda” alisema Padre Kaiza pia aliwataka wanakwaya kuendeleza umoja ambao utawasaidia katika kukua kwa kwaya yao. Aidha zaidi ya shilingi milioni kumi zilipatikana katika uzinduzi huo ikiwemo fedha taslimu na ahadi.

Kwaya Dodoma 25 Yrs.
03 January 2019, 13:00