Cerca

Vatican News
Jimbo kuu teule la Mbeya Tanzania hivi karibuni limepata Mashemasi wapya 6 tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake! Jimbo kuu teule la Mbeya Tanzania hivi karibuni limepata Mashemasi wapya 6 tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake! 

Jimbo kuu teule la Mbeya lapata Mashemasi sita wapya!

Mashemasi wanawekwa wakfu kwa ajili ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu. Ni mashuhuda wa utakatifu wa watu wa Mungu unaopata chimbuko lake katika maisha ya Sala za Kanisa, Tafakari ya Neno la Mungu na Nidhamu katika maisha ya Utii, Useja na Ufukara kama kielelezo makini cha ufuasi wa Kristo kwa njia ya maisha ya wakfu!

Na Thompson Mpanji, Mbeya & Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mashemasi hushiriki kwa namna ya pekee utume na neema ya Kristo Yesu. Sakramenti ya Daraja huwapa chapa isiyoweza kufutwa na hufananishwa na Kristo aliyejifanya Shemasi, yaani mtumishi wa watu. Dhamana na wajibu wa Shemasi katika maisha na utume wa Kanisa ni kuwa shuhuda na chombo cha Injili ya huduma na huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Shemasi ni mhudumu wa Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa kadiri ya sheria, taratibu na kanuni za Kanisa.

Mashemasi wanawekwa wakfu kwa ajili ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu. Ni mashuhuda wa utakatifu wa watu wa Mungu unaopata chimbuko lake katika maisha ya Sala za Kanisa, Tafakari ya Neno la Mungu na Nidhamu katika maisha ya Utii, Useja na Ufukara kama kielelezo makini cha ufuasi wa Kristo kwa njia ya maisha ya wakfu! Askofu Taricisius Ngalalekumtwa wa Jimbo Katoliki Iringa, Tanzania hivi karibuni ametoa Ushemasi kwa Mafrateri sita wa Jimbo kuu teule la Mbeya, katika Parokia ya Mtakatifu Anthony wa Padua.

Katika Wosia wake, Askofu Ngalalekumtwa amewataka Mashemasi kuwa ni vyombo vya sala inayofumbatwa katika unyenyekevu na uchaji wa Mungu; wawe ni watu wa huduma kwa watu wa Mungu, ili kuwaletea amani, upendo na utulivu. Wawe wadumifu katika mashauri ya Kiinjili yaaani: Ufukara, Utii na Useja. Mashemasi watambue kwamba, wao ni wasaidizi wakuu wa Maaskofu na Mapadre katika huduma ya Neno, Altare, ukarimu na upendo kwa watu wa Mungu. Wawe ni walimu hodari na mahiri katika Katekesi na Sakramenti za Kanisa. Mambo yote haya wayatekeleze kwa kuendelea kumuiga Kristo Yesu aliyekuja hapa duniani si kutumikiwa bali kutumikia na kutoa maisha yake ili yaweze kuwa ni fidia ya wengi.

Askofu Ngalalekumtwa amewataka Mashemasi wapya kuwa ni watu wenye bidii, ibada na uchaji wa Mungu; waaminifu na wenye furaha katika kuwatumikia watu wa Mungu, daima watoe kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; kwa njia ya sadaka na majitoleo ya maisha yao. Mashemasi wapya wawe ni vyombo vya uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Mashemasi wametakiwa kusali kwa imani na bidii, ili ulimwengu uweze kupata haki, amani na maridhiano pamoja na wokovu.

Askofu Taricisius Ngalalekumtwa wa Jimbo Katoliki Iringa, Amewaomba waamini kuendelea kuwaombea Mashemasi wapya, ili Mwenyezi Mungu akipenda, siku moja, aweze kuwateua kujongea Altare yake kama Makuhani, kwa mfano wa Melkisedek. Amewashuruku wazazi na walezi kwa kuwakabidhi kwa Kanisa ili waweze kuwa ni faraja kwa Kanisa na Taifa la Mungu katika ujumla wake. Mashemasi wapya ni: Alex Mwampashi na Benedikti Mwamlima kutoka Parokia ya Mlowo; Shemasi Joseph Mwakapila  wa Parokia ya Kyela; Shemasi Leonard Sing’ambi Parokia ya Lupa, Shemasi Mathayo Mwakasege Parokia ya Vwawa na Shemasi Yves Maouvi kutoka Parokia ya Itumba.

Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko ameunda Jimbo kuu Jipya ya Mbeya nchini Tanzania linaloundwa na Jimbo Katoliki la Mbeya, Jimbo Katoliki la Iringa na Jimbo Katoliki la Sumbawanga. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu ametemua Askofu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga kuwa Askofu mkuu wa kwanza wa Jimbo kuu la Mbeya nchini Tanzania. Kabla ya uteuzi huu, Askofu Nyaisonga ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, alikuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda. Jimbo kuu la Mbeya kwa sasa linaundwa na Parokia 48 zinazohudumiwa na Mapadre wa Jimbo 73, Mapadre watawa 15; lina watawa wa kiume 15 na watawa wa kike ni 299 kadiri ya takwimu za Kanisa kwa Mwaka 2018.

Kabla ya kuundwa kwa Jimbo kuu la Mbeya, Jimbo Katoliki la Iringa lilikuwa ni sehemu ya Jimbo kuu la Songea likiwa na Parokia 38, zinazohudumiwa na Mapadre wa Jimbo 72, Mapadre watawa 38, watawa wa kiume ni 332 na watawa wa kike ni 667. Jimbo Katoliki la Sumbawanga lilikuwa chini ya Jimbo kuu la Tabora likiwa na Parokia 21 zinazohudumiwa na Mapadre wa jimbo 53, Mapadre watawa ni 7; watawa wa kiume ni 71 na watawa wa kike ni 348.

Mashemasi Jimbo kuu la Mbeya
04 January 2019, 12:51