Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya lina laani vitendo vya kigaidi kwa nguvu zote! Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya lina laani vitendo vya kigaidi kwa nguvu zote! 

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya la laani vitendo vya kigaidi!

Maaskofu wanawaomba viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wadau wengine wote kuhakikisha kwamba, wanasaidia kufyekelea mbali sera za mauaji na badala yake, watu wakite nguvu kutafuta na kudumisha: haki, amani, utu na maisha ya binadamu. Wananchi wa Kenya washirikiane kwa karibu zaidi na vyombo vya ulinzi na usalama ili kudumisha amani na utulivu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Heri wapatanishi, maana hao watamwona Mungu! Hii ni sehemu ya Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake. Heri hizi zinatumiwa kwa wakati huu na Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya kama ujumbe wa matumaini na mshikamano na familia ya Mungu nchini Kenya baada ya kutikishwa na shambulizi la kigaidi lililotokea katika hoteli ya DusitD2 eneo la 14 Riverside Drive, Jijini Nairobi siku ya Jumanne, tarehe 15 Januari 2019. Shambulizi hili limesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Maaskofu wanawakumbuka na kuwaombea wale wote walioguswa na kutikiswa na vitendo hivi vya kigaidi.

Askofu mkuu Philip Arnold Subira Anyolo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, anapenda kuvipongeza vyombo vya ulinzi na usalama nchini Kenya, kwa ujasiri na utayari wao wa kupambana na magaidi pamoja na kuhakikisha kwamba, usalama na utulivu vinarejea tena katika eneo hili. Maaskofu wanawaombea ulinzi na tunza kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili waweze kutekeleza majukumu yao barabara, katika mchakato wa ulinzi wa wananchi na mali zao nchini Kenya. Wanawaombea ili waendelee kuboresha hali ya ulinzi na usalama nchini Kenya.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linawapongeza wananchi wote waliojitokeza kuwasaidia wahanga wa shambulizi hili kwa haraka; wafanyakazi katika sekta ya afya ambao wamefanya jitihada kubwa kuokoa maisha ya ndugu zao Wakenya. Wanawapongeza wananchi kwa kueneza ujumbe wa matumaini kwenye mitandao ya kijamii, iliyosaidia watu kujitokeza kwa wingi kuchangia damu kwa waathirika. Maaskofu wanasikitishwa sana na utamaduni wa kifo unaoendelea kushika kasi katika akili na nyoyo za watu kiasi hata cha watu kuthubutu kufanya mauaji bila woga wowote.

Maaskofu wanawaomba viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wadau wengine wote kuhakikisha kwamba, wanasaidia kufyekelea mbali sera za mauaji na badala yake, watu wakite nguvu kutafuta na kudumisha: haki, amani, utu na maisha ya binadamu. Wananchi wa Kenya washirikiane kwa karibu zaidi na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutambua kwamba, ulinzi na usalama wa Kenya uko pia mikononi mwao; watoe taarifa pale wanapohisi uwepo wa vitendo vinavyohatarisha amani na usalama wa raia na mali zao, ili viweze kuingilia kati mara moja! Maaskofu wanawaalika viongozi wa dini mbali mbali kusaidia mchakato wa kuganga na kuponya madonda haya kwa familia zilizoguswa na kutikiswa na vitendo hivi kwani itawachukua muda mrefu hata kuweza kupona! Kanisa kwa upande wake, litaendelea kushirikiana na Serikali kwa ajili ya kukuza  na kudumisha misingi ya haki, amani, utulivu, ustawi na mafao ya wengi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linapenda kuungamana na Jumuiya ya Kimataifa kulaani kwa nguvu zote vitendo vya kigaidi, ambavyo kwa mara nyingine tena, vimewagusa na kuwatikisa wananchi wa Kenya. Katika mazingira kama haya, familia ya Mungu inapaswa kushikamana ili kujenga na kudumisha umoja wa kitaifa. Ni muda wa kukataa sera za ukabila na udini usiokuwa na mashiko wala mvuto kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wa Kenya. Wananchi wasikubali siasa za utengano na migawanyiko katika misingi ya kijinsia, kidini na mahali anapotoka mtu. Familia ya Mungu nchini Kenya ijisikie kuwa wamoja na kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa watu na mali zao.

Maaskofu Kenya: Ugaidi

 

18 January 2019, 16:43