Cerca

Vatican News
Askofu mkuu Mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwaichi asema, vishawishi vikuu katika maisha ya mwanadamu ni: madaraka, uchu wa mali na heshima. Askofu Mkuu Mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwaichi asema, vishawishi vikuu katika maisha ya mwanadamu ni: madaraka, uchu wa mali na heshima. 

Dar Es Salaam: Vishawishi: Madaraka, mali na heshima!

Kishawishi cha kwanza ni madaraka, uchu wa mali na heshima. Vishawishi hivi pia vinaweza kuwakumba hata wakleri katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa. Hii inatokana na ukweli kwamba, hata wakleri wanapojongea na kupokea Daraja Takatifu, daima wanakuwa na: mitazamo, vionjo na ndoto zao zinazopaswa: kuchambuliwa, kutakaswa na kunyooshwa ili kukidhi maisha ya Daraja.

Na Joseph Peter Mosha & Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika maisha ya mwanadamu, vishawishi vikuu ni vitatu: kishawishi cha kwanza ni madaraka, uchu wa mali na heshima. Vishawishi hivi pia vinaweza kuwakumba hata wakleri katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa. Hii inatokana na ukweli kwamba, hata wakleri wanapojongea na kupokea Daraja Takatifu, daima wanakuwa na: mitazamo, vionjo na ndoto zao zinazopaswa: kuchambuliwa, kutakaswa na kunyooshwa ili yabaki yale tu yanayokidhi mahitaji na wasifu wa wito na maisha ya Daraja Takatifu.

Hili ni angalisho ambalo limetolewa na Askofu mkuu Mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania, Jumamosi, tarehe 5 Januari 2019 alipokuwa anatoa Daraja takatifu ya Ushemasi kwa Majandokasisi sita kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Anasema, hata Kristo Yesu kabla ya kuanza maisha yake ya hadhara alijitenga kwa muda wa siku arobaini ili kusali na kufunga na hatimaye Ibilis, Shetani akamjribu katika mambo hayo makuu matatu!

Askofu mkuu Mwandamizi Ruwa’ichi anaendelea kufafanua kwamba, vishawishi hivi vilioneshwa hata na Mitume wote wa Yesu, hata baadhi yao wakadiriki kumwomba awateuwe kuwa ni viongozi wakuu, jambo ambalo liliwakasirisha sana Mitume wenzao. Lakini, Yesu alitumia fursa hii kuwasahihisha kwa kuwakumbusha kwamba, maana ya ufuasi wa kweli inafumbatwa katika fadhila ya unyenyekevu na huduma ya utumishi kwa wote pasi na makuu na wala si katika mali, madaraka na heshima kadiri ya mtazamo na vionjo vya walimwengu!

Askofu mkuu Mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwa’ichi ametumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyewajalia Mitume wa Yesu hekima ya kuteuwa Mashemasi wa kwanza, watu maarufu, ili waweze kuwa wasaidizi wa Maaskofu na Mapadre katika maisha na utume wa Kanisa. Hawa walikuwa ni wahudumu wa Mafumbo ya Imani na Neno la Mungu kiasi hata cha kuyasadaka maisha yao kama ilivyotokea kwa Shemasi Stefano, Shahidi, shuhuda wa kwanza kuyamimina maisha yake kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Hata leo hii, Kanisa kwa njia ya Roho Mtakatifu linaendelea kutambua uhitaji wa Mashemasi katika maisha na utume wa Kanisa, ndiyo maana bado vijana: wema na wenye afya; akili na waadilifu; wanayofu na wakarimu wanaendelea kuitwa ili kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa. Waamini wanahamasishwa kuendelea kusali na kumwomba Roho Mtakatifu ili kweli Mashemasi waweze kutenda kazi na utume wa Kanisa kwa umakini mkubwa.

Askofu mkuu Mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwa’ichi ametumia fursa hii kufafanua dhamana na wito wa Mashemasi katika maisha na utume wa Kanisa. Kwanza kabisa wanapaswa kutambua kwamba, wanaitwa na kutumwa na Kristo Yesu mwenyewe, changamoto ni kuhakikisha kwamba, wanafanana na Kristo Mchungaji mkuu. Katika maisha na utume wao, wanaitwa kumtumikia Mungu pamoja na jirani zao: kwa kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu. Mashemasi baada ya masomo na majiundo ya kitaalimungu wanayo haki ya kutangaza Neno la Mungu kwa ufasaha na wametakiwa kuandaa kikamilifu Mahubiri yao ili kamwe watu wa Mungu katika safari yao ya kiimani, kimaadili na kiutu wasitindikiwe chakula cha njiani.

Mashemasi wamewekwa wakfu kuwa watumishi wa Altare, kwa kumsaidia Askofu na Mapadre, huku wakiendelea kujenga uelewa mpana katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, ili kwa wakati nao waweze kuyaadhimisha Mafumbo haya kwa ushiriki na uelewa mpana zaidi kama Mapadre. Mashemasi ni wahudumu wa Sakramenti ya Ubatizo na Ekaristi Takatifu; kwa kuwagawia waamini pamoja na kuwapelekea wagonjwa.

Askofu mkuu Mwandamizi Ruwa’ichi amewataka Wakleri kuwa makini katika kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa, vinginevyo, watashughulikiwa na Kanisa kama “chuma chakavu” kwa sababu ya kufuru. Hakuna sababu ya kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa haraka. Mashemasi katika maisha na utume wao, watasimamia na kubariki ndoa. Watakuwa ni wawakilishi wa Kanisa na Serikali, kumbe, wanapaswa kutambua kwamba, wanapaswa kupata kibali cha serikali ili kutimiza wajibu huu kwa ibada na uchaji wa Mungu.

Mashemasi wanayo pia dhamana ya kutoa mafundisho ya imani, maadili na Sakramenti za Kanisa, changamoto kubwa mbele yao ni kuhakikisha kwamba, wanajiandaa vyema kutekeleza dhamana na wajibu huu. Mashemasi pia ni wahudumu wa Injili ya huruma na mapendo kwa watu wa Mungu hasa kwa: maskini, wajane na watoto yatima. Mwishoni, Mashemasi kimsingi ni wasaidizi wakuu wa Askofu na Mapadre kadiri ya sheria, taratibu na kanuni za Kanisa. Mwishoni, Askofu mkuu Mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwa’ichi amewaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kuwaombea Mashemasi wapya, ili kazi aliyoanzisha Mungu ndani mwao, aweze kuikamilisha. Mashemasi wapya ni: Alset Oyubo Wakhaya; Shemasi David Joseph Ngate; Shemasi Gregory John Kijanga; Shemasi Jaime Vieira Anton Paim; Shemasi Murivan Medrado Brado pamoja na Shemasi Titus Edward Mwami.

Waamini wa Jimbo kuu la Dar Es salaam walikuwa na shahuku ya kusikia Padre Alister Makubi amepangiwa wapi baada ya kuhitimu na kufaulu masomo yake Roma na hatimaye, kurejea Jimboni mwake hivi karibuni! Padre Makubi ameteuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya Oysterbay, Jimbo kuu la Dar es Salaam na atakuwa pia Mtaribu wa Idara ya Shughuli za Kichungaji Jimbo kuu la Dar es Salaam. Wanoko wanasema, shida ya Parokia ya St. Peter’s pale ni Ibada za Kimombo! Yaani ninapofikia hapo, hata kwenda kumtembelea Paroko inakuwa ni shidaaaa! Wengine wanasema, Paroko itambidi apambane na Ibada za Kiingereza hadi kieleweke!

Mashemasi Dar es Salaam
05 January 2019, 15:45