Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè: 2018-2019: Kauli mbiu "Kamwe hatuwezi kusahau ukarimu" Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè: 2018-2019: Kauli mbiu "Kamwe hatuwezi kusahau ukarimu" 

Fra Alois: Utamaduni wa ukarimu unawezekana kabisa!

Maadhimisho ya Siku ya 41 ya Vijana wa Kiekumene kwa Mwaka 2018 yanayoongozwa na kauli mbiu “Kamwe hatuwezi kusahau ukarimu”. Hii ni mara ya kwanza kwa mji wa Madrid kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya Siku ya kiekumene ya Vijana Barani Ulaya ambayo kama kawaida yanaanza tarehe 28 Desemba 2018 hadi tarehe Mosi, Januari 2019.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Vijana wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè kutoka sehemu mbali mbali za Bara la Ulaya, wametinga timu mjini Madrid, Hispania kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya 41 ya Vijana wa Kiekumene kwa Mwaka 2018 yanayoongozwa na kauli mbiu “Kamwe hatuwezi kusahau ukarimu”. Hii ni mara ya kwanza kwa mji wa Madrid kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya Siku ya kiekumene ya Vijana Barani Ulaya ambayo kama kawaida yanaanza tarehe 28 Desemba 2018 hadi tarehe Mosi, Januari 2019.

Vijana hawa watapewa malazi na chakula na waamini kutoka katika Parokia 170, ili kuonja na kushiriki uwepo wa vijana wanaozama katika sala, ukimya na mchakato wa ujenzi wa urafiki kati ya vijana ili kuondokana na woga na wasi wasi usiokuwa na mvuto wala mashiko, unaoendelea kujengeka siku kwa siku hasa Barani Ulaya. Waamini wanakumbushwa kwamba, ukarimu ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu na kwamba, Mwenyezi Mungu daima anapenda kuwapokea watoto wake wanapomkimbilia kwa toba na wongofu wa ndani.

Kristo Yesu anaendelea kubisha hodi katika malango ya nyoyo za waamini, kwa wale walio tayari wanaweza kumfungulia malango yao na Yeye kupata nafasi ya kuingia na kukaa pamoja nao! Ili kufanikisha azma hii kuna haja ya kujenga na kudumisha imani na matumaini kwani utamaduni wa ukarimu ni jambo linalowezekana kabisa anasema Fra Alois, Mkuu wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè. Katika mkutano huu, wa sala vijana watawakumbuka na kuwaombea waathirika wa vitendo vya kigaidi sehemu mbali mbali za dunia, changamoto na mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya kukataa kwa nguvu zote kishawishi cha kutaka kutumbukizwa katika utamaduni wa kifo na badala yake, wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya uhai na wajenzi wa madaraja yanayowakutanisha watu kama anavyokaza kusema, Baba Mtakatifu Francisko.

Mkutano wa vijana wa Taizè unafumbatwa katika sala na mchakato wa ujenzi wa urafiki. Vijana watapata muda wa kusali, kutafakari na kukaa kimya, ili kujenga na kudumisha mahusiano mema na Kristo Yesu katika maisha yao. Watapata nafasi ya kusikiliza Neno la Mungu pamoja na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa, hasa zaidi kwa kukazia Sakramenti ya Upatanisho kati yao na Kristo Yesu; Upatanisho kati ya Wakristo na kati ya watu wa Mataifa, ili hatimaye, kujenga urafiki unaovuka mipaka ya jiografia kitaifa.

Fra Alois anasema, hii ni fursa ya kusikiliza na kuandamana na vijana wa kizazi kipya katika hija ya maisha yao, changamoto na mwaliko uliotolewa na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa mwaka 2018 ambayo alibahatika kushiriki. Wanataka kuwasaidia vijana kugundua Kanisa kuwa ni mahali pa ujenzi wa urafiki na tunu msingi za maisha ya kifamilia; ni mahali pa kurutubisha imani, matumaini na mapendo ya kweli, ili kujenga utandawazi unaofumbatwa katika tunu msingi za maisha ya Kikristo na kiutu! Hii ni fursa ya vijana kutembea kwa pamoja, kufahamiana, kushirikiana na kusaidiana kama ndugu hata kama wanatoka katika Makanisa tofauti duniani.

Taizè 2018-2019

 

 

 

27 December 2018, 13:33