Tafuta

Vatican News
Jumuiya ya kiekumene ya Taize katika mkutano wa  sala huko Madrid Jumuiya ya kiekumene ya Taize katika mkutano wa sala huko Madrid  

Tveit(Wcc):Ukarimu wa makaribisho unaweza kuokoa maisha!

Kukaribisha ni mtindo wa upendo ulio mkubwa na ambao lakini haujatambuliwa. Ni maandishi ya Ujumbe wa Katibu Mkuu wa Baraza la Makanisa duniani, mchungaji Olav Tveit (Wcc) kwa vijana wa Ulaya wanaoshiriki Mkutano wa Jumuiya ya kiekumene Taize jijini Madrid nchini Uhispania uliofunguliwa 28 Desemba na utamalizika Mosi Januari 2019

Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Kukaribisha ni mtindo wa upendo ulio mkubwa na ambao hautambuliwi. Anaadika Katibu Mkuu wa Baraza Makanisa duniani mchungaji Olav Tveit (Wcc) katika ujumbe aliowaelekeza washiriki wa Mkutano wa vijana Ulaya ulioandaliwa na Jumuiya ya kiekuemene Taize Mkutano uliofunguliwa  tarehe 28 Desemba jijini  Madrid nchini Uhispania  unaoongozwa na mada,“Usisahau makaribisho”.

Jumuiya ya taize inawakilisha vema maana ya uekumene

 Makaribisho siyo suala la fadhila iliyomo ndani mwetu tu, bali hata  yanaingia katika mahusiano ya kukaribisha, kupokeana na kujenga urafiki wa kweli na wa kuaminiana wakati wa kushirikishana chakula na malazi. Makaribisho ni hatua muhimu sana na lakini pia  iliyo na hatari wakati mwingine, anaandika mchungaji Tveit, ambapo anafikiri kuwa, kukaribisha pia  ni karama maalum ya jumuiya ya kiekumene ya Taize, jumuia ambayo inawakilisha vema nini maana ya chama hicho cha Uekumene.

Tunageuka kuwa nyumba yetu hapa duniani kwa mwaliko wa Mungu

Kukaribisha wengine katika nyumba zetu ina maana ya kuwaalika katika mioyo yetu. Anaendelea kuandika mchungaji Tveit na kwamba pia ni wito msingi katika Biblia na ni sura yenyewe na uwepo wa Mungu kwa maana Mungu ni nyumba yetu, haijalishi tunamoishi au tunakwenda wapi kwa maana sisi wenyewe tunageuka kuwa nyumba ya Mungu hapa duniani.

Upendo huo wa kukaribishana  ambao tumepewa bure na kwa namna ya unyenyekevu, unahitajika sana katika nyakati zetu leo hii. Anasema hayo akiwakumbuka wahamiaji na wakimbizi, wasio kuwa na makazi na  wenye kuhitaji, hata ambao kiurahisi ni tofauti na sisi. Makaribisho yetu mema yanaweza kuokoa maisha, kuunda jumuiya, hata kuokoa wakati wetu. Kwa maana hiyo Mchungaji Tveit  kwa vijana waliokusanyika Madrid anawapa angalisho la kuwa makini kwa chama hiki cha Kiekumene kwa maana ni chama cha  upendo na si tu kwa wakati ujao bali kuanzia hata sasa.

Bila uzoefu wa kukutana haiwezekani kujenga Ulaya

Wakati huo huo naye Askofu Mkuu wa Madrid  Kardinali Carlos Osoro akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa vijana  amesema: “uzoefu wa kidugu, kugundua mwingine  kuwa ni ndugu, kwa sababu Mungu yupo ndani mwake na mwangu na anatupenda, ndiyo ujumbe muhimu wakati huu kwa vijana wakristo wa Ulaya. Na huo ndiyo ujumbe ambao Bara la kizamani la Ulaya linataka kuwaleza vijana wote wa Ulaya wanaoudhuria mkutano huo, ulioandaliwa na Jumuiya ya Kiekumene ya  Taize katika mji uliojengwa na watu wote wanaotoka nchini Uhispania na sasa kutoka dunia nzima!

Kardinali ambaye pia ni mdau wa mikutano hii, kwani katika miaka ya 60  hata yeye mwenye alikuwa anakwenda katika jumuiya ya Taize Ufaransa. Kwa maana hiyo anathibitisha kuwa, kuna umuhimu wa mkutano huo kwa sababu ya ukimya na kusikiliza. Hivi ni viungo viwili ambavyo vikikosekana, huwezi kumpata Mungu na wala ndugu. Ni hali ambayo inamsaidia mtu kukutana na kuingia binafsi kwa ukina wa moyo wa kujitafiti wewe ni nani na ni kitu gani tunafikiria. Kwa kufanya hivyo ndipo inazaliwa hata sala ya Baba Yetu, inayotufundisha kushikamana na ndugu kama anavyotukambatia Mungu Baba. Kardinali Osoro anasema bila uzoefu huo haiwezekani kujenga Ulaya, na bila kufanya hivyo   watagawanyika kila mmoja katika eneo lake na mipaka yake, bila kuwa na madaraja ambayo Bwana anaomba kila mmoja ajenge, kwa utambuzi kuwa kila kaka na dada ni ndugu kuanzia jinsi anavyofikiri. Na iwapo itafikia hatua hiyo ya udugu ni hakika kuwa dunia utabadilika.

28 December 2018, 14:32