Vatican News
Biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu! Biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu!  (AFP or licensors)

Biashara haramu ya binadamu ni uhalifu dhidi ya ubinadamu!

Jumuiya ya Kimataifa inakabiliana na uvunjifu mkubwa wa haki msingi za binadamu kutokana na: vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, kidini na kikabila; Umaskini wa hali na kipato; uhalifu unaofanywa na magenge ya uhalifu kimataifa; mifumo ya utumwa mamboleo, biashara ya binadamu na viungo vyake; yote haya ni mambo yanayonyanyasa na kudhalilisha utu wa binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina katika tamko lake kama sehemu ya maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 70 ya Tamko la Haki Msingi za Binadamu na Miaka 25 ya Tamko la Vienna linasema, biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni kati ya matukio makubwa yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu na kwamba, huu ni uhalifu dhidi ya ubinadamu na uvunjaji mkubwa wa haki zake msingi.

Leo hii, Jumuiya ya Kimataifa inakabiliana na uvunjifu mkubwa wa haki msingi za binadamu kutokana na: vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, kidini na kikabila; Umaskini wa hali na kipato; uhalifu unaofanywa na magenge ya kitaifa na kimataifa; mifumo mipya ya utumwa mamboleo, biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; yote haya ni mambo yanayonyanyasa na kudhalilisha utu na heshima ya binadamu sehemu mbali mbali za dunia.

Kwa upande wake, Rais Sergio Mattarella wa Italia katika tamko lake kwa vyombo vya habari anakaza kusema, Tamko la Haki Msingi za Binadamu ni kielelezo cha ustaarabu wa binadamu na rejea muhimu kwa Jumuiya ya Kimataifa. Utunzaji wa haki msingi za binadamu ni dhamana na wajibu wa kimaadili unaopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, bado kuna uvunjifu mkubwa wa haki msingi za binadamu.

Kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe kulinda na kudumisha misingi ya uhuru; kwa kuheshimu usawa wa binadamu, utu na heshima yake. Rais Mattarella anasema, Italia kuanzia mwezi Januari, mwaka 2019 itakuwa ni nchi mwanachama katika Baraza la Haki Msingi za Binadamu la Umoja ili kuendeleza wajibu huu wa kimaadili; kwa kuzuia vita na ghasia, ili hatimaye kujenga jamii inayojikita katika amani, usalama na maendeleo fungamani ya binadamu!

Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Ulaya, “Justitia et Pax Europa” katika tako lake kwa ajili ya maadhimisho haya inasema, Tamko la Haki Msingi za Binadamu ni zawadi kwa binadamu wote. Kila mtu anahamasishwa kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu, lakini dhamana hii inapaswa kutekelezwa kwa umakini mkubwa na viongozi pamoja na taasisi zilizopewa dhamana ya kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu. Tamko la Vienna na Mafundisho Jamii ya Kanisa ni nyenzo msingi katika kudumisha utu na heshima ya binadamu; kwa kuwa na sera na mipango thabiti ya maendeleo fungamani; demokrasia shirikishi na utawala wa sheria unaozingatia haki msingi za binadamu na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Uhuru wa kujieleza, uhuru wa kidini, uwezekano wa kupata tiba, elimu na makazi bora ni mambo ambayo bado yanaendelea kuwa ni changamoto kubwa kwa mataifa mengi duniani.

Biashara ya Binadamu

 

11 December 2018, 15:14