Tafuta

Vatican News
Shirika la Masista wa Maria Immakulata, SMI, Tanzania lazindua Mwaka wa katiba: Lengo ni utakatifu wa maisha! Shirika la Masista wa Maria Immakulata, SMI, Tanzania lazindua Mwaka wa katiba: Lengo ni utakatifu wa maisha! 

Shirika la Masista wa B. M. Imakulata, SMI Tanzania: Mwaka wa Katiba

Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili kwa mwaka 2018, imekuwa ni fursa ya kuzindua Mwaka wa Katiba, kama chachu ya kuimarisha maisha ya umoja, udugu, upendo na msamaha tunu msingi katika kuchuchumilia utakatifu wa maisha. Katiba ni sheria mama inayowaongoza katika maisha na utume wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kristo Yesu ni amani ya watu wake na dunia katika ujumla wake. Yesu ndiye mkuu wa amani ya kimasiha. kwa Damu yake Azizi pale Msalabani, amevunjilia mbali uadui na hivyo, amewapatanisha watu na Mungu na amelifanya Kanisa lake kuwa Sakramenti ya umoja wa ubinadamu na ya umoja wake na Mungu. Hii ni changamoto ya kutafakari juu ya tunu zinazojenga utu: umoja, haki, amani na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wake. Viongozi wanapaswa kusimamia: ustawi wa watu wanaowaongoza; kutenda kwa hekima na haki; kulinda, kudumisha umoja, pamoja na kustawisha amani. Maandiko Matakatifu yanamuweka Kristo kama mfano ambao viongozi wote wanaopaswa kujifunza namna ya kuyatimiza hayo, daima watu watambue kwamba, cheo ni dhamana na uongozi ni huduma.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mheshimiwa Sr. Maria Agnes J. Mwanajimba, aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa Mama mkuu wa kwanza mzalendo kwa upande wa Shirika la Masista wa Maria Immakulata, SMI nchini Tanzania. Itakumbukwa kwamba, Shirika hili lilianzishwa kunako mwaka 1854 na Padre Yohane Schneider, wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, ndiyo maana, akawekwa kuwa ni mlinzi na msimamizi wa Shirika. Masista wa Shirika hili waliingia nchini Tanzania kunako mwaka 1972 na hadi sasa kuna jumla ya watawa 81 wazalendo na 5 wamisionari kutoka Poland wanaotekeleza dhamana na utume wao sehemu mbali mbali za Tanzania.

Sr. Maria Agnes J. Mwanajimba, katika hotuba yake ya kwanza, amewashukuru wanashirika wenzake na kwamba, amekipokea “Kikombe hiki” kama sadaka ya upendo wa Fumbo la Msalaba, linaloweza kufahamika tu, kwa njia ya macho ya imani. Anasema, Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alishughulikia mahitaji halisi ya watu wake, aliwajali, aliunganisha makundi yasiyopatana na akajitoa sadaka Msalabani ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.  Yesu ni Mfalme wa amani na amani ya walimwengu, changamoto ni kujikita katika tunu msingi za maisha ya Kiinjili ili kudumisha matunda ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kweli.

Sr. Mwanajimba anasema, waamini wanakumbushwa kwamba, uongozi ni huduma  na sadaka kwa ajili ya watu wa Mungu. Ili kuweza kutoa huduma hii kikamilifu, kuna haja ya kuwa na toba na wongofu wa kimisionari, kusoma alama za nyakati, sanjari na kudumisha umoja na udugu katika maisha ya kitawa! Lengo kuu ni kuinjilisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Amewaomba watawa wenzake kumsindikiza katika maisha na utume wake mpya kwa njia ya sala na sadaka zao, ili, aweze kulitumikia Shirika nchini Tanzania katika kipindi hiki cha mpito kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2019.

Sr. Mwanajimba katika mahojiano maalum na Vatican News anasema Maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili kwa mwaka 2018, imekuwa ni fursa ya kuzindua Mwaka wa Katiba, kama chachu ya kuimarisha maisha ya umoja, udugu, upendo na msamaha tunu msingi katika kuchuchumilia utakatifu wa maisha. Katiba ni sheria mama inayowaongoza katika maisha na utume wao; kwa kufumbata mashauri ya Kiinjili, maisha ya kijumuiya na maisha ya kiroho kadiri ya karama ya mwanzilishi wa Shirika. Maadhimisho ya Mwaka wa Katiba yanaongozwa na kauli mbiu “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38.

Lengo la Mwaka wa Katiba ni kutaka kumuiga Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili aliyekubali kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha yake. Shirika la Masista wa Maria Immakulata, SMI katika maisha na utume wake nchini Tanzania wanataka kumuiga Bikira Maria, kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu; utakatifu wa maisha yao na wokovu wa walimwengu! Tangu mwaka 1972 Masista wamekuwa wakifanya kazi nchiniTanzania na kutimiza wosia wa Mwanzilishi: “Fanya hima kuokoa roho ambazo zimesimama katika ncha ya maadili yaliyopotoka, hurumieni shida za mabinti”. Kituo chao cha kwanza cha kazi za kitume kilikuwa ni Kilimarondo. Mwaka 1976 nyumba ya pili ilifunguliwa Nanjota, Jimbo Katoliki la Mtwara, Kusini mwa Tanzania karibu na mpaka wa Msumbiji.

Toka mwanzo kabisa Masista wameelekeza nguvu zaidi katika dhamira ya shirika kwa kufanya kazi pamoja na wasichana, wanawake na watoto. Wanaongoza shule za awali za watoto wadogo, wanatoa mafundisho ya dini shuleni, wanafundisha kushona, kazi za mikono, mapishi, kuwatunza wagonjwa hospitalini na huduma ya afya ya mama na mtoto. Baada ya muda nyumba ya Kilimarondo imefungwa. Kwa sasa Masista wa Maria Immakulata wanafanya kazi huko Chikukwe kwa ajili ya malezi ya wanavosi na hapa ndiyo nyumba mama. Huko Nanjota: Jimbo la Tunduru-Masasi ni kwa ajili ya malezi ya waombaji na wapostulanti; Jimbo Katoliki la Mtwara. Makao makuu ya Shirika yako Kurasini, Jimbo kuu la Dar es Salaam na hapo pia wanafanya utume katika Ubalozi wa Vatican nchini Tanzania. Masista hawa wako Jimbo la Morogoro. Jimboni Same wanaendesha shule ya Sekondari na kufundisha katekesi. Katika Jimbo kuu la Dodoma wanasaidia huduma hospitalini, shule ya msingi, chekechea pamoja na kufundisha katekesi.

Sr. Mwanajimba anasema katika ulimwengu mamboleo kuna mijeledi isiyo na idadi: ulevi wa kupindukia na kubobea katika matumizi haramu ya dawa za kuleva, vijana kukengeuka na kutopea katika maadili na utu wema. Kumbe, Masista wa Maria Imakulata wamejiingiza katika shughuli za mafungo ya kiroho, “siku za tafakari” kwa vijana pamoja na huduma kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Masista wa Maria Immakulata wanajitahidi kufuata sauti ya Mwenyezi Mungu, wanatambua wito wao na kutimiza majukumu yao ambayo wamekabidhiwa katika utume na shughuli za Shirika. Wanaipeleka huduma yao kwenye nyumba za wazee, makazi ya watu, na hospitali. Vilevile wanawasaidia kazi za Mapadre. Wanafundisha dini shuleni na kuongoza makundi ya vijana hasa wasichana.

Shirika B. M. Immaculata, SMI
20 December 2018, 11:38