Tafuta

Vatican News
Mkutano wa SECAM 2018: Wakimbizi na Wahamiaji; Biashara haramu ya binadamu na viungo vyake! Mkutano wa SECAM 2018: Wakimbizi na Wahamiaji; Biashara haramu ya binadamu na viungo vyake!  (AFP or licensors)

SECAM Inajadili kuhusu: Wakimbizi na Biashara ya binadamu!

SECAM inataka kutekeleza kwa dhati Sera za Uhamiaji Barani Afrika katika Kipindi cha Mwaka 2018-2030. Inaendelea kupembua Itifaki ya uhuru wa watu na mizigo Barani Afrika pamoja na Mkataba wa “Global Compact 2018” yaani “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018” unaopania pamoja na mambo mengine kukomesha ubaguzi na maamuzi mbele.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kila mwaka kuna mamilioni ya watu wanaotumbukizwa katika mifumo ya utumwa mamboleo, hususan katika kazi za suluba, utalii wa ngono na biashara haramu ya binadamu na viungo vyake. Kashfa hii imeanza kuzoeleka kati ya watu, kiasi kwamba, inaonekana kuwa ni jambo la kawaida katika maisha. Lakini, huu ni ukatili dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Kutokana na kukosena kwa fursa halali za uhamiaji, Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema, watu wengi wanajikuta wakihatarisha maisha yao kwa kujitumbukiza hata katika mitego haramu inayohatarisha maisha, utu na heshima yao kama binadamu.

Matokeo yake ni wahamiaji na wakimbizi kutumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Makundi ya kigaidi na magenge ya uhalifu wa kimataifa yanatumia njia za wakimbizi na wahamiaji kujipatia fedha haramu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na wadau mbali mbali kujizatiti katika mapambano ya utumwa mamboleo na mifumo yake yote, kwa kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu!

Tume za Haki, Amani na Maendeleo Fungamani kutoka katika Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM kuanzia tarehe 5-9 Desemba 2018 zinafanya mkutano huko Abijan, Pwani ya Pembe, kujadili kuhusu mbinu mkakati wa kuragibisha miundombinu ya Kanisa mintarafu changamoto kubwa ya wahamiaji, wakimbizi pamoja na biashara haramu ya binadamu, ili kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu. Lengo la mkutano huu ni kuendelea kuelimisha familia ya Mungu Barani Afrika kutambua kuhusu uhamiaji haramu na madhara yake; kuimarisha mchango wa Kanisa katika kudhibiti wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji pamoja na kuwasaidia kadiri ya mbinu mkakati uliobainishwa na Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani:  “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea, kwa kuwapatia hifadhi na usalama wa maisha! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, sera na mikakati hii inamwilishwa pia kwenye Makanisa mahalia, ili kuwasaidia watu hawa ambao mara nyingi wanajikuta wakitumbukia katika biashara ya binadamu, utumwa mamboleo na aina mbali mbali ya nyanyaso dhidi ya utu na heshima yao.

SECAM inataka kuelimisha familia ya Mungu Barani Afrika kutambua madhara makubwa yanayotokana na uhamiaji haramu, ili kupata mapendekezo na maamuzi yanayoweza kufanyiwa kazi katika muktadha wa Bara la Afrika. SECAM inataka kutekeleza kwa dhati Sera za Uhamiaji Barani Afrika katika Kipindi cha Mwaka 2018-2030. Inaendelea kupembua Itifaki ya uhuru wa watu na mizigo Barani Afrika pamoja na Mkataba wa “Global Compact 2018” yaani “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018” unaopania pamoja na mambo mengine kukomesha ubaguzi na maamuzi mbele; kuongeza fursa za ushirikishwaji wa wahamiaji katika maisha ya nchi wahisani; sanjari na kupunguza gharama za kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji ambazo kwa sasa umekuwa ni mzigo mkubwa kwa nchi wahisani.

SECAM: Wakimbizi 2019
04 December 2018, 10:00