Cerca

Vatican News
Askofu Nkwande: Tunzeni Injili ya uhai na kudumisha: utu na heshima yenu kama binadamu! Askofu Renatus Nkwande: Tunzeni Injili ya uhai na kudumisha: utu na heshima yenu kama binadamu!  (Vatican Media)

Askofu Nkwande: Tunzeni uhai na kuheshimu utu wenu!

Kutamani jinsia tofauti na ile Mungu aliyokuumbia, ni kufuru kwa Mwenyezi Mungu. Leo hii wapo wanaothubutu kufanya upasuaji ili kubadili jinsia zao. Wapo wanaofanya majaribio ya kimapenzi kati ya wanaume kwa wanaume, na kati ya wanawake kwa wanawake. Haya ni majaribio ya kumkosoa aliyekupatia zawadi bila mastahili yako.

Na Askofu Renatus Nkwande, - Mwanza.

Utangulizi: Wapendwa wana wa Mungu, katika adhimisho hili la mkesha wa sikukuu ya Noeli, ni furaha kubwa kuona kwa mara nyingine tena, tunasherekea kwa pamoja fumbo la kuzaliwa Masiha Immanueli, yaani Mungu pamoja nasi. Ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu mwenyewe kuchukua mwili na kufanana na mwanadamu hali akibaki na umungu wake pia. Maamuzi hayo anayachukua Mungu, ili apate kumrudishia mwanadamu tunu ya uzima wa milele, tunu ambayo mwanadamu aliipoteza kwa dhambi ya asili. Napenda tutafakari kwa pamoja juu ya utambulisho wetu (identity), na juu ya zawadi ya uhai ambavyo Mwenyezi Mungu anatutunuku.

Zawadi ya Utu, Utambulisho: Mungu amemuumba mwanadamu kwa hadhi ya juu, ambapo alipenda mwenyewe afanane naye. Anaposema: na tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu (Rej., Mwanzo 1:26), Mungu analenga katika utu wa mwanadamu, yaani akili na utashi vinavyompa uwezo mwanadamu kufikiri, kuchanganua na kutambua jema na ovu, kisha kuchagua. Mwanadamu kaumbwa kwa hulka ya kupendelea lililo jema katika kuchagua. Hata hivyo Ibilisi humshawishi mwanadamu achague lililo baya. Katika hali ya namna hii, mwanadamu huachwa huru kuchagua mwenyewe lipi la kutenda au kutotenda. Mungu anaporuhusu vishawishi anaviruhusu vinavyoendana na akili na utashi wa mwanadamu kuvishinda, na zaidi sana, kama asemavyo mtume Paulo: lakini pamoja na lile jaribu, Mungu hufanya na mlango wa kutokea, ili tuweze kustahimili majaribu (Rej., IWakoritho 10:13).

Katika kumuumba mwanadamu, Mwenyezi Mungu alimuumba mtu mke na mtu mume (Rej., Mwanzo 1:27). Tunaposoma katika lile simulizi la pili la uumbaji, tunaona Mungu anapoamua kumfanyia Adamu msaidizi. Bwana haoni wa kufanana naye, wala kumfaa kati ya wanyama, ndege na viumbe vingine vyote (Rej., Mwanzo 2: 18-20). Naye msaidizi aliyemfanyia, hakuwa tena mwanamume wa kufanana mpaka maumbile, bali alimuumbia mwanamke, ndiye aliyeona anamfaa. Zawadi hii ya maumbile ya kike na ya kiume, vinayoendana na hulka na tabia za kiume na za kike, ni zawadi inayostahili kuheshimiwa, kutunzwa na kuendelezwa.

Kutamani jinsia tofauti na ile Mungu aliyokuumbia, ni kufuru kwa Mwenyezi Mungu. Leo hii wapo wanaothubutu kufanya upasuaji ili kubadili jinsia zao. Wapo wanaofanya majaribio ya kimapenzi kati ya wanaume kwa wanaume, na kati ya wanawake kwa wanawake. Haya ni majaribio ya kumkosoa aliyekupatia zawadi bila mastahili yako. Kufuru ya namna hii inapaswa kukemewa na kila mmoja katika taifa letu na ulimwengu kwa ujumla.

Kila kiumbe, kila kiungo na kila maumbile vina malengo yake. Lazima vitumiwe kadiri ya malengo yake Yeye aliyeviumba, na siyo kubadili matumizi kadiri unavyojisikia. Kubadili mpango wa uumbaji na kujidhania wewe unayo mamlaka ya kufanya hivyo, ni ishara ya kukengeuka. Huku ni kupoteza utambulisho wetu wanadamu (our identity). Huku ni kupoteza mwelekeo wa maisha na kujishusha sana thamani, sababu akili na utashi wetu, ulio sura na mfano wa Mungu, hatuvitumii kwa namna ambayo imenuiwa na Mungu mwenyewe. Thamani yako mwanadamu lazima uitambue, uienzi na uishi kuendana na thamani hiyo uliyozawadiwa na Muumbaji.

Katika masimulizi hayo ya uumbaji, tunaona viumbe vyote vinaumbwa kwa Neno wa Mungu, lakini zaidi sana kwa mwanadamu kuna nyongeza ya thamani tunayopaswa kuizingatia. Nyongeza hiyo ni pumzi ya uhai. Tunasoma katika ile sura ya pili, mstari wa saba wa kitabu cha Mwanzo kwamba: Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai, mtu akawa nafsi hai (Rej., Mwanzo 2:7).

Zawadi ya Uhai, Uzima: Pumzi hiyo tuliyopokea kutoka kwake Mwenyezi Mungu, inatufanya kuwa washiriki wa umungu huo. Hivyo uhai wa binadamu ni mtakatifu, sababu ni pumzi inayotoka kwa Mungu Mwenyewe. Naye mwanadamu anaumbwa na kuwa binadamu, tangu sekunde ile anapotungwa mimba na kuwa kiumbe hai ndani ya tumbo la uzazi la mama yake. Hapa kuna mambo kadhaa ningependa tukumbushane na kuyakemea yale yanayokwenda kinyume. Uhai huo tunaoshirikishwa wanadamu, tunapaswa kuutunza kwa hali na mali mpaka pale Bwana mwenyewe atakapopenda kumchukua mwanadamu huyo kwa kifo asilia. Hivyo utoaji mimba na mauaji ya namna yeyote, ni dhambi kubwa tunayopaswa kuiepuka na kuikemea kwa nguvu zote.

Mtoto Yesu anazaliwa kati yetu, na kuchukua hali yetu, ili kuinua tena thamani ya uhai tulionao wanadamu, kututakasa na kutufundisha namna ya kuuishi ubinadamu wetu. Wazazi, walezi, wahudumu wa afya, madereva, waajili na kila mmoja mwenye nafasi ya kuzingatia, kutunza na kuhudumia uhai, wafanye hivyo kwa moyo wa upendo na kuuthamini uhai wa kila mwanadamu bila ubaguzi wa umri, jinsia, kimo, maumbile, hali ya kiuchumi, mkondo wa dini wala siasa, ama tabaka la aina yeyote. Utungaji mimba na taratibu za mtoto kuzaliwa vifuate mipango na mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Hata leo hii, ni Mungu Mwenyewe ndiye anayeumba. Wanadamu wanashirikishwa tu uumbaji huo. Hivyo panapokuwa na ugumu wa kushika mimba, wana familia husika watumie njia sahihi kuchunguza afya zao na kufuata tiba zilizo na maadili. Wayatende hayo yote huku wakiendelea kumwomba Yesu mwenyewe aliye Bwana wa uhai, na ambaye vitu vyote vinaumbwa kupitia yeye (Rej., Yohane 1:4).

Kristo anapozaliwa leo katika mioyo yetu, katika familia zetu, jumuiya zetu, parokia zetu, na katika jamii yetu kwa ujumla, tuwe na utambuzi wa zawadi na thamani ya uhai huo. Tuwe jasiri kuikili imani hiyo hata mbele ya wasioamini hilo, au waliokengeuka na kufuata mienendo ya kukufuru. Tujitambue na kukiri kwa imani kama anavyofanya Paulo mtume mbele ya mkusanyiko wa wasioamini katika Areopago kule Athene kwamba: ndani yake Yeye Kristo Yesu tunaishi, tunakwenda na kuwa na uzima wetu (Rej., Matendo 17:28). Tuwatetee wanyonge, na tupaze sauti zetu bila kukoma kwa ajili ya haki ya kila mmoja. Hivyo tunakemea wale wote wanaoshiriki kwa namna moja ama nyingine kupandikiza mbegu na mayai ya binadamu ili kukuza mtoto katika chupa. Sayansi na teknolojia havipaswi kupingana wala kukufuru dini, bali kwa pamoja vinapaswa kuitafuta hekima ya kimungu ya uumbaji, na kuyatenda yote kadiri ya mapenzi yake Mungu mwenyewe.

Mtoto Yesu anazaliwa katika familia na analelewa na kukuzwa katika familia. Mapenzi ya Mungu tangu kuumbwa kwa ulimwengu, hata kwa fumbo la umwilisho, amependa pia Kristu azaliwe na aishi katika familia. Jamii yetu leo inakosa kuona thamani ya zawadi hiyo ya familia. Vijana wengi wanakwepa kufunga ndoa, wanakwepa majukumu, wanakwepa changamoto za ndoa na familia, wanakwepa uhalisia wa maisha. Lakini tujifunze kutoka kwa mtoto Yesu, anayekubali kuzaliwa kati ya wanadamu kadiri ya utabiri wa manabii kwamba: bikira atachukua mimba naye atazaa mtoto mwanamume, mtoto huyo watamwita Immanueli (Rej., Isaya 7:14; Mathayo 1:23). Lakini alifahamu pia yatakayompasa baadae kuyapitia mateso ya msalaba (Rej., Isaya 50: 5-7), bado alikubali kuyakabili yote.

Hivyo vijana na wote wanaoishi kinyume na maadili ya ndoa na familia, ni mwaliko kubadilika katika siku kuu hizi za Noeli. Mzibue masikio yenu, muivae nuru ya matumaini ya mtoto Yesu na kuyakabili yote kwa ajili wokovu wa wanadamu na sifa na utukufu wa Mungu. Mfanye hivyo bila kuwa wakaidi, bila kuona fedheha, bila kutelekeza familia, mke/mme, bila kutelekeza watoto, bali tutetee haki za wanyonge. Kwa namna hii wote wataweza kuiona haki ya mtoto Yesu iking’ara, na kumruhusu kuwa kweli ndiye mtawala wa maisha yao, ili maisha hayo yarudishiwe thamani yanayoistahili.

Hitimisho: Nimatumaini yangu ya kwamba, wengi wetu tumejiandaa kwa namna mbali mbali kuadhimisha sikukuu hii ya Noeli. Tumejiandaa kimavazi, chakula, kimwili, ibada za maungamo na kadhalika. Tunapoadhimisha Noeli hii katika Jubilei ya miaka 150 ya Ukristu wetu, tuoneshe sasa ukomavu na utofauti wa vizazi vilivyotutangulia na kizazi tulichopo leo. Isiwe tu sikukuu ya kula na kunywa, bali haswa sikukuu ya kuenzi na kutunza thamani ya utu wetu na uhai wetu wanadamu, ili kwa hakika tuweze siku moja kuurithi ule uzima wa mbingu na kuziimba fadhili za Bwana milele (Rej., Zaburi 89:1-2).

Nawatakieni nyote mliopo hapa, na Taifa zima la Tanzania, Sikukuu njema za Noeli!

Alleluya… Mtoto Yesu Amezaliwa!

Tumsifu Yesu Kristo

25 December 2018, 16:16