Tafuta

Vatican News
SEDAC: Maandalizi ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 yanaendelea vyema! SEDAC: Maandalizi ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 yanaendelea vyema! 

SEDAC: Maandalizi ya Siku ya Vijana Duniani 2019 yapamba moto!

Wajumbe wa mkutano huu wa SEDAC pamoja na mambo mengine, wamepembua kwa kina na mapana matumaini, matatizo, changamoto na matamanio halali ya vijana kama yalivyopembuliwa na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana kwa mwaka 2018 kwa kufanya rejea kwa vijana wanaotoka Amerika ya Kati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sekretarieti Kuu ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Amerika ya Kati, SEDAC, hivi karibuni imehitimisha mkutano wake wa mwaka huko Honduras, uliokuwa unaongozwa na kauli mbiu “Farijianeni na kusaidiana kama mnavyofanya hadi sasa”. Wajumbe wa mkutano huu pamoja na mambo mengine, wamepembua kwa kina na mapana matumaini, matatizo, changamoto na matamanio halali ya vijana kama yalivyopembuliwa na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana kwa mwaka 2018 kwa kufanya rejea kwa vijana wanaotoka Amerika ya Kati.

Hii pia imekuwa ni fursa ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani huko Panama kuanzia tarehe 22 - 27 Januari 2019 yanaongozwa na kauli mbiu “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38. Katika hija hii, vijana wanasindikizwa kwa mfano na maombezi ya Bikira Maria, aliyeteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa Mama wa Mwanaye Mpendwa, Kristo Yesu.

SEDAC imeangalia changamoto za utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na athari zake, zinazoendelea kuwatumbukiza watu wengi kwenye umaskini na magonjwa. Wajumbe wamefurahishwa sana na Kanisa kumtangaza Askofu Oscar Armulfo Romero kuwa Mtakatifu kutokana na ushuhuda wake kama mchungaji mwema na nabii, aliyejitahidi katika maisha na utume wake kutangaza na kushuhudia upendo na huruma ya Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mtakatifu Oscar Romero awe sasa ni chachu ya umoja na upatanisho wa kitaifa, tayari kuwasaidia waamini kuchuchumilia toba na wongofu wa ndani, ili kuambata utakatifu wa watu wa Mungu.

SEDAC imeguswa sana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wa shuruti wanaoendelea kuteseka kwa kutafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Hawa ni watu ambao utu na heshima yao viko mashakani. Kuhusu Vijana wajumbe wanasema, Hati ya Sinodi ya Maaskofu imejadili kuhusu: umuhimu wa Kanisa na Jamii kujikita katika mchakato wa kukuza na kudumisha haki dhidi ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu. Ukosefu wa fursa za ajira, umaskini; dhuluma na nyanyaso; kutengwa na jamii kutokana na sababu mbali mbali; ubaguzi na ukabila; mambo yanayohitaji : toba, wongofu na mshikamano!

Wajumbe wanawataka vijana kuendelea kujisadaka kwa kujitolea, kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote; kwa kujihusisha kikamilifu katika masuala ya kisiasa, kijamii na kiuchumi, ili kusimama kidete: kulinda: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kudumisha haki jamii, changamoto ambayo vijana wanataka kuona Kanisa inalivalia njuga pasi na mzaha! Mababa wa Sinodi wanasema, sanaa, muziki na michezo ni rasilimali kubwa katika sera, mikakati na shughuli za kichungaji kwa vijana, kwani zinasaidia katika mchakato wa: elimu, malezi na mafungamano ya kijamii. Muziki unaweza kusaidia pia katika maboresho ya liturujia ili Mwenyezi Mungu aweze kuabudiwa na mwanadamu kutakatifuzwa. Vijana wanataka kushirikishwa katika liturujia hai inayofumbatwa katika ukweli, furaha, ibada na uchaji wa Mungu, ili kuweza kukutana na Mwenyezi Mungu pamoja na jumuiya ya waamini.

Kutokana na changamoto hizi, SEDAC inasema, itaendeleza mchakato wa sanaa na ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza vijana wa kizazi kipya kwa kuendelea kuzama katika mawazo ya Injili yanayowaonesha wale wafuasi wa Emau, waliokuwa wanaandamana na Kristo Yesu Mfufuka; Yakafunguliwa macho yao nao wakamtambua; Wakatoka kwa haraka kwenda kutangaza kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa na kufa Msalabani, amefufuka. Lengo ni kuwasaidia vijana kung’amua maisha yao; kutafsiri matukio mbali mbali katika mwanga wa Maandiko Matakatifu na hatimaye, kufanya maamuzi magumu ambayo watapaswa kuyatekeleza haraka, kwa kushirikishana mang’amuzi yao baada ya kukutana na Kristo Mfufuka kama ilivyokuwa kwa wanafunzi wa Emau; kwa kujikita katika tunu msingi za Kiinjili ili kweli vijana hawa waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Kristo, watakaosaidia kuleta mageuzi muhimu huko Amerika ya Kati.

SEDAC imeonesha mshikamano wake na wananchi wa Nicaragua ambao kwa siku za hivi karibuni wamekumbana na mashambulizi ya kutisha, hali inayohatarisha ulinzi na usalama, amani na utulivu kati ya watu. Wajumbe wamewataka wananchi kuondoa hofu na woga kwa kudumisha: uhuru, majadiliano katika ukweli na uwazi kama njia muafaka ya ujenzi wa demokrasia shirikishi.

SEDAC: Amerika ya Kati

 

05 December 2018, 12:45