Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ni mwaliko wa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ni mwaliko wa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia 

Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu

Familia ya Yesu, Maria na Yosefu nayo inaelezwa kwa kufuata taswira hiyo hiyo ya mateso. Tangu kuchukuliwa mimba kwa njia isiyo ya kibinadamu, kujifungulia katika zizi la ng’ombe, kutishiwa kuuawa na Herode, kukimbilia Misri hadi kufa Msalabani. Hizi ni familia zilizokuwa zikimtumainia Mungu. Zilijiaminisha kwa Mungu katika yote zilizokuwa zikipitia.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunaadhimisha Sherehe ya Familia Takatifu, familia ya Yesu, Maria na Yosefu. Huu ni mwaliko na changamoto kwa waamini kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Injili ya familia katika ulimwengu mamboleo ambao unaonekana kwenda kinyume cha Injili ya familia na mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu!

Masomo kwa ufupi: Somo la kwanza (1 Sam 1,20-22. 24-28) ni kutoka kitabu cha Nabii Samweli na linahusu familia ya nabii huyo huyo Samueli. Linaelezea kuzaliwa kwake Samueli. Mama yake Samueli alikuwa mgumba na katika kipindi kirefu cha ndoa yake na mumewe aliyeitwa Elkana hawakuwa na mtoto.  Baada ya muda mrefu sana wa kusali mbele ya Bwana Hana alichukua mimba na akamzaa mtoto mwanamume akamwita Samweli. Somo linaendelea kutueleza kuwa baada ya kuachishwa kwa mtoto, Hana – mamaye – alimchukua na akaenda kumtolea kwa Bwana. Alitambua kuwa mtoto huyo amepewa na Bwana na hivyo alimtoa kwa Bwana ili Bwana amtumie kadiri ya makusudi yake “Naliomba nipewe mtoto huyu; Bwana akanipa dua yangu niliyomwomba; kwa sababu hiyo nami nimempa Bwana mtoto huyu wakati wote akaokuwa hai amepewa kwa Bwana”.

 

Somo hili, pamoja na mafundisho yake mengi juu ya familia, linasisitiza kwa namna ya pekee sana kuwa watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu. Familia inaitwa kuwarudisha watoto hao kwa Mungu ili awatumie kwa makusudi yale aliyowaletea duniani. Kumbe katika makuzi ya watoto ni wazazi walio na jukumu la kwanza la kuwasaidia watoto kukua huku wakimjua Mungu, wakimpenda na wakiwa na shauku ya kumtumikia katika maisha yao.

Somo la pili (1 Yoh 3, 1-2. 21-24) ni waraka kwa kwanza wa mtume Yohane kwa watu wote. Mtume Yohane analeta ujumbe kwetu kuwa pamoja na kuwa na familia zetu za kuzaliwa, sisi sote tunaunda familia moja ya wana wa Mungu. “tazameni ni pendo la namna gani alilotupa Baba kwamba tuitwe wana wa Mungu, na ndivyo tulivyo”.  Na katika familia yetu hii kubwa ni lengo lake Mungu kuwa tufanane naye. Zoezi linaloanza tukingali hapa duniani na litakalokamilika pale atakapodhirishwa kwetu. Zoezi hili la kufanana naye si lingine bali ni la kujitakasa “na kila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa, kama yeye alivyo mtakatifu”. Mtume Yohane anaeleza kuwa sisi tulio wakristo tunazidi kuunganishwa zaidi katika kuwa wana wa Mungu  kwa sababu ya imani yetu na katika kushika wajibu wa imani hiyo.

Injili (Lk. 2, 41-52) injili ya leo inaelezea tukio la Yesu, akiwa kijana wa miaka 12, kupotea kutoka kwa wazazi wake na hatimaye wazazi kumkuta hekaluni katikati ya waalimu wa sheria, akiwasikiliza na kuwauliza maswali.  Somo hili linaionesha familia ya Yesu, Maria na Yosefu kuwa ilikuwa ni familia inayoshika taratibu, mila na desturi.  kwa pamoja wanaenda Yerusalemu kwa ajili ya sikukuu ya pasaka ya wayahudi kama ilivyokuwa desturi. Wakati wa kurudi nyumbani Yesu anabaki Yerusalemu bila wazazi kujua. Wazazi wanahangaika na kuanza kumtafuta. Haya ni mahangaiko ambayo mzazi yoyote angekuwa nayo kwa mtoto wake. Tena somo linatuambia walimtafuta kwa siku tatu, kuonesha jinsi tatizo hilo lilokuwa kubwa. Mwisho wanamkuta hekaluni. Baada ya mahangaiko hayo ya wazazi furaha ya kumpata tena Yesu inakutana na jibu la kuwashitua. Yesu anawaambia “hamkujua imenipasa kuwa katika nyumba ya Baba yangu”.

Kwa jibu hilo Yesu anajitambulisha waziwazi kwa wazazi wake kuwa amekuja kuyatekeleza mapenzi ya Mungu na ni hayo anayoyapa nafasi ya kwanza kwake. Anaialika familia yake iendelee kuyapokea mapenzi ya Mungu kama ilivyofanya kwa kumpokea yeye. Ni hapa tunaona kuwa somo hili linazialika familia kuwa tayari kuyapokea mapenzi ya Mungu katika maisha. Kuyapokea mapenzi ya Mungu si tu katika nyakati nzuri bali na hasa zaidi katika yale yasiyoeleweka wala kuelezeka vema na kuyakabidhi yote kwa Mungu.

TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News leo tunaadhimisha sherehe ya Familia Takatifu. Maandiko Matakatifu ambayo tumeyaona kwa kifupi yametuingiza katika tafakari ya familia katika mwanga wa imani ya Kikristo. Ni siku ya kujiuliza tena na tena, kwetu Familia Takatifu ni ipi? Tunawezaje kuuishi utakatifu katika familia? Tunawezaje kuufikia utakatifu ndani ya familia? Tunawezaje kuuonesha au kuushuhudia utakatifu wa familia katika mazingira yetu ya leo?

Maandiko Matakatifu, tangu Agano la Kale hadi Agano Jipya limejaa masimulizi kuhusu familia na wakati mwingine yanataja baadhi ya familia kwa majina na kuelezea maisha yao. Biblia haizitaji familia hizo moja kwa moja kuwa ni takatifu. Na tena tunapoangalia familia zinazotajwa katika Biblia, karibu zote ni familia zilizoteseka. Tukianza na familia ya Adamu na Eva licha ya kuingia katika dhambi ya asili ndiyo inayotakwa kwa mara ya kwanza kuonja uchungu wa mauaji ya ndugu. Kaini alimuua ndugu yake Abeli. Familia ya Abrahamu na Sara iliteseka kwa kukosa mtoto hadi uzee. Isaka alizaliwa Abrahamu akiwa na miaka 100. Ndivyo ilivyokuwa pia familia ya Elkana na Hana na familia ya Zakaria na Elizabeti wazazi wa Yohane Mbatizaji kwa uchache.

Familia ya Yesu, Maria na Yosefu nayo inaelezwa kwa kufuata taswira hiyo hiyo ya mateso. Tangu kuchukuliwa mimba kwa njia isiyo ya kibinadamu, kujifungulia katika zizi la ng’ombe,  kutishiwa kuuawa na Herode, kukimbilia Misri hadi kufa Msalabani. Pamoja na mahangaiko na mateso ya familia hizo kitu kimoja kinaonekana waziwazi: ni familia zilizokuwa zikimtumainia Mungu. Zilijiaminisha kwa Mungu katika yote waliyokuwa wakiyapitia. Tumeona katika Injili ya leo Bikira Maria anayaweka moyoni mambo aliyoambiwa na Yesu mwanae. Huenda hapo alipoambiwa hakuyaelewa, ila kwa kuyaweka moyoni alijiamisha kwa Mungu kwani mapenzi ya Mungu kwa mtu hujifunua polepole. Kwa sababu ya tumaini hilo familia hizi hazikuchoka kusali na kumwomba, hazikuchoka kuvumilia na hazikuchoka kuamini. Na mwisho si mateso yaliyoshinda bali ni utukufu wa Mungu ulioonekana katika familia zote hizo.

Hata sisi leo hii familia zetu haziko mbali na uhalisia wa familia za watangulizi wetu wa imani zinazoelezwa katika Maandiko Matakatifu. Kumbe utakatifu wa familia tunaoufakari leo sio ule wa kuishi maisha ya raha mustarehe katika familia. Tukiyapata hayo tumshukuru Mungu. Lakini katika nafasi ya kwanza utakatifu wa familia ni kujiaminisha kwa Mungu katika yote ambayo familia inayapitia. Kumtumainia Mungu, kumwamini Mungu na kumweka yeye mbele daima. Kuuoa uwezo wa Mungu kuwa ni mkubwa kuliko changamoto zozote zile ambazo familia inazipitia.

Mtume Yohane katika masomo ya sherehe ya leo ametuambia kuwa pamoja na kuwa na familia zetu za nyumbani tunaunda pia familia kubwa zaidi ya wana wa Mungu. Na hapa tunaweza kuzungumzia familia ya kitaifa, ya kimataifa au hata ile familia ya kanisa la kiulimwengu. Familia hizi zinategemeana. Kinachoendelea katika familia zetu kiwe kizuri au kibaya kinaathiri pia familia hii kubwa na vivyo hivyo kinachoendelea katika familia hii kubwa kiwe kizuri au kibaya kinaathiri pia familia zetu za nyumbani.

Pamoja na hayo, Kwa kutambua kuwa familia ya nyumbani kuwa ndio kiini cha maisha ya jamii (KKK 2207) leo, katika sherehe ya Familia Takatifu, tunaalikwa kuutwaa upya wajibu wa kuilinda familia ya nyumbani, kulinda hadhi yake, kulinda tunu zake dhidi ya uharibifu au upotofu wowote ule. Huu ni wajibu wetu wanafamilia na ni wajibu wa vyombo vyote vya kitaifa na vya kimataifa. Ni katika msingi huu huu Kanisa linaendelea kupinga utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika vitendo vya utoaji mimba, ushoga, ndoa za watu wa jinsia moja, mauaji ya visasi nk. kwani ni mojawapo ya vitendo vinavyoharibu misingi na tunu bora za familia. Na kila jumuiya ya kitaifa au kitaifa inayoona haya kukemea mwendendo wowote unaoharibu familia inapaswa kujikosoa. Familia ni kiini. Ustawi wa familia haupaswi kuwekwa rehani kwa ajili ya malengo yoyote yale yawe ya kisiasa au ya kiuchumi. Kucheza na misingi ya familia ni kuiua familia na kuiua familia ni kuiua jamii nzima.

Sherehe Familia Takatifu
29 December 2018, 07:46