Matumaini ya Kikristo yanafumbatwa katika toba, wongofu wa ndani na fadhila! Matumaini ya Kikristo yanafumbatwa katika toba, wongofu wa ndani na fadhila! 

MAJILIO: Matumaini yanafumbatwa katika: toba, wongofu na fadhila!

Wongofu ni mwaliko na zoezi la kila siku tunaalikwa kumrudia Mungu kutoka katika upotevu wetu; mdogomdogo na hata ule mkubwa. Kwa njia ya fadhila, hasa hizo alizotukumbusha Mt. Paulo; ushuhuda wa furaha ya injili, majitoleo na upendo wa kidugu tunapiga hatua kumpokea Masiya. Na kwa njia hii tutakuwa kweli tunaitengeneza njia yake na kunyoosha mapito yake.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunaadhimisha dominika ya pili ya Kipindi cha Majilio, dominika ambayo tunaalikwa kutafakari nafasi ya Toba, Wongofu na Fadhila njema katika kukuza matumaini ya kumngojea Masiya. Ujumbe wa Yohane Mbatizaji “itengenezeni njia ya Bwana, yanyoosheni mapito yake” unasikika tena kwetu leo kama mwaliko wa kudumu wa kuyaishi majilio.

Masomo kwa ufupi: Somo la kwanza (Bar. 5, 1-9) Nabii Baruku analeta ujumbe wa matumaini kwa mji wa Yerusalemu, mji ambao ulikuwa umeharibiwa na kuachwa magofu kwa sababu wakazi wake walikuwa wametwaliwa mateka. Ni mji ambao kwa maneno ya nabii ulikuwa katika matanga na huzuni. Lakini kwa nafasi ambayo ulikuwa nao mji huu kwa Waisraeli, haya matanga na huzuni havikuwa kwa mji huu tu bali kwa waisraeli wote. Baruku anatoa unabii kuwa Yerusalemu utajengwa upya, vilima vyake vitashushwa, mabonde yatajazwa na nchi yote itakuwa sawa. Wanawe walikokuwa wametawanywa watarudishwa na tena watarudishwa kwa heshima na maadui walewale waliowachukua kwa kebehi.

Kitabu hiki cha Nabii Baruku, kwa uchambuzi wa wataalamu wa Maandiko Matakatifu, ni kitabu ambacho kiliandikwa miaka mingi sana baada ya tukio lenyewe la kuharibiwa mji wa Yerusalemu na hatimaye kujengwa upya. Na kiliandikwa katika mazingira tofauti na hayo; ni nje ya Yerusalemu kwa wayahudi ambao walikuwa wakiishi nje (diaspora) ili waendeleze mapokeo ya kiyahudi mintarafu ufunuo wa Mungu katika historia yao.

Kumbe simulizi hili lilikuwa ni kuwasaidia kutafsiri maisha yao wa wakati huo katika mwanga wa yale ambayo Mungu alikuwa amewatendea katika kipindi cha nyuma. Na kwa kuwa sasa katika kipindi hicho walikuwa katika changamoto ambapo ni kama walikuwa wamekata tamaa, nabii anawakumbusha kuwa hata mwanzo wazee wao walikuwa katika magumu na walikuwa wamekata tamaa ila Mungu aliwatendea makuu. Hivyo hata sasa wamtegemee Mungu. Kwa lengo hilo hilo, Kanisa linatuletea ujumbe huu katika kipindi cha majilio kuimarisha matumaini yetu nasi pia, matumaini ya ujio wa masiya na ya utimilifu wa ahadi zake kwetu.

Somo la pili (Fil. 1:4-6, 8-11) Mtume Paulo anawaandikia waraka Wafilipi kama ilivyokuwa kawaida yake kuendeleza mawasiliano na jumuiya za Kikristo au makanisa mahalia aliyoyaanzisha kwa mahubiri na utume alioufanya kati yao. Waraka huu kwa wafilipi anauandika akiwa kifungoni na katika sehemu hii ya kwanza ambayo ndio somo letu anawaandikia kuwapa moyo, anawahakikishia kuwa anawaombea daima, akiwashukuru kwa misaada mbalimbali waliyompa na akiwaasa waendelee kukua katika fadhila njema.  Na hasa fadhila zinazowajenga kama jumuiya ya kikristo na fadhila zinazomjenga kila mmoja wao; ndiyo kuwa watu wa furaha, wa kujitolea kwa ajili ya kuwezesha mchakato wa uenezaji wa Injili na wanaozidi kukua katika upendo wa Kikristo na kudumu hivyo hadi siku ya Kristo yaani siku atakaporudi tena.

Injili (Lk. 3:1-6) injili ya leo inazungumzia mwito wa kinabii wa Yohane Mbatizaji na utume wake wa kuwaandaa watu kwa ujio wa masiya. Mwinjili anaweka tukio hili katika muda maalumu wa kihistoria na anataja majina ya watawala wa kisiasa wa wakati huo na wale wa kidini. Yohane Mbatizaji anapata mwito wake wa kinabii kwa njia ya Neno linalomjia akiwa jangwani. Naye anaanza kuhubiri ubatizo wa toba, akitekeleza yaliyoandikwa tayari na nabii Isaya 40:3: sauti ya mtu aliaye nyikani, itengenezi njia ya Bwana, yanyoosheni mapito yake…” Nabii Isaya kwa unabii wake huo alikuwa anatangaza kurudi kwa wana wa israeli katika nchi ya ahadi akifananisha kurudi huko kama walivyorudi waisraeli kutoka utumwani Misri.

Yohane Mbatizaji naye anawaandaa Waisraeli wa wakati wake kwa ujio wa Masiya ambaye anakuja kuwatoa upya watu kutoka utumwa wa dhambi kuwapitisha katika uhuru wa wana wa Mungu. Anataja pia jangwa, mahali ambapo waisraeli waliundwa kuwa taifa la Mungu, walijifunza kumpenda Mungu na wakaweka agano naye. Kumbe hata sasa Masiya anakuja kuwaunda upya ili wamjue vema Mungu, wampende na waweke upya agano naye. Nayo njia ya Bwana anayowaalika kuitengeneza ni njia inayomwongoza mtu kumrudia Mungu. Agano la Kale limejaa mwaliko wa mwanadamu kushika njia ya Bwana; kuenenda kadiri ya mapenzi ya Mungu. Yohane Mbatizaji anapoalika watu kutengeneza njia ya Bwana anaalika kuweka mpango mkakati katika maisha utakaomwezesha mtu kuenenda katika mapenzi yake Bwana

TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, dominika hii ya pili ya majilio ni dominika inayoamsha ndani yetu matumaini ya kumngojea Masiya. Inaweka hai ujio wa masiya kati yetu na kutuonesha kuwa yeye anakuja kuinua hali yetu, ni Mungu katika ukuu wake anayekuja kukutana na mwanadamu katika unyonge wake ili kumuokoa. Hivi kipindi hiki cha majilio kinakuwa kwetu sauti ya kinabii, sauti ambayo katika Agano la Kale iliweka hai kwa waisraeli tumaini la ujio wa masiya na sauti ambayo kwa njia ya Yohane Mbatizaji ilimtambulisha pale alipokuja.

Tukiwa katika hali hiyo, Masomo ya leo yanatualika kudhihirisha matumaini hayo kwa njia ya Toba, Wongofu na Fadhila. Kwa njia ya toba tunakiri udhaifu na makosa yetu; tunaona ubaya na madhara yake kwetu na kwa wenzetu na hii inatuandaa kupokea msamaha na maondoleo. Kwa njia ya wongofu, ambao ni mwaliko na zoezi la kila siku tunaalikwa kumrudia Mungu kutoka katika upotevu wetu; mdogomdogo na hata ule mkubwa. Kwa njia ya fadhila, hasa hizo alizotukumbusha Mt. Paulo; ushuhuda wa furaha ya Injili, majitoleo na upendo wa kidugu tunapiga hatua kumpokea Masiya. Na kwa njia hii, tutakuwa kweli tunaitengeneza njia yake na kunyoosha mapito yake.

Liturujia Majilio J2
07 December 2018, 15:03