Tafuta

Vatican News
Ni wakati wa kutafakari Fumbo kuu la Umwilisho wa Neno wa Mungu! Ni wakati wa kutafakari Fumbo kuu la Umwilisho wa Neno wa Mungu! 

Kama B. Maria, Kanisa linasubiri kwa imani ujio wa Kristo Yesu!

Ni kwa utii kwa Mungu Baba na kwa mapenzi yake matakatifu, Yesu Kristo anatwaa mwili na kuzaliwa kwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu kwake yeye Bikira Maria. Ni hapa tunaona kuwa ni katika mlango wa kutokutii kwa Adamu na Eva dhambi iliingia ulimwenguni na sasa katika mlango wa utii anaingia ulimwenguni Yule anayekuja kuishinda dhambi ulimwenguni.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunaadhimisha dominika ya nne na ya mwisho ya Majilio. Tunaikaribia sana Siku kuu ya kuzaliwa mwokozi wetu na Maandiko Matakatifu siku ya leo yanatusogeza katika kulitafakari fumbo hilo kuu la wokovu wetu.

Masomo kwa ufupi: Somo la kwanza (Mika 5, 1-4a) Ni kutoka kitabu cha Nabii Mika. Huyu ni nabii aliyefanya kazi yake ya unabii katika kipindi sambamba na Nabii Isaya pamoja na Nabii Yeremia. Tunaliona hilo kwa sababu kiasi fulani ujumbe wa unabii wao unafanana japo kila mmoja anakuwa anaueleza kwa namna yake. Katika somo la leo, Nabii Mika anaitabiria Israeli iliyo katika kipindi cha mahangaiko na mateso kuwa Mungu ataiinulia mtawala atakayewaondoa katika mahangaiko na mateso hayo. Kuhusu mtawala huyo nabii anaagua kuwa atazaliwa Bethlehemu, mji uliokuwa mdogo, mji ambao  Daudi aliweka kwanza makao yake ya kifalme na ukaitwa mji wa Daudi na ni mji sasa ambao utakuwa mkubwa zaidi kwa sababu kwake atazaliwa kiongozi mkuu zaidi.

Pili mtawala huyo hamwiti tena Mfalme kama walivyokuwa wafalme wengine ambao kwa kutokutii agano la Mungu na kwa kutokusikiliza sauti yake waliliingiza taifa zima katika uchungu. Anamwita mtawala kwa mantiki kuwa ni Yeye Mungu atakayempa mamlaka huyo mtawala, na mtawala atawatawala waisraeli kwa kufuata sauti ya Mungu na maagizo ya Mungu na wala si utashi wake binafsi. Atatawala kwa kutekeleza mapenzi ya Mungu na si mapenzi yake. Unabii huu pamoja na kuzungumzia mazingira halisi ya waisraeli wa wakati huo, ni unabii wa kimasiha na ndani yake tunamwona Kristo katika nafsi ya mtawala huyo aliyetabiriwa. Agano Jipya linanukuu unabii huu na linaeleza kuwa Kristo anazaliwa Bethlehemu na ni yeye  yeye anayekuja kutimiza ahadi zile Mungu alizomwapia Daudi, na ni yeye anayekuja kukalia kiti cha Daudi. Tena zaidi ya hapo, Kristo ndiye anayeonesha hali ya juu ya kufuata mapenzi ya Baba na kwa kufanya hivyo analeta amani kwa watu wote wa taifa la Mungu

Somo la pili (Ebr. 10,5-10) ni waraka kwa Waebrania. Linaeleza kuwa Kristo amekuja ulimwenguni kwa sababu amemtii Baba. na kwa sababu ya utii huo amemtolea Baba sadaka inayopendeza zaidi kuliko zile sadaka za kuteketezwa zilizokuwa zikitolewa katika Agano la Kale. Ni somo linalohimiza utii kwa Mungu Baba na utayari wa kutimiza mapenzi yake kama mwendelezo wa sadaka impendezayo Mungu kuliko sadaka nyingine ile katika maisha ya mwamini.

Injili (Lk. 1, 39-45) Injili ya leo inamwelezea Mama Bikira Maria, baada ya kupashwa habari ya kuzaliwa Bwana, anakwenda kumtembelea Elizabeti, mama wa Yohane Mbatizaji. Katika maamkio ya Bikira Maria kitoto kinaruka ndani ya tumbo la Elizabeti, naye anajazwa Roho Mtakatifu na anatoa utabiri wake. Na katika utabiri wake, Elizabeti anaeleza mambo makuu manne: Mosi, anamtaja Bikira Maria kuwa ni mbarikiwa “umebarikiwa wewe kuliko wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa” na haya ni maneno ambayo Kanisa linayatumia katika sala ya Salamu Maria.

Pili, anamwita Maria “mama wa Bwana wangu”. Anakiri kuwa yule ambaye Maria amemchukua mimba ni Bwana, yaani ni Mungu.  “Yule ambaye Maria amemchukua mimba kama mtu na ambaye amekuwa mwana wake kadiri ya mwili ndiye Mwana wa milele wa Baba, nafsi ya pili ya Utatu Mtakatifu sana” (Rej. KKK 498. ) Tatu, anaeleza maana ya kuruka kwa mtoto wake, Yohane Mbatizaji, kuwa ni furaha. Yohane Mbatizaji anapata furaha ya kujazwa na Roho Mtakatifu akingali tumboni mwa mama yake. Na hili linatafsiri tendo zima la Bikira Maria kumtembelea Elizabeti kuwa ni tendo la Mungu kuwaijia watu wake na kuwapa furaha (Rej KKK 717). Nne, anakiri imani kuu ya Bikira Maria na anamwita mwenye heri na ambaye atakayeamini kwa kufuata mfano wake naye atakuwa na heri.

TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Maandiko Matakatifu katika dominika hii ya nne ya majilio yanajikita katika dhamira ya utii. Yanatuonesha kuwa Umwilisho, yaani fumbo la nafsi ya pili ya Mungu kutwaa mwili na kushuka ulimwenguni limefanyika kwa sababu ya utii. Ni kwa utii kwa Mungu Baba na kwa mapenzi yake matakatifu, Yesu Kristo anatwaa mwili na kuzaliwa kwetu. Ni hapa tunaona kuwa ni katika mlango wa kutokutii kwa Adamu na Eva dhambi iliingia ulimwenguni na sasa katika mlango wa utii anaingia ulimwenguni Yule anayekuja kuishinda dhambi ulimwenguni.

Naye Yesu Kristo ambaye hakushuka ulimwenguni kuyafanya mapenzi yake bali ya Baba anaishi utii huu hadi mwisho pale msalabani na ni katika utii huo ulimwengu unapata utakaso na kukombolewa kwa sadaka yake (Rej. KKK 2824). Mama Bikira Maria anawekwa kwetu kama kielelezo cha utii wa imani. Kwa imani anapokea ujumbe wa Malaika na anakubali kuwa Mama wa Mungu. Anakwenda kumtazama Elizabeti, si ili kuthibitisha aliyomwambia Malaika bali anakwenda kwa furaha kupeleka Habari Njema, ndiye Kristo Bwana wetu.

Hii ni dominika basi inayotualika kutafakari juu ya nafasi ya utii katika maisha yetu wakristo hasa katika nyakati zetu hizi ambazo utii unaonekana kama udhaifu na kinyume chake kuwa ushujaa. Nyakati ambazo uhuru unapewa nafasi dhidi ya utii kiasi cha kusahau kuwa Mungu aliyemuumba mwanadamu na kumpa uhuru ndiye Mungu yule yule aliyempa pia mwanadamu agizo la kutii: kumtii Yeye, kuitii sauti yake na kuyatii maagizo na amri zake. Utii ni mojawapo ya sadaka kubwa sana ambayo mwanadamu anapaswa kuitoa iwe ni katika ustawi wa jamii, iwe ni katika ustawi wa imani. Na kwa namna ya pekee leo tunaona kuwa bila utii haiwezekani kuyatimiza mapenzi ya Mungu na haiwezekani kuyaelewa mapenzi ya Mungu katika maisha. Kristo, Masiha anayekuja kwetu atusaidie kuamsha ndani yetu fadhila hii ya utii.

Liturujia J4 Majilio
21 December 2018, 14:32