Kipindi cha Majilio: Itengenezeni Njia ya Bwana, Yanyoosheni mapito yake! Kipindi cha Majilio: Itengenezeni Njia ya Bwana, Yanyoosheni mapito yake! 

Jumapili ya Pili ya Majilio: Mnatumwa kutangaza na kushuhudia imani!

Kipindi cha Majilio kinatukumbusha matendo makuu aliyotutendea Mwenyezi Mungu na kutumaini ujio mtakatifu wa hukumu ya wazima na wafu. Ufahamu sahihi wa pendo hili la kimungu unakuwa wokovu kwetu sisi na yule anayefahamu na kuwa na kumbukumbu nzuri na hai ataishi kwa matumaini. Na matumaini hayo yanatuwajibisha ili sisi tumshukuru Mungu kwa upendo wake.

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma, Tanzania.

Ndugu mpendwa, karibu tena tusali pamoja na kutafakari neno la Mugu siku hii ya Bwana katika dominika hii ya pili ya majilio. Leo tunapata somo la kwanza toka kitabu cha Baruku. Kitabu hiki kimeandikwa ili kuwaonya watu juu ya dhambi zao na kuwahimiza katika matumaini. Kwa namna ya pekee somo la leo latualika kuvua nguo za matanga na kuuvaa uzuri utokao kwa Mungu. Hapa Israeli anatoka utumwani, hivyo anahimizwa au kuitwa kuwa tayari kuanza upya.

Somo la Injili linatualika kutangaza kwa matendo. Hapa tunapata mfano kamili wa maisha ya ushuhuda. Yohane aliishi alichohubiri – angalia mavazi, maisha yake, mazingira ya kazi yake. Atualika kujivika kilemba chake aliye juu. Hapa Yohani atualika kutubu na kuongoka. Anamwonesha Yesu moja kwa moja kwetu. Tangu kuzaliwa kwake Yohani, baba yake anamwita nabii – Lk. 1:76. Kwa nini aitwe nabii? Katika msingi wa uelewa wa Israeli, alikemea unyanyasaji na kuongea waziwazi dhidi ya dhuluma yo yote ile. Hii ilikuwa sifa kuu ya unabii. Pia katika Injili ya leo – tunasikia aliye na kanzu mbili na aitoe kwa mwingine, kwa watoza ushuru wasinyanyase wengine n.k. Kwa hiyo twaweza kuona na kuelewa wajibu wa Nabii hata kwetu leo – mapambano dhidi ya aina yo yote ile ya dhuluma. Yohani ananyoosha kidole dhidi ya uovu wowote ule – Mt. 14:4.

Kama Nabii, Yohane Mbatizaji anafanya zaidi. Anawaelimisha watu habari ya wokovu na maondoleo ya dhambi – Lk. 1:77.  Kwa kawaida wajibu wa Nabii katika Israeli ulikuwa ni kuonesha au kuongea juu ya wokovu ujao. Yohani Mbatizaji hatangazi wokovu ujao. Yeye huonesha wokovu uliopo kati yetu. Ananyoosha kidole na kumwonesha Mwanakondoo wa Mungu – Yoh. 1:29 – Yule aliyesubiriwa tangu karne – huyu hapa. Manabii wengine waliongea juu ya wokovu ujao ila Yohane anasema na kuonesha wokovu huo kati ya watu. Hii ndiyo tofauti ya manabii wengine na Yohane Mbatizaji. Yohane Mbatizaji anaanzisha aina mpya ya unabii wa kikristo, ambayo ni tofauti na manabii wengine. Yeye hatangazi wokovu ule ujao, bali afunua na kuweka wazi uwepo wa Kristo ulimwenguni. Hapa twahitaji imani kubwa na ushuhuda wa pekee. Somo la pili linapata maana kubwa sana hapa. Latualika kuishi imani thabiti.

Sisi leo tunatakiwa kufanya yote ili hiyo sauti ya Yohane iendelee kusikika na kuonekana katika ulimwengu wetu. Lakini zaidi si kutangaza tu uwepo wa Kristo lakini pia kuishi huo wito ambao Kristo kwa upendo ametushirikisha katika watakatifu wake kama Yohane alivyoishi na kushuhudia. Tutafakarishwe na mfano huu. Mwanamuziki maarufu Mwiitaliano kwa jina Paganini, alipewa zawadi ya saa ya dhahabu na mfalme wa Ufaransa. Aliipenda sana zawaidi hiyo na kila mara akiongea na rafiki zake iliitaja hiyo zawadi aliyopewa na mfalme.  Hata zikiwa zimepita siku nyingi tangu alipopewa hiyo zawadi, rafiki yake alimwuliza kama anajua vizuri thamani ya hiyo saa. Paganini alishangaa sana kwa swali hilo. Rafiki yake huyo akamwambia aifunue ndani aone kilichopo. Alipofunua akakuta ndani yake limeandikwa jina lake kwa herufi za dhahabu. Hapa ndipo alipoipenda zaidi ile zawadi. Akagundua kuwa mfalme hakuinunua tu dukani bali pia aliogezea thamani kwa kuandika kwa mkono wake jina lake na kuweka ndani ya hiyo saa.

Sisi leo tunajiuliza ni kwa kiasi gani tunatambua thamani ya upendo wa Mungu kwetu?. Ni kwa jinsi gani tunathamini maisha yetu, zawadi ya imani yetu ya kikristo. Yohane anatufundisha nini leo. Majilio hutupa nafasi ya kukumbuka matendo makuu ya Mungu na kutumainia upendo wake mkuu ambao kwetu sisi ni wokovu wa milele. Tunatambua kuwa kipindi cha Majilio ni kipindi cha kukumbuka makuu aliyotutendea Mwenyezi Mungu na kutumaini ujio mtakatifu wa hukumu ya wazima na wafu. Ufahamu sahihi wa pendo hili la kimungu unakuwa wokovu kwetu sisi na yule anayefahamu na kuwa na kumbukumbu nzuri na hai ataishi kwa matumaini. Na matumaini hayo yanatuwajibisha ili sisi tumshukuru Mungu kwa upendo wake kwetu.

Tunakumbuka nini? Tunamkumbuka Yesu Kristo aliyejifanya mtu - tunatafakari uwepo wake na maisha yake hapa duniani kama Mungu na mwanadamu na akaupa maana na heshima uwepo wetu sisi – hadhi ya kimungu, akatuonesha maana ya maisha ya Kimungu - eti Mungu akawa mwanadamu. Tumshukuru Mungu. Tunatumaini nini? Tunatumaini ujio mtakatifu aliotuahidia, jumuiya takatifu na utu uliofungamanishwa na upendo wa Mungu. Angalia Pope Benedict XVI (Joseph Card Ratzinger) “Seek that what is above” 1986 … Memory Awakanes Hope.

Kumbukumbu zinaamsha matumaini. Tunakumbuka kuwa Mungu amekuja kwetu, akakaa nasi na tunahuisha matumaini yetu kwamba Kristo atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu wazima na wafu. Katika kipindi cha majilio tunakumbuka matendo makuu ya Mungu na tunatumainia upendo mkuu wa Mungu. Hatuna budi kutambua kuwa sisi ndiyo sauti ya kinabii kwa wakati wetu huu. Sisi tunatakiwa tuchukue nafasi ya Yohani Mbatizaji katika ulimwengu wetu huu. Je, sisi tunaotambua upendo huu wa Mungu tunauambia ulimwengu wa leo kitu gani cha pekee? Tunashuhudia nini? Ulimwengu wetu wa leo unataka kusikia sauti gani ya kimungu/kinabii? Je, kama Yohane Mbatizaji twaweza kuendelea kumwonesha Mwanakondoo wa Mungu kwa watu katika mazingira ya wakati wetu huu? Tumwombe Mungu Roho Mtakatifu aendelee kutufunulia upendo huo na sisi tujiweke tayari kuishi wito huo aliotujalia Mungu Baba ili tuweze kushuhudia kwa matendo yetu. Tumsifu Yesu Kristo.

04 December 2018, 14:40