Padre Joseph Peter Mosha: Asili ya binadamu na utu wake ndio msingi wa umoja na udugu! Padre Joseph Peter Mosha: Asili ya binadamu na utu wake ndio msingi wa umoja na udugu! 

Padre Joseph Peter Mosha atunukiwa shahada ya uzamivu, Roma!

Udugu na umoja ni tunu ambazo kwa sasa zinakabiliwa na changamoto kubwa katika jamii ya watanzania kiasi hata cha kutishia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kumbe, Kanisa nchini Tanzania katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya uinjilishaji, linajikuta kuwa na dhamana ya kuendelea kupyaisha umoja na udugu mintarafu uinjilishaji wa kina.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Udugu wa Kikristo nchini Tanzania kama nyenzo msingi ya kustawisha utu wa mtu ndiyo tema iliyodadavuliwa kwa kina na mapana na Padre Joseph Peter Mosha kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam, kiasi cha kuwaridhisha majaalimu wake na hivyo tarehe 17 Desemba 2018 kutunukiwa Shahada ya Uzamivu kutoka Taasisi ya Maadili ya Alfonsianum iliyoko Jijini Roma. Padre Mosha katika kazi yake, anasema, hekima, umoja, uhuru na amani ndizo nguzo kuu zinazowaongoza na kuwafungamanisha watanzania kiasi cha kujisikia kuwa ni ndugu wamoja.

Udugu na umoja ni tunu ambazo kwa sasa zinakabiliwa na changamoto kubwa katika jamii ya watanzania kiasi hata cha kutishia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kumbe, Kanisa nchini Tanzania katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya uinjilishaji, linajikuta kuwa na dhamana ya kuendelea kupyaisha umoja na udugu mintarafu uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa kama Mama na Mwalimu linapaswa kuendelea kuwekeza katika majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa kutoa kiumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ikumbukwe kwamba, asili ya binadamu na utu wake ndio msingi wa umoja na udugu.

Padre Mosha anaendelea kudadavua kwa kusema, umoja na udugu ni tema ambayo imepembuliwa vyema na Mababa wa Kanisa pamoja na nyaraka mbali mbali zilizotolewa na viongozi wa Kanisa na kwa namna ya pekee, Hati ya Mtakatifu Yohane Paulo II, “Ecclesia in Africa”, yaani “Kanisa Barani Afrika” pamoja na Hati ya Kitume ya Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, “Africae munus” yaani “Dhamana ya Afrika! Hapa mkazo ni uinjilishaji unaokwenda sanjari na utamadunisho ili kupyaisha tunu msingi za maisha ya kiafrika mintarafu mwanga wa Injili.

Udugu na ujamaa unaofumbatwa katika tunu msingi za maisha ya kifamilia, bado ni muhimu miongoni mwa jamii ya watanzania, ili kupambana na ubinafsi na uchoyo ambao umepelekea uvunjifu wa maadili na haki msingi za binadamu. Mauaji ya kikatili, rushwa na ufisadi ni dalili za kumong’onyoka kwa tunu msingi za maisha ya kijamii nchini Tanzania, jambo linaloweza kuibua tena matabaka na hivyo kudhohofisha mshikamano na mafungamano ya kidugu nchini Tanzania. Kanisa liendelee kuwekeza katika majiundo makini ya dhamiri nyofu, kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo inayofumbatwa katika: haki, amani na upatanisho.

Ikumbukwe kwamba, uongozi ni huduma inayopania kukuza na kudumisha utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na wala si kichaka cha watu kujilimbikizia mali. Huruma na upendo wa Mungu, viwe ni chachu ya ujenzi wa umoja, udugu na mshikamano kati ya watanzania, kanuni maadili na utu wema vikipewa msukumo wa pekee! Haya ni mambo yanayosimikwa katika mshikamano wa upendo unaoongozwa na kanuni auni pamoja na kujitegemea kwa kusimamia mambo msingi katika maisha, bila ya kuyumbishwa na ukoloni wa kiitikadi!

Tukio hili adhimu limehudhuriwa na umati mkubwa wa familia ya Mungu kutoka Tanzania na kwa namna ya pekee, uwepo wa Padre Charles Kitima, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania pamoja na Mama Eliambuya Mosha, Mama Mzazi wa Padre Joseph Peter Mosha. Mama Inno anasema, amependa kulipamba tukio hili kwa machozi ya furaha na shukrani kwa Mwenyezi Mungu; mwingi wa huruma na mapendo kwa waja wake. Amejifunga kibwebwe kutoka Tanzania ili kuja kushuhudia mwanaye akivikwa taji ya Shahada ya Uzamivu kutoka Taasisi ya Maadili ya Allfonsianum.

Mama Inno kama anavyojulikana na wengi Jijini Dar es Salaam katika mahojiano maalum na Vatican News anasema, haikuwa rahisi sana wazo la Joseph Peter Mosha kuwania Upadre! Baba mzazi hakuridhia sana, lakini kutokana na machozi yake na hatimaye, wazazi wote wawili wakaridhia, Mosha akaenda Seminarini na hatimaye kunako tarehe 7 Julai 2006 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Lakini, Baba yake mzazi hakufanikiwa kuiona siku hii maalum, kijana wake akijisadaka kwa ajili ya kumtumikia Mungu na jirani zake kwa njia ya Daraja Takatifu ya Upadre, kwani alifariki dunia tarehe 14 Novemba 1997 na tangu wakati huo, akabeba dhamana ya kumhudumia mtoto wake kwa upendo mkuu!

Mama Eliambuya anasema, yeye ni Mluteri kwa asili, lakini daima, aliona uwepo wa Padre Mosha katika maisha ya familia yao kama chachu ya majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika sala, maisha ya kiroho na huduma kwa watu wa Mungu; ndiyo maana tangu mwanzo, alifurahia kuona mwanaye akienda seminarini na alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre, akampigia Mungu magoti ya shukrani. Leo hii anapomwona anavikwa taji ya udaktari, kwa hakika ni siku ambayo amempigia Mungu kelele ya furaha na shukrani kutoka katika sakafu ya moyo wake; na kwamba, anaendelea kumwombea heri, baraka na udumifu katika huduma kwa shamba ya Bwana, ili kwa njia ya sadaka ya maisha na utume wake wa Kipadre, aweze kuwainua watu wengi zaidi, ili wampende Mwenyezi Mungu na jirani zao.

Mama Eliambuya anamshukuru Mungu, viongozi wa Kanisa na watanzania wenzake, waliomsaidia na kumsindikiza hadi kufikia hatua hii. Anawashukuru na kuwapongeza wote waliomsaidia: kufikiri, kupanga na kuandika, hata kazi yake ikakubalika. Anapenda kuchukua fursa hii kuwahimiza watanzania wengine wanaoendelea na masomo yao kujituma zaidi na kamwe wasimwachie nafasi shetani kuwavuruga na kuwakatisha tamaa na hatimaye, wakajikuta wakirejea nchini Tanzania wakiwa “wameficha makoti” nyuma. Wajitahidi, kuiga mifano bora ya ndugu zao waliowatangulia, ili hata wao siku moja, waweze kuvishwa taji ya ushindi katika maisha na masomo!

Kwa upande wake, Padre Charles Kitima, amemshukuru Mungu kwa kumwezesha Padre Joseph Peter Mosha kukamilisha na kutetea kazi yake kwa ufundi mkubwa na hatimaye, kutunukiwa shahada ya uzamivu katika maadili. Anasema, udugu wa Kikristo ni njia muafaka ya kumwendeleza mwandamu: kiroho na kimwili. Kutokana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza, leo hii Tanzania inahitaji wanataalimungu maadili, watakaoweza kutoa tafsiri sahihi matukio na changamoto mbali mbali zinazoendelea katika masuala ya maadili na utu wema. Sayansi ya maadili na hofu ya Mungu ni mambo msingi kwa wakati huu. Kumbe, udugu wa kiinjili unaweza kuchochea: utu, heshima, umoja na mshikamano wa dhati kati ya watanzania.

Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni, Padre Alister Makubi kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam, alitetea kazi yake na kutunukiwa Shahada ya Uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterano, tukio ambalo lilishuhudiwa pia na Mama Beatrice Makubi, Mama mzazi wa Padre Makubi, aliyemfundisha hisabati na kimombo tangu mwaka 1965 hadi mwaka 2007 alipong’atuka na kuanza kula “bata” wa pensheni ya uzeeni. Mama Makubi alifundisha shule ya Msingi Mlimani, Jijini Dar es Salaam! Mama Makubi aliwapongeza watanzania kwa kuonesha: furaha, umoja, upendo na mshikamano pamoja na kusaidiana wanapokuwa ughaibuni. Kama Mama alipenda kuwatia shime, majandokasisi wanaoendelea na masomo yao kwenye Seminari Ndogo ya Visiga Jimbo kuu la Dar es Salaam, ambayo bado anaikumbuka sana, kwani alimposindikiza kwa mara ya kwanza mwanae Padre Makubi, Visiga, kulikuwa porini, lakini Makubi hakukatishwa tamaa, akabahatika kuwa Padre na leo hii ni daktari. Yaani, hadi raha!

Rev. Dr. Mosha

 

 

18 December 2018, 10:46