Marekani:Maaskofu watoa msaada kwa ndugu wa Amerika ya Kusini!
Sr. Angela Rwezaula – Vatican
Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Marekani (USCCB) wametenga dola milioni 4 za kimarekani kwa ajili ya shughuli za Kanisa la Amerika ya Kusini, hizo ni fedha kwa ajili ya shughuli za kichungaji kwa vijana, katekesi na kusaidia kuinua watu katika maeneo yaliyokumbwa na majanga ya asili. Kwa mujibu wa taarifa kutoka habari za kimisionari Fides, kamati ndogo ya Baraza la Amerika ya Kusini katika Baraza la Maaskofu wa Marekani (USCCB), katika mkutano wake wa tarehe 10 Novemba 2018 uliofanyika huko Baltimore, imetenga zaidi ya dola milioni 3.2 kwa ajili ya kufadhili misaada 173 ili kusaidia shughuli za kichungaji katika Kanisa la Amerika ya Kusini na Caribbean; na karibu dola 800,000 kwa ajili ya misaada saba ya mipango ya ujenzi katika maeneo yaliyoharibiwa na tetemeko la ardhi huko Haiti na Mexico na kwa vimbunga vya Matthew, Maria na Irma.
Fedha kwa ajili ya miradi mingi ya mafunzo, kichungaji na ujinjilishaji huko Amerika ya Kusini
Kadhalikataarifa hiyo inaeleza kuwa wametenga fedha kwa ajili ya miradi ambayo inatakiwa kufanyika katika nchi kadhaa za kanda hilo. Kwa mfano, katika miradi ya Cuba na Equador imefadhiliwa kusaidia kuundwa mradi kwa ajili ya mafunzo ya watu walei na viongozi wa Kanisa, wakati nchini Uruguay na El Salvador, fedha zimepangwa kwa ajili ya mipango ya uinjilishaji na katekesi. Mpango mingine inayotarajiwa ni kusaidia watu wa asili katika nchi ya Brazil na Venezuela. Kamati ndogo pia imepitisha rasilimali muhimu kwa ajili ya msaada wa vijana katika huduma ya kichungaji na gharama ya usafiri kwa ajili ya washiriki watakaoudhuria Siku ya Vijana Duniani, itakayotarajiwa kufanyika nchini Panama kuanzia tarehe 22 hadi 27 Januari 2019, kutoka nchi mbalimbali za Amerika ya Kusini, ikiwa ni pamoja na Haiti, Peru na Quba na ili waungane pamoja na vijana wenzao kufanya maadhimisho hayo muhimu katika maisha yao.
Shukrani kwa wakatoliki wa Marekani kwa sababu ya ukarimu wao
Mkusanyo wa sadaka kwa Kanisa nchini Amerika unalengo kubwa sana kwa ajili ya watu wa kanda na kwa namna ya pekee katika mataifa yaliyo athirika. Hayo yamethibitishwa na Askofu Mkuu Paul Dennis Ettinee, wa Jimbo Kuu la Anchorage ambaye pia ni Rais wa Kamati ya makusanyo ya sadaka Kitaifa ya Baraza la Maaskofu Marekani. Kutokana na hilo, Askofu mkuu anachukua fursa hiyo kuwashukuru kwa dhati Wakatoliki wote nchini Marekani kwa ukarimu wao na mshikamano kwa ajili ya dada na kaka hao wa Amerika ya Kusini na visiwa vya Caribbean.
Jumapili ya nne ya mwezi Januari na mkusanyo maalum wa USCCB
Sadaka hizo kwa ajili ya huduma ya kichungaji zinapatikana kutokana na mkusanyo wa fedha wa mwaka kwa ajili ya Kanisa la Amerika ya Kusini na ambao utafanyika katika majimbo mengi katoliki ya Marekani katika siku ya Jumapili ya nne ya Mwezi Januari na wakati wa kipindi cha dharura na ujenzi, Baraza la Maaskofu wa Amerika (USCCB), uhamasisha makusanyo maalumu kwa ajili hiyo.