Vijana nchini Ufilippini wanahamasishwa kutembea katika mwanga wa Injili ya Kristo! Vijana nchini Ufilippini wanahamasishwa kutembea katika mwanga wa Injili ya Kristo! 

Kardinali Tagle: Vijana tembeeni katika mwanga wa Injili!

Kardinali Luis Antonio Chito Tagle katika ujumbe wake wa Noeli kwa Mwaka 2018 anapenda kukazia zaidi dhamana na nafasi ya vijana wa kizazi kipya katika maisha na utume wa Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Anasema, Sherehe za Noeli ni wakati muafaka wa kutakiana furaha na amani inayobubujika kutoka kwa Mtoto Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya  XXXIV ya Vijana Duniani itakayoadhimishwa kuanzia tarehe 22 -27 Januari 2019 huko Panama sanjari na maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana iliyoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya miito” ni sehemu ya mchakato wa utume wa Kanisa kwa vijana wa kizazi kipya! Mama Kanisa anataka kujenga sanaa na utamaduni wa kuwasikiliza na kutembea na vijana katika hija ya maisha yao, kwa kutambua kwamba, wao wana thamani kubwa sana mbele ya Mungu, Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Vijana wakumbuke kwamba, katika hija ya maisha yao, daima wanasindikizwa na Bikira Maria ambaye Mwenyezi Mungu alimtendea makuu katika maisha yake. Anawafundisha vijana kuangalia historia yao ya nyuma, kusikiliza kwa makini sauti ya Mungu inayowatia shime pamoja na kuwapatia neema ili kuweza kujibu kwa makini “Usiogope Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu”. Januari mwaka 2019, Panama itakuwa ni gumzo la watu wa mataifa kutokana na maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, yatakayowashirikisha vijana kutoka kila pembe ya dunia. Ni muda wa kutafakari vipaumbele vya maisha na utume wa vijana, changamoto, matatizo na fursa walizo nazo kama mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili.

Ni katika mwelekeo huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini, limetangaza kwamba, mwaka 2018-2019 ni Mwaka wa Vijana Kitaifa. Kardinali Luis Antonio Chito Tagle, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manila nchini Ufilippini katika ujumbe wake wa Noeli kwa Mwaka 2018 anapenda kukazia zaidi dhamana na nafasi ya vijana wa kizazi kipya katika maisha na utume wa Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Anasema, Jina la Yesu maana yake “Mungu anawaokoa watu wake” na kwa na namna ya pekee, Sherehe za Noeli ni wakati muafaka wa kutakiana furaha na amani inayobubujika kutoka kwa Mtoto Yesu.

Kristo Yesu ndiye Mfalme wa amani anayekuja kuwashirikisha waja wake furaha na amani na kwamba, vijana wa kizazi kipya nchini Ufilippini wanayo kila sababu ya kufurahia amani ya kweli na wala si amani mpito inayokuja na kutoweka kama ndoto ya mchana isiyokumbukwa kamwe! Nyimbo za Noeli zinafumbata ujumbe wa pekee kabisa kuhusu furaha na amani inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, changamoto na mwaliko wa kutembea katika mwanga wa Mtoto Yesu, unaofyekekelea mbali giza la dhambi na mauti.

Kardinali Tagle anasema, hii ni nafasi kwa vijana nchini Ufilippini kujikita katika kanuni na maadili mema, kwa kutembea katika mwanga wa Injili, upendo wa kweli unaokita mizizi yake katika utu na heshima ya binadamu. Upendo wa namna hii unapata asili yake kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wala si upendo wa nipe nikupe; hatari sana katika maisha ya vijana wa kizazi kipya! Upendo wa Mungu ni wa kweli na wala hauna mipaka na kwa namna ya pekee kabisa umefunuliwa kwa njia ya Mtoto Yesu, katika hali ya unyenyekevu pasi na makuu!

Kumbe, kipindi cha Noeli ni wakati muafaka wa kumwilisha furaha, amani, upendo na utulivu katika maisha ya watu kama ilivyokuwa kwa Mtoto Yesu, Mwana wa Baba wa milele. Wazee wanaomba msamaha kwa makwazo na mapungufu waliotenda katika maisha yao, kiasi hata cha kuitumbukiza dunia katika ombwe la giza la uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote; vita, kinzani na misigano inayohatarisha utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi. Wazee wanaomba msamaha kutokana na biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya, kichaka cha maovu miongoni mwa vijana pamoja na rushwa inayokwenda kinyume cha haki msingi za binadamu! Kristo Yesu aliyezaliwa, alete upya wa maisha kwa watu na jamii katika ujumla wake, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi!

Kardinali Tagle: Vijana
27 December 2018, 09:54