Vatican News
Monsinyo John Mutiso Mbinda, tarehe 14 Desemba 2018 ana adhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Upadre. Monsinyo John Mutiso Mbinda, tarehe 14 Desemba 2018 ana adhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Upadre.  (AFP or licensors)

Mons. John Mutiso Mbinda: Jubilei ya Miaka 50 ya Upadre! Yaani!

Monsinyo John Mutiso Mbinda kutoka Jimbo Katoliki la Machakos Kenya, ni kati ya wakleri walioshiriki katika Ibada ya Misa na Baba Mtakatifu Francisko Jumanne, tarehe 11 Desemba 2018 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, kama kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 14 Desemba 1968.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordia et misera” yaani “Huruma na amani” anasema, huruma ni kielelezo makini cha upendo wa Mungu unaosamehe, unaopyaisha na kubadili mwelekeo wa maisha; ni kielelezo cha ufunuo wa Fumbo la Mungu ambalo ni huruma ya milele inayowakumbatia na kuwaambata wote pasi na ubaguzi, kiasi cha kuwakirimia maisha mapya, chemchemi ya furaha na matumaini mapya yanayovunjilia mbali ubinafsi ili kutenda wema, kufikiri vyema na kuondoa huzuni moyoni. Huu ni mwaliko kwa waamini kufanya mang’amuzi ya huruma inayowakirimia furaha, hata kama maisha yao bado yanasheheni matatizo na changamoto mbali mbali, ili kuondokana na utamaduni wa huzuni, utupu na upweke unaopelekea msongo wa mawazo kwa watu wengi!

Mapadre wanakumbushwa kwamba, utume wao wa Kipadre unajikita katika Sakramenti ya Upatanisho inayopaswa kufumbatwa katika ukarimu, ushuhuda, huruma; ukweli na uwazi katika kanuni maadili. Mapadre wawe tayari kuwasindikiza waamini katika hija ya toba na wongofu wa ndani, kwa kuonesha uvumilivu; kwa kuwa na mawazo mapana na wakarimu katika kutoa msamaha wa Mungu. Mapadre pia wanapaswa kuwa ni kielelezo cha toba na wongofu wa ndani na kwamba, Sakramenti ya Upatanisho inapaswa kuwa ni kiini cha maisha ya Kikristo kwani Mapadre ni vyombo vya Upatanisho.

Monsinyo John Mutiso Mbinda kutoka Jimbo Katoliki la Machakos, nchini Kenya lakini kwa wakati huu, anatekeleza dhamana na utume wa shughuli za kichungaji kwenye Parokia ya Mtume Yohane Mwinjili, huko Honolulu, nchini Hawaii, ni kati ya wakleri walioshiriki katika Ibada ya Misa na Baba Mtakatifu Francisko Jumanne, tarehe 11 Desemba 2018 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, kama kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 14 Desemba 1968.

Katika maisha na utume wake, amewahi kuwa ni Katibu mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, yaani AMECEA kati ya mwaka 1982 hadi mwaka 1986. Amewahi pia kuwa ofisa katika Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo kuanzia mwaka 1986 hadi mwaka 2006 alipong’atuka kutoka katika huduma za kiofisi na kuelekea Jimbo Katoliki la Honolulu nchini Hawaii ambako anaendeleza huduma ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kama Paroko!

Monsinyo John Mutiso Mbinda anasema, Jubilei ni muda wa toba kwa mapungufu yaliyojitokeza, ni muda wa shukrani kwa neema na baraka kutoka kwa Mungu ni muda wa kujikabidhi kwa Mungu ili amwezeshe kuendelea kuwa mwaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, hadi siku ile, atakapokutana naye, kama Hakimu mwenye haki, tayari kurithi maisha ya uzima wa milele!

Mons. Mutiso Mbinda
11 December 2018, 15:43