Tafuta

Kardinali Bassetti: Amani ya kweli inafumbatwa katika: utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na upatanisho Kardinali Bassetti: Amani ya kweli inafumbatwa katika: utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na upatanisho 

Amani inafumbatwa katika utu wa binadamu, haki na upatanisho!

Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika hotuba yake ya ufunguzi wa Mwaka wa Masomo 2018-2019 kwenye Kitivo cha Taalimungu huko Puglia, Kusini mwa Italia alisema, amani ya kweli inafumbatwa katika haki msingi, utu na heshima ya binadamu pamoja na upatanisho. Inasikitisha kuna mataifa yanapimana nguvu kwa njia ya mtutu wa bunduki!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema maadhimisho ya Siku ya 52 ya kuombea amani kwa Mwaka 2019 yanaongozwa na kauli mbiu “Siasa safi ni huduma ya amani”. Siasa safi ni msingi wa maendeleo endelevu na fungamani; demokrasia shirikishi na uongozi bora unaojikita katika hoja zenye mashiko na huduma kwa wananchi. Siasa safi inafumbatwa katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi yanayowashirikisha wadau mbali mbali mbali katika jamii; marika pamoja na tamaduni, daima wakijitahidi kujenga imani kati yao kama sehemu ya kukuza na kudumisha amani.

Hivi karibuni, Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika hotuba yake ya ufunguzi wa Mwaka wa Masomo 2018-2019 kwenye Kitivo cha Taalimungu huko Puglia, Kusini mwa Italia alisema, amani ya kweli inafumbatwa katika haki msingi, utu na heshima ya binadamu pamoja na upatanisho. Jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, vita imekuwa kama njia ya kuweka uwiano katika Jumuiya ya Kimataifa kwa kupimana nguvu za kijeshi. Haya ndiyo yaliyopelekea Jumuiya ya Kimataifa ikajikuta ingia katika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia na hatimaye, Vita Kuu ya Pili ya Dunia; mambo ambayo yamevunja kwa kiasi kikubwa haki msingi za binadamu, utu na heshima yake na hivyo kujikuta akitumbukia katika majanga na maafa makubwa. Hata baada ya maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka mia moja tangu kusitishwa kwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, bado walimwengu wanatumbukia katika kishawishi  cha vita kama njia ya kutafuta suluhu kwa changamoto mbali mbali zinazomwandama mwanadamu.

Kardinali Gualtiero Bassetti anakaza kusema, kuna haja ya kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa kwa kujikita katika kanuni auni. Miaka 70 ya Tamko la Haki Msingi za Binadamu iwe ni changamoto ya kujikita katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika mshikamano; uhuru, daima ikijitahidi kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu, ili kufutilia mbali kishawishi cha wanasiasa kutumbukia katika ubaguzi wa rangi, jinsia, imani na mahali anapotoka mtu. Licha ya tofauti zao msingi, watu watambue kwamba, wanaunda familia moja ya watu wa Mungu.

Umoja huu unapaswa kufumbatwa katika nia njema, tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu, tayari kuwasha moto wa imani, matumaini na mapendo miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Umoja na mshikamano unaoongozwa na kanuni auni, uisaidie Jumuiya ya Kimataifa kupambana na changamoto mamboleo na kwamba, hakuna taifa lolote lile linaloweza kutatua changamoto hizi kwa kusimama peke yake! Eneo la Mediterrania ni muhimu sana kwa Bara la Ulaya katika kukuza na kudumisha amani, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba eneo hili linageuka kuwa ni jukwaa la matumaini ikilinganishwa na hali kwa sasa ambako Mediterrania imegeuka kuwa ni kaburi lisilo na alama. Dhamana ya kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu inapaswa kuvaliwa njuga na familia ya Mungu kuzunguka Bahari ya Mediterrania.

Dhambi ya utengano anasema Kardinali Bassetti inaendelea kuipekenya Jumuiya ya Kimataifa kiasi cha kutishia umoja na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa hata kwa mambo msingi kama vile utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, haki msingi za binadamu, utu na heshima yake! Kuna mgawanyiko mkubwa wa watu kadiri ya imani yao, siasa na uwezo wao wa kisilaha na kitikadi. Utengano miongoni mwa Wakristo umepelekea kuibuka kwa siasa kali na matumizi ya nguvu kupita kiasi. Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni kati ya changamoto changamani katika eneo la Bahari ya Mediterrania, lakini Kanisa litaendelea kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kama sehemu ya maisha na utume wake. Ukristo hauna budi kuwa ni kielelezo cha umoja na mshikamano unaovuka mipaka ya utaifa, imani, lugha, tamaduni, mila na desturi za watu!

Haki, amani na upatanisho

 

20 December 2018, 10:34