Tafuta

Askofu mkuu Beatus Kinyaiya: Boresheni maisha yenu ya kiroho na kutunza mazingira nyumba ya wote! Askofu mkuu Beatus Kinyaiya: Boresheni maisha yenu ya kiroho na kutunza mazingira nyumba ya wote! 

Askofu mkuu Kinyaiya: Muhimu: Sakramenti za Kanisa na Mazingira!

amewataka waamini kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kikristo, ili kushiriki kikamilifu Mafumbo ya Kanisa pamoja na kujizatiti katika ulinzi na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, changamoto endelevu na changamani kwa watanzania kwa sasa na kwa siku za usoni! Askofu mkuu Kinyaiya ameyasema, haya wakati wakati wa Noeli 2018.

Na Rodrick Minja, Dodoma & Padre Richard Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Beatus Kinyaia wa Jimbo kuu la Dodoma, nchini Tanzania amewataka waamini kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kikristo, ili kushiriki kikamilifu Mafumbo ya Kanisa pamoja na kujizatiti katika ulinzi na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, changamoto endelevu na changamani kwa watanzania kwa sasa na kwa siku za usoni! Askofu mkuu Kinyaiya ameyasema, haya wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Noeli kwa Mwaka 2018 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba.

Askofu mkuu Kinyaiya anasema, Sakramenti za Kanisa zinagusa hatua zote na nyakati zote muhimu katika maisha ya mwamini. Sakramenti zinaboresha maisha ya imani ya Mkristo; Kuzaliwa na kukua; kupona utume. Katika jambo hili kuna ufanano kati ya hatua mbali mbali za maisha ya mwanadamu na hatua za maisha ya kiroho. Kumbe, kwa waamini wanaoendelea kuishi katika “uchumba sugu” au “Usuria” watambue kwamba wanajiweka katika mazingira na hatari ya kukosa huduma ya Kanisa. Askofu mkuu Kinyaiya amewataka waamini wa Jimbo Katoliki la Dodoma kuhakikisha kwamba, wanarekebisha maisha yao ya Kisakramenti mapema iwezekanavyo, ili kujinasua kutoka katika shimo hili la uharibifu.

Askofu mkuu Kinyaiya ameitaka familia ya Mungu Jimbo kuu la Dodoma kuhakikisha kwamba, inasimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira nyumba ya wote, ili kupata amani na utulivu, ustawi na maendeleo ya wengi. Hii inatokana na ukweli kwamba, uchafuzi wa mazingira ni chanzo kikuu cha umaskini, njaa, magonjwa na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji. Askofu mkuu Kinyaiya amewataka watanzania kutunza mazingira ili mazingira nayo yawatunze. Askofu mkuu Kinyaiya anakaza kusema, Kanisa na Jamii ya Tanzania inaendelea kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu ili kuwapatia watanzania wengi: elimu, ujuzi na maarifa ya kupambana na hali yao, ili hatimaye, Tanzania iweze kuwa ni mahali pazuri zaifi pa kuishi. Kumbe, wanafunzi katika ngazi mbali mbali za masomo wametakiwa kuwa waaminifu, waadilifu na watu wenye bidi katika masomo, ili kujijengea maisha bora zaidi kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Askofu mkuu Kinyaiya amewataka wanafunzi kuwa makini na matumizi ya simu za viganjani kwani zina faida kubwa katika tasnia ya mawasiliano lakini, pia ni sawa na upanga wenye makali kuwili, mitanda hii ikitumiwa vibaya ni chanzo cha kukengeuka na kuopea katika maadili na utu wema. Kumbe, vijana wanatakiwa kutumia vyema mitandao ya kijamii kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Askofu mkuu Kinyaiya ameipongeza Serikali kwa kuendelea kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watanzania. Amewataka watanzania kutambua kwamba, ulinzi, usalama na amani nchini Tanzania ni dhamana na wajibu wa watanzania wote.

Kumbe, watanzania wahakikishe kwamba, wanajizatiti kulinda, kutunza na kudumisha amani ambayo kimsingi ni jina jipya la maendeleo endelevu na fungamani. Waamini waendelee kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake; kwa kujenga umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa daima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi vikipewa kipaumbele cha kwanza.

Askofu Mkuu Beatus

 

 

28 December 2018, 14:47