Tafuta

Vatican News
Askofu mkuu mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwa'ichi anasema kuwekeza kwenye Uinjilishaji wa familia ni jambo muhimu sana kwa wakati huu! Askofu mkuu mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwa'ichi anasema kuwekeza kwenye Uinjilishaji wa familia ni jambo muhimu sana kwa wakati huu! 

Askofu mkuu mwandamizi Ruwa'ichi: Injili ya familia muhimu!

Familia ni Kanisa dogo la nyumbani; ni kitalu cha uhai; shule ya maadili, utu wema na uwajibikaji. Ni chimbuko la miito mitakatifu ndani ya Kanisa, yaani wito wa ndoa na familia, daraja takatifu na maisha ya kuwekwa wakfu. Lakini pia familia ni shule ya mahusiano na mafungamano ya kijamii; hapa ni mahali pa kwanza pa kutekeleza utume na ushuhuda wao kama Wakristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia katika jamii. Kanisa linatambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, ni shule ya utakatifu haki na amani; ni mahali pa kujifunzia fadhila mbali mbali za Kikristo, kiutu na kijamii! Lakini, familia katika ulimwengu mamboleo inakabiliwa na changamoto pevu kama zilivyoainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”.

Injili ya Kristo ni chemchemi inayowapatia wanafamilia ari, nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa nyakati hizi kwa kuzingatia tunu msingi za Injili ya familia mintarafu Mafundisho ya Kanisa. Ili kuweza kukabiliana na changamoto zote hizi, Baba Mtakatifu Francisko kunako 15 Agosti 2016 alianzisha Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kama sehemu ya mchakato wa Sekretarieti kuu ya Vatican kusoma alama za nyakati na kujibu kwa ufasaha na weledi mkubwa changamoto mamboleo katika maisha na utume wa Kanisa.

Askofu mkuu Mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam katika mahojiano maalum na Vatican News anafafanua zaidi kwa kusema, familia ni Kanisa dogo la nyumbani; ni kitalu cha uhai; shule ya maadili, utu wema na uwajibikaji. Ni chimbuko la miito mitakatifu ndani ya Kanisa, yaani wito wa ndoa na familia, daraja takatifu na maisha ya kuwekwa wakfu. Lakini pia familia ni shule ya mahusiano na mafungamano ya kijamii; hapa ni mahali pa kwanza pa kutekeleza utume na ushuhuda wao kama Wakristo.

Askofu mkuu Mwandamizi Ruwa’ichi anasikitika kusema kwamba, zama mamboleo si rafiki sana kwa Injili ya familia, kwani familia aidha inabezwa au inapigwa vita au inamomonyolewa kiholela kadiri ya vionjo vya watu na vipaumbele vyao sahihi au potofu. Ili familia iwe ya Kikristo na iweze kutekeleza vyema dhamana, wajibu na utume wake mzito; ili iweze kuwa ni mahali pa kukua na kutakatifuzana; ili iweze kuwa ni chimbuko la miito yote ndani ya Kanisa ni lazima familia hiyo Iinjilishwe, itetewe, ishauriwe na kutakatifuzwa.

Kwa hiyo kuna uhitaji mkubwa wa ukaribu wa kichungaji dhamana na wajibu unaopaswa kutekelezwa kikamilifu na mihimili yote ya uinjilishaji ili kuwa karibu na familia, ili hatimaye, kuzitegemeza, kuzisaidia, kuzichangamotisha na kuzilinda. Askofu mkuu Mwandamizi Thaddeus Ruwa’ichi anakaza kusema, ni muhimu kwa familia zenyewe kwa kadiri ya urika wa wanafamilia awezeshwe kuifanya familia kuibuka ikiwa imara, thabiti na uhai na pia mihimili ya kuitegemeza katika changamoto mamboleo. Utume wa familia ni endelevu na kwamba, hili ni jambo muhimu sana katika ulimwengu mamboleo kuwekeza katika kuinjilisha familia kwani hili ni eneo muhimu sana!

Ruwa'ichi: Injili ya familia
29 December 2018, 14:37