Tafuta

Askofu mkuu Justin Welby: Ujumbe wa Noeli kwa Mwaka 2018 Askofu mkuu Justin Welby: Ujumbe wa Noeli kwa Mwaka 2018 

Sherehe za Noeli: Kanisa linao ujumbe wa amani na matumaini!

Mababa wa Kanisa wanasema, dhahabu ni alama ya ufalme wa Kristo. Huu ni ufalme wa milele na wa ulimwengu wote; ni ufalme wa kweli na uzima, utakatifu, haki, upendo na amani! Uvumba ni alama ya Umungu wa Kristo, yaani Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Manemane ni kielelezo cha ubinadamu wake, Kristo Yesu aliyezaliwa kwake Bikira Maria, akateswa, akafa na kufufuka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwinjili Mathayo anaposimulia hija ya Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali anasema kwamba, wakaingia nyumbani, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia. Nao walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu: dhahabu, uvumba na manemane. Mababa wa Kanisa wanasema, dhahabu ni alama ya ufalme wa Kristo. Huu ni ufalme wa milele na wa ulimwengu wote; ni ufalme wa kweli na uzima, utakatifu, haki, upendo na amani! Uvumba ni alama ya Umungu wa Kristo, yaani Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Manemane ni kielelezo cha ubinadamu wake, Kristo Yesu aliyezaliwa kwake Bikira Maria, akateswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Hii ni sehemu ya barua ya kiekumene katika maadhimisho ya Sherehe ya Noeli kwa Mwaka 2018 kutoka kwa Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Canterbury ambaye pia ni kiongozi mkuu wa Kanisa la Kiangalikani. Barua hii inaongozwa na kauli mbiu “Kama Wakristo tunayo Habari Njema”, zawadi ambayo wanataka kuwapatia walimwengu katika maadhimisho ya Sherehe ya Noeli, yaani kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu. Noeli ni kipindi cha kutoa na kupokea zawadi na kwamba, zawadi ni kiini cha Fumbo la Umwilisho kama lilivyofafanuliwa na Mwinjili Mathayo. Zawadi hizi ni: Asili na Umungu wa Kristo; Ufalme na Ukuhani wake wa milele sanjari na Ubinadamu wake unaofumbatwa katika mateso, kifo na ufufuko.

Askofu mkuu Justin Welby anaendelea kufafanua kwamba, hizi ni tunu ambazo ni a ghali, lakini Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali waliamua kumtolea Mwenyezi Mungu kwa njia ya Mtoto Yesu, alama ya upendo usiokuwa na kifani na kielelezo cha neema ya Mungu iliyoletwa kwa njia ya Fumbo la Umwilisho. Kristo Yesu ni zawadi kwa walimwengu, ni ufunuo wa utukufu wa Mungu na mwaliko wa kumtolea Mwenyezi Mungu sifa, ukuu na shukrani. Neno wa Mungu alipofanyika mwili na kukaa kati ya watu wake, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam mauti ya Msalaba. Kwa njia ya Kristo Yesu, Mwenyezi Mungu amejipatanisha na ulimwengu, zawadi kubwa kwa binadamu!

Askofu mkuu Justin Welby anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumtolea Mwenyezi Mungu sifa na shukrani, kwa zawadi kuu aliyoupatia ulimwengu, yaani Mwanaye mpendwa Kristo Yesu, sasa ni wakati wa kumpenda na kumtumikia. Ulimwengu mamboleo unaendelea kuogelea katika dimbwi la hofu, mashaka na majanga mbali mbali yanayomwandama mwanadamu, lakini kama Wakristo, wanayo Habari Njema ya Wokovu, kama walivyotangaziwa Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali kwamba, Mwenyezi Mungu amewapatia walimwengu zawadi ya Mwanaye wa pekee. Shukrani kwa Mungu inafumbatwa katika toba, wongofu wa ndani; upendo na msamaha kwa jirani. Hata katika mapungufu yao kama binadamu, bado wataendelea kuwa ni watoto wa Mungu.

Katika ulimwengu unaoendelea kugubikwa kwa umaskini wa hali na kipato, watu wanataka kusikia tena na tena Habari Njema ya Wokovu, inayobubujika kutoka kwenye chemchemi ya ukarimu wa Kristo. Mahali ambapo mtutu wa bunduki unaendelea kurindima; watu wanateseka na kulazimika kuyakimbia makazi yao, hata wao wanatamani kusikia Habari Njema kutoka kwa Kristo Mfalme wa amani. Ni matumaini ya Askofu mkuu Justin Welby kwamba, katika kipindi hiki cha Sherehe ya Noeli, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wataweza kukirimiwa matumaini, amani na furaha ya kweli kutoka kwa Kristo Yesu!

Askofu Mkuu Welby: Noeli

 

24 December 2018, 09:37