Tafuta

Vatican News
Askofu mkuu mteule Gervas Nyaisonga wa Jimbo kuu la Mbeya anawataka watanzania kutunza mazingira, kulinda afya zao na kumisha amani. Askofu mkuu mteule Gervas Nyaisonga wa Jimbo kuu la Mbeya anawataka watanzania kutunza mazingira, kulinda afya zao na kumisha amani. 

Askofu mkuu Nyaisonga: Ujumbe wa Noeli kwa Mwaka 2018

Askofu mkuu mteule Gervas Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, katika ujumbe wake wa Noeli kwa mwaka 2018 na baraka kwa Mwaka mpya wa 2019 anapenda kuwahimiza watanzania kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kujikita katika utamaduni wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Na Suzan Kaneka-Mpanda, Tanzania & Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S  - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anaiita dunia kuwa “Nyumba ya wote” ambayo tunawajibika sote kuitunza. Hakuna mwenye milki binafsi juu ya dunia isipokuwa Mungu tu. Hivi yeyote anayeiharibu kwa namna yoyote ile anamsaliti Mungu, anasaliti binadamu na ubinadamu. Dunia ni “mama na mkunga”, anasema Mtakatifu Yohane Krisostom, “imeumbwa na Mungu ili kumtunza mwanadamu” (Krisostom, Homilies on Genesis, 9.3). Kwa bahati mbaya, mwanadamu ameonekana hajali na anaharibu uumbaji kwa kiwango cha kutisha. Kazi ya mikono ya mwanadamu sasa inasababisha uharibifu kwa kazi ya mikono ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, “Mungu alitupatia dunia iliyosheheni zawadi nyingi, lakini tumeigeuza kuwa nchi iliyoharibiwa kwa uchafuzi wa takataka, ukiwa na uchafu.”

Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, ni mada iliyojadiliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa mwaka 2017. Askofu mkuu mteule Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga wa Jimbo kuu la Mbeya ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, katika ujumbe wake wa Noeli kwa mwaka 2018 na baraka kwa Mwaka mpya wa 2019 anapenda kuwahimiza watanzania kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kujikita katika utamaduni wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Askofu mkuu mteule Nyaisonga anaendelea kusema, Sherehe za Noeli ni wakati wa kutafakari kuhusu Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu anapozaliwa tena katika maisha ya waja wake, ili kuwapatia uzima na maisha mapya. Ni wakati wa kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Lakini, ikumbukwe kwamba, Injili ya uhai inategemea kwa kiasi kikubwa utunzaji bora wa mazingira kwa kuondokana na kishawishi cha uchafuzi wa mazingira na vyanzo vya maji. Watu wanahitaji maji safi na salama ili kuendeleza afya zao, kumbe, watanzania wajenge utamaduni wa kutunza vyanzo vya maji.

Askofu mkuu mteule Nyaisonga anawataka watanzania kulinda na kutunza vyema afya zao; kwa kupambana dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI; kwa kujilinda, kupima na kujua afya zao; kutowanyanyapaa waathirika wa ugonjwa wa UKIMWI, bali kuwalinda na kuwasaidia; kwa kuwapatia mahitaji yao msingi pamoja na dawa za kupambana na magonjwa nyemelezi. Watanzania wajitahidi kuishi na waathirika wa ugonjwa wa UKIMWI kwa huruma na upendo. Ameishauri Serikali kuongeza juhudi katika maboresho ya sekta ya afya; kwa kuboresha mazingira, huduma na vifaa tiba. Waganga na wauguzi wawasaidie akina Mama wajawazito kudhibiti maambukizi ya UKIMWI.

Askofu mkuu mteule Nyaisonga anawataka watanzania kuwa ni vyombo na wajenzi wa amani, upendo na mshikamano wa dhati; kwa kupinga ukatili unaotendeka mara nyingi wakati wa Sherehe. Watu wawe na kiasi katika matumizi ya pombe, kwani vitendo vyote vinavyokatisha uhai wa mwanadamu ni kinyume cha maadhimisho ya Sherehe za Noeli. Huu ni muda wa toba na wongofu wa ndani, tayari kutembea katika mwanga wa Fumbo la Umwilisho.

Noeli 2018 Tanzania
24 December 2018, 10:47