Tanzia: Askofu mkuu mstaafu John Njenga wa Jimbo kuu la Mombasa, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 90 Tanzia: Askofu mkuu mstaafu John Njenga wa Jimbo kuu la Mombasa, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 90 

TANZIA: Askofu mkuu mstaafu John Njenga amefariki dunia!

Marehemu Askofu mkuu mstaafu John Njenga atazikwa, Jumanne tarehe 13 Novemba kwenye Kanisa kuu la Familia Takatifu Jimbo kuu la Nairobi. Ibada hii ya Misa Takatifu, itatanguliwa na mkesha utakaoanza Jumatatu, tarehe 12 Novemba 2018 majira ya jioni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu mstaafu John Njenga wa Jimbo kuu la Mombasa, Kenya, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 90 Jumapili, tarehe 4 Novemba 2018 kwenye Hospitali ya Mater Misericordiae iliyoko Jijini Nairobi baada ya kuugua kwa muda mfupi! Marehemu Askofu mkuu mstaafu Njenga atazikwa, Jumanne tarehe 13 Novemba, 2018 kwenye Kanisa kuu la Familia Takatifu Jimbo kuu la Nairobi. Ibada hii ya Misa Takatifu, itatanguliwa na mkesha utakaoanza Jumatatu, tarehe 12 Novemba 2018 majira ya jioni!  

Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde wa Jimbo kuu la Mombasa anasema, familia ya Mungu nchini Kenya itamkumbuka sana Marehemu Askofu mkuu mstaafu John Njenga kwa majitoleo na sadaka yake kwa ajili ya huduma kwa familia ya Mungu nchini Kenya. Alijitosa bila kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na ustawi wa familia ya Mungu nchini Kenya hususan katika sekta ya elimu kama chachu ya ukombozi kwa watu wengi. Amewahi pia kuwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya kuanzia mwaka 1976 hadi mwaka 1982.

Itakumbukwa kwamba, alizaliwa tarehe 25 Desemba 1928 huko Tigoni, Wilaya ya Kiambu, akiwa ni mtoto wa Marehemu Mzee Peter Kimani na Maria Wanjiru. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, tarehe 17 Februari 1957 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwenye Seminari kuu ya Falsafa, Kibosho, Jimbo Katoliki la Moshi, Tanzania.

Tarehe 19 Oktoba 1970 Mtakatifu Paulo VI akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Eldoret na wakati wa kuwekwa wakfu kama Askofu, akambatiza Mama yake mzazi, Maria Wanjiru! Kwa hakika, hii ilikuwa ni siku ya furaha na ushuhuda wa neema na zawadi ya imani iliyokuwa inaingia kwenye familia ya Mzee Peter Kimani. Tarehe 25 Oktoba 1988 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Mombasa. Na tarehe 21 Mei 1990, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteua kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo kuu la Mombasa.

Tarehe Mosi, Aprili 2005, akang’atuka kutoka madarakani. Tangu wakati huo, akaendelea kujiwekea “akiba ya mafuta” huku akimngojea Bwana arusi, ili atakapokuja, aweze kumlaki huku akiwa na taa ya imani inayoendelea kuwaka! Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya katika salam zake za rambi rambi, amemwelezea Marehemu Askofu mkuu mstaafu John Njenga wa Jimbo kuu Mombasa kuwa ni kiongozi aliyekuwa na mwono mpana, aliyesimama kidete katika mchakato wa maboresho ya sekta ya elimu nchini Kenya, akajenga shule nyingi, ili kuwapatia watoto wa Kenya nafasi ya kupambana na ujinga katika maisha yao, kama sehemu ya mchakato wa ukombozi wa mwanadamu: kiroho na kimwili. Anakumbukwa kwa kujenga shule 40 wakati alipokuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Eldoret! Rais Kenyatta anasema, kwa hakika alikuwa ni “Mzee wa shoka, hapana mchezo”.

Askofu mkuu Njenga

 

08 November 2018, 14:04