Tafuta

Vatican News
Ni wakati wa amani sasa nchini Sudan Ni wakati wa amani sasa nchini Sudan  (AFP or licensors)

Sudan:ni wakati wa amani kutoka Kaskazini hadi milima ya Nuba!

Maaskofu wa Sudan wameandika ujumbe wao, mara baada ya Mkutano wa mwaka wakipongeza kutiwa saini ya Rais Salva Kiir na Riek Machar katika mkataba ili kufikia mapatano ya kusitisha vita na kukomesha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe

Sr. Angela Rwezaula - Vatican

“Ni wakati wa amani sasa kutoka Kaskazini hadi milima ya Nuba. Ni furaha kubwa kutokana na mkataba wa amani uliotiwa saini huko Sudan na kututia moyo kwa ajili ya mchakato wa mazungumzo kati ya Serikali na wapinzani wake”. Ni maelezo yaliyomo katika ujumbe wa Maaskofu wa Sudan mara baada ya Mkutano wao mkuu mapema wiki hii uliofanyika mjini Khartoum.

Kiini cha ujumbe wao kimejikita katika waraka wao, wa tarehe 12 Septemba 2018 kwa Rais Salva Kiir na Riek Machar, ambao kwa karibia miaka 5 wamedumu katika mapigano ya silaha huko juba.  Ikumbukwe kwamba mazungumzo kati ya mahasimu wawili wa kisiasa yaani, Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na makamu wake wa zamani, Riek Machar kwa ajili ya kufikia mapatano ya kusitisha vita na kukomesha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yalifanyika miezi ya hivi karibuni, katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum, chini ya mpatanishi Rais wa Sudan,Bwana  Omar al Bashir. Pande hasimu ziliafikiana kuhusu usitishaji vita wa kudumu, lakini wakati huo huo kulibaki wasiwasi kwamba mapatano hayo yasingeweza kudumu na kusambaratika kufuatia na uzoefu wa nyuma.

Kutokana na mkataba huo, Maaskofu wa Sudan wanashukuru wale wote  waliotoa mchango wao ili kufikia mkataba wa amani na wanayo  matumaini ya kuwa, inawezakana kabisa kufikia hatua ya dhati ya matendo ya mkataba ambao ni muhimu, na  hivyo ni lazima kuwa makini na kuzingatia ahadi hizo. Katika waraka wao wa mwisho wanakumbusha hata juu ya majukumu ambayo yametolewa na wapatanishi wa Rais Kiir kulingana na migogoro hiyo.

Hiyo ni kutokana na kwamba Sudan Kusini ilijitenga na Sudan mwaka 2011 na katika vyanzo mbalimbali vya habari vinasema sababu ilikuwa  ni mashinikizo na ushawishi wa nchi za Magharibi. Nchi hiyo changa zaidi duniani ilitumbukia katika vita vya ndani mwaka 2013, baada ya kiongozi wa sasa wa nchi hiyo, Salva Kiir kumtuhumu aliyekuwa makamu wake, Riek Machar kuwa alifanya jaribio la kupindua serikali yake.

Maaskofu wa Sudan wako tayari kusaidia kila jitihada

Maaskofu wanaandika kuwa, wako tayari kusaidia kila aina ya jitihada ambazo zitapelekea msimamo wa amani katika maeneo hayo yaliyokumbwa na migogoro nchini Sudan ili nchi yote iweze siku kumoja kuonja na kufarijika  wakati endelevu wa amani. Ujumbe huo wa Baraza la Maaskofu wa Sudan na Sudan ya kusini umetiwa saini kuanzia na Rais wa Baraza la Maaskofu, Askofu Eduardo Hiliboro Kussala.

14 November 2018, 14:10