Cerca

Vatican News
Patriaki Tawadros II atuma ujumbe wa imani, matumaini na umoja wa kitaifa dhidi ya vitendo vya kigaidi nchini Misri. Patriaki Tawadros II atuma ujumbe wa imani, matumaini na umoja wa kitaifa dhidi ya vitendo vya kigaidi nchini Misri.  (ANSA)

Patriaki Tawadros II: Imani ina nguvu kuliko hata vitisho na kifo

Vitendo vya kigaidi vina madhara makubwa katika maisha ya wananchi wa Misri kwani vinavuruga umoja na mafungamano ya kijamii, lakini kwa Wakristo mashambulizi ya kigaidi yamewaimarisha zaidi katika umoja na mshikamano wa kiimani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili, tarehe 4 Novemba 2018 aliwakumbuka na kuwaombea mahujaji 21 wa Kanisa la Kikoptik la Kiorthodox la Alexandria nchini Misri waliouwawa wakati wa shambulio la kigaidi lililotokea hapo tarehe 2 Novemba 2018. Mahujaji hawa wameuwawa kutokana na chuki za kidini kwa sababu tu kwamba, walikuwa ni Wakristo! Taarifa kutoka Misri inaonesha kwamba, magaidi 19 wameuwawa na vyombo vya ulinzi na usalama nchini Misri.

Patriaki Tawadros wa pili wa Kanisa la Kikoptik la Kiorthodox la Alexandria, Misri katika ujumbe wake baada ya shambulizi hili la kigaidi anasema, imani ina nguvu zaidi kuliko chuki na uhasama. Vitendo vya kigaidi vina madhara makubwa katika maisha ya wananchi wa Misri kwani vinavuruga umoja na mafungamano ya kijamii, lakini kwa Wakristo mashambulizi ya kigaidi yamewaimarisha zaidi katika umoja na mshikamano wa kiimani. Huu ni ujumbe wa imani, matumaini, umoja na mshikamano wa kitaifa. Mashambulizi ya kigaidi yamefanywa dhidi ya mahujaji wa Kikristo waliokuwa wanakwenda hija kwenye Monasteri ya Mtakatifu Samueli, mwongofu!

Patriaki Tawadros wa pili anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wale wote waliopoteza maisha yao kutokana na chuki za kidini. Hawa ni waamini waliofariki dunia wakiwa na matumaini katika maisha na uzima wa milele, Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo, awarehemu na hatimaye, kuwakirimia maisha na uzima wa milele. Viongozi wa Kanisa wanamshukuru Rais Abdel Fattah Al-Sisi, Baraza la Mawaziri pamoja na wahudumu katika sekta ya afya waliojitahidi kuokoa maisha ya mahujaji wale. Serikali imeamua kuwalipa kifuta machozi, wale wote waliofikwa na majanga haya.

Patriaki Tawadros wa pili anaialika familia ya Mungu nchini Misri kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa licha ya tofauti zao msingi katika imani, ili kuendeleza: usalama na amani kwa watu wote bila ubaguzi. Wanawaombea hata wale waliosababisha mauaji haya, ili waweze kutambua uzito wa makosa yao, tayari kumwongokea Mungu kwa toba na wongofu wa ndani kadiri ya imani yao. Mashuhuda wa imani waliouwawa kikatiliki kutokana na chuki za imani “Odium fidei” ni chachu ya kusonga mbele kwa imani na matumaini katika maadhimisho ya Liturujia mbali mbali za Kanisa, kwa kuwakumbuka na kuwaombea, ili Kanisa liendelee kuwa aminifu kwa Kristo Yesu.

Salam za rambi rambi zimetolewa pia na Ahmad Muhammad Al-Tayyib, Imam mkuu wa Msikiti mkuu wa Al-Azhar, ulioko Cairo, nchini Misri aliyepiga simu na kuzungumza moja kwa moja na Patriaki Tawadros wa pili, kuonesha masikitiko yao kutokana na mashambulizi haya ya kigaidi. Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 2017, shambulizi ya kigaidi lilisababisha mauaji ya watu 30 na wakati wa maadhimisho ya Jumapili ya Matawi tarehe 9 Aprili, 2017, magaidi walishambulia Kanisa kuu la Mtakatifu Marko mjini Alessandria na lile la Mtakatifu George na kusababisha watu zaidi ya hamsini kupoteza maisha.

Tawadros II

 

07 November 2018, 11:57