Cerca

Vatican News
Shirika la Mateso linaadhimisha Jubilei ya Miaka 300 tangu kuanzishwa kwake na Mtakatifu Paulo wa Msalaba Shirika la Mateso linaadhimisha Jubilei ya Miaka 300 tangu kuanzishwa kwake na Mtakatifu Paulo wa Msalaba   (ANSA)

Jubilei ya miaka 300 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Mateso!

Jubilei ya Miaka 300 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Mateso ni fursa ya kupyaisha maisha na utume wao, ni muda wa kushuruku na kuendelea kujikita katika unabii unaofumbatwa katika matumaini. Hii ni nafasi ya kupyaisha maisha ya kijumuiya, kwani utume wa Shirika unapata chimbuko lake katika ushuhuda wa umoja na maisha ya kidugu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Mateso maarufu kama “Wapasionisti” linaadhimisha Jubilei ya Miaka 300 tangu kuanzishwa kwake na Paulo Francesco, ambaye baadaye alianza kutambulikana kama Paulo wa Msalaba, aliyezaliwa kunako mwaka 1674, akafariki dunia mwaka 1775 na kutangazwa kuwa Mtakatifu mwaka 1867. Kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei hii, Baba Mtakatifu Francisko amewataka Wapasionisti kujikita katika mchakato wa upyaisho wa maisha na utume wao, kama kielelezo cha shukrani, unabii na utume. Amewataka wawe ni vyombo na mashuhuda wa utume wa uponyaji na upatanisho, ili kutangaza na kushuhuda wema, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Baba Mtakatifu anasema, kama sehemu ya utekelezaji wa sera na mikakati ya uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko, Wapasionisti wanaitwa na kutumwa kwenda pembezoni mwa vipaumbele vya jamii ili kuwatangazia watu wa Mungu furaha ya Injili, daima wakijiachilia chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu katika mchakato wa uinjilishaji unaojikita katika kipaji cha ugunduzi. Wapasionisti wakumbuke kwamba, huruma na upendo wa Mungu vimefunuliwa katika Fumbo la Msalaba,yaani katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kwa wafu!

Itakumbukwa kwamba, Shirika la Mateso lilianzishwa tarehe 22 Novemba 1720 na Mtakatifu Paulo wa Msalaba baada ya kufanya tafakari ya kina na mapana kwa muda wa siku arobaini, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu Jangwani kabla ya kuanza utume na maisha yake ya hadhara. Akiwa amejichimbia kwenye Kanisa la Carlo huko Castellazzo, akatunga Katiba ya Shirika kwa ajili ya “maskini wa Yesu”. Haikuwa ni kazi rahisi sana, kwani Mtakatifu Paulo wa Msalaba alikumbana na matatizo na changamoto za maisha, hadi pale Papa Benedikto XIII alipomruhusu kuanza kukusanya vijana watakaojisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Padre Joachim Xavier Rego, Mkuu wa Shirika la Mateso aliyechaguliwa hivi karibuni, kuliongoza Shirika kwa awamu ya pili anasema kwamba, kwao tarehe 22 Novemba ndiyo siku ya kuanzishwa kwa Shirika lao! Familia ya Mateso imeongezeka na kupanuka kwa kiasi kikubwa, kwani ina Shirika la watawa wa ndani, Mashirika matano ya watawa wa kike pamoja mkondo wa waamini walei wanaotaka kushiriki katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Injili ya mateso ya Kristo duniani, inayofumbata kimsingi: huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu!

Padre Joachim Xavier Rego anaendelea kufafanua kwamba, Jubilei ya Miaka 300 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Mateso ni muda muafaka wa: kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa matendo yake makuu aliyowakirimia! Ni fursa ya kufanya toba na wongofu wa ndani, tayari kuomba huruma na neema ya kusonga mbele kwa imani, matumaini na mapendo, tayari kutangaza na kushuhudia ukuu na utukufu wa Mungu unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba. Ni muda wa kuwakumbuka Wapasionisti wote waliojisadaka, wakawa waaminifu kwa Kristo, Kanisa na Karama ya Shirika, kiasi cha kushuhudia upendo wa Mungu unaobubujika kutoka katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu.

Kamwe, tukio hili lisigeuzwe kuwa ni sehemu ya mapito ya kihistoria, bali fursa ya kukua na kukomaa katika maisha ya kiroho na utume wa Shirika, kwa kuendelea kutamadunisha na kuimwilisha karama ya Mtakatifu Paulo wa Msalaba kama njia ya kuimarisha utambulisho wa Wapasionisti, ili hatimaye kulipatia Shirika “Sura ya Kiinjili” inayopendeza na kuleta mvuto. Shirika la Mateso linaendelea kupambana na hali yake, kwa wanashirika wengi kutoka Ulaya, Amerika na Australia kuendelea kuzeeka. Lakini, Shirika linafarijika kwa kupata “Majembe mapya na yenye nguvu” kutoka Afrika, Asia na Amerika ya Kusini.

Shirika linapaswa kujikita katika uaminifu unaofumbatwa katika ugunduzi kama njia ya kumbu kumbu endelevu ya mateso na kifo cha Kristo kinachokomboa na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Jubilei ya Miaka 300 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Mateso ni fursa ya kupyaisha maisha na utume wao, ni muda wa kushuruku na kuendelea kujikita katika unabii unaofumbatwa katika matumaini. Hii ni nafasi ya kupyaisha maisha ya kijumuiya, kwani utume wa Shirika unapata chimbuko lake katika ushuhuda wa umoja na maisha ya kidugu!

Shirika la Mateso
27 November 2018, 08:18