Tafuta

Vatican News
Miaka 100 tangua kuanzishwa kwa ILO: Ushauri wa COMECE Miaka 100 tangua kuanzishwa kwa ILO: Ushauri wa COMECE  (ANSA)

Tamko la COMECE: Kumbu kumbu ya Miaka 100 ya ILO Duniani!

Tume ya Mabaraza ya Maaskofu Barani Ulaya, COMECE kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Kazi Duniani, ILO kunako mwaka 1919 mara tu baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia imeandaa Waraka kuhusu “Kazi kwa Siku za Usoni” kutokana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa kidigitali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni aliwakumbusha waamini wa mji wa Geneva kwamba, takribani miaka 600 iliyopita, Papa Martino V alipata nafasi ya kutembelea mjini humu. Geneva ni makao makuu ya Mashirika ya Kimataifa na kati yake ni Shirika la Kazi Duniani, ILO, ambalo mwaka 2019 linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake.

Ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, ukuaji hafifu wa uchumi kitaifa na kimataifa pamoja na hupatikanaji wa kazi zenye staha na zinazoheshimu utu na heshima ya binadamu ni kati ya changamoto endelevu kwa Shirika la Kazi Duniani. Kazi inapaswa kutambuliwa kuwa ni chanzo cha mapato na sehemu muhimu sana ya utambulisho wa utu na heshima ya binadamu. Kazi inamwezesha mwanadamu kutambua dhamana na wajibu wake ndani ya jamii na hivyo kusaidia kukoleza ustawi na maendeleo ya mtu binafsi pamoja na kusaidia mchakato wa kuitengeneza dunia ili iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, kwa kuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi!

Tume ya Mabaraza ya Maaskofu Barani Ulaya, COMECE kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Kazi Duniani, ILO kunako mwaka 1919 mara tu baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia imeandaa Waraka kuhusu “Kazi kwa Siku za Usoni” kutokana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa kidigitali, kuna haja ya kuwa na mwono mpana zaidi na ulio wa wazi kuhusu masuala ya kazi na kama sehemu ya maandalizi ya uchaguzi kwenye Umoja wa Ulaya!

COMECE inalitaka Shirika la Kazi Duniani kuhakikisha kwamba, linasaidia mchakato wa maboresho ya kazi kwa kuzingatia utu na heshima ya binadamu; kwa kuweka sera na mipango ya kazi endelevu na shirikishi, hasa kutokana na changamoto inayoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa kidigitali ili kweli uchumi uweze kuwa ni sehemu ya huduma ya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu! Waraka huu unakazia pamoja na mambo mengine, maendeleo endelevu kama mhimili mkuu wa uwekezaji kutoka katika sekta binafsi; ushiriki wa jamii na Makanisa; umuhimu wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kijamii katika ngazi mbali mbali.

ILO iendelee kuwasaidia wafanyakazi katika kipindi hiki cha mpito kuelekea katika ulimwengu wa kidigitali; kuibu sera na mbinu mkakati wa kupambana na ukosefu wa fursa za ajira kwa muda mrefu zaidi. Jitihada hizi hazina budi kwenda sanjari na ukuzaji wa haki ya kifedha kati ya kazi na mtaji pamoja na kuhakikisha kwamba, sheria, kanuni na taratibu za soko la fedha zinazingatiwa na kuheshimiwa na wote!

Shirika la Kazi Duniani linapania pamoja na mambo mengine kudumisha haki msingi za binadamu maeneo ya kazi, maboresho ya mazingira ya kazi na vitendea kazi; kuendeleza na kudumisha hifadhi ya jamii sanjari na kukuza majadiliano katika masuala ya kazi! Utu wa mwanadamu ndicho kipimo cha heshima ya kazi na haki jamii inayopatikana kwa njia ya utu na heshima katika mchakato mzima wa kazi ya mwanadamu. Hizi ni tunu msingi ambazo zimekuwa ni mihimili mikuu katika Mapokeo na mafundisho ya dini mbali mbali duniani. Katika kipindi hiki cha kuchechemea kwa uchumi wa kimataifa na athari kuendelea kuonesha makucha sehemu mbali mbali za dunia, kuna haja ya kuwa na mwongozo makini kuhusu masuala ya kazi

Comece: ILo: Jubilei 100
27 November 2018, 15:23