Tafuta

Tafakari kuhusu: Mambo ya Nyakati na Ujio wa Pili wa Kristo Yesu! Tafakari kuhusu: Mambo ya Nyakati na Ujio wa Pili wa Kristo Yesu! 

Tafakari ya mambo ya mwisho wa nyakati na ujio wa pili wa Kristo Yesu! Msiwe na hofu!

Mkutano wa mwanadamu na Mwenyezi Mungu unalenga kutakasa, kujalia neema na kuleta amani. Tafakari hii ya mambo ya mwisho wa nyakati na ujio wa pili wa Kristo Kanisa linaileta kwetu kutufunulia siri ya ushindi hata baada ya maisha ya hapa duniani.

Na Padre William Bahitwa - Vatican.

UTANGULIZI: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu, leo dominika ya 33 ya mwaka B wa Kanisa. Dominika ya leo pia, pamoja na Kanisa zima tunaadhimisha “Siku ya Maskini” ambayo ilianza kuadhimishwa mwaka jana kama mwaliko wa kanisa zima kuonesha mshikamano wa kiinjili kwa masikini na wahitaji duniani. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa mwaka huu unabeba kauli mbiu “Maskini huyu aliita na Bwana akasikia” (Zab 34:7) ambapo hutualika kusikia, kuitika na kuokoa si tu maskini bali wahitaji mbalimbali katika mazingira tuliyomo.

Masomo kwa ufupi: Somo la kwanza (Dan 12:1-3) Unabii katika kitabu cha Danieli ni wa pekee kabisa katika kufikisha ujumbe wa Mungu kwa watu wake. Kitabu cha Danieli kimeandikwa katika kipindi ambacho wayahudi walikuwa chini ya udhalimu wa Antioko Epifani aliyewataka waache kuishika Torati na mapokeo ya wazee wao na waipokee miungu ya Uajemi. Ni kwa jumuiya hiyo inayoteseka mwandishi wa kitabu cha Danieli analeta masimulizi ya wengi walioteseka zamani kama wao lakini hawakuyaacha mapokeo yao na mwishoni walishinda. Mwandishi analeta pia mambo yajayo kama maono kuwa hata wao katika madhulumu waliyonayo, nyakati za mwisho wale watakaovumilia madhulumu ya sasa na watakaodumu kushika Torati watashinda. Katika ujumla huo wa kitabu cha Danieli, somo la leo linagusa mambo matatu.

Jambo la kwanza linamtaja Mikaeli jemedari mkuu. Huyu ni mjumbe wa Mungu atakayekuja kwa watu katika kipindi kigumu cha mateso yao ili kuwapa faraja na kuwaokoa watakaokuwa wameandikwa katika kitabu kile, yaani watakaokuwa wamedumu waaminifu kwa Torati. Jambo la pili katika somo hili ni ufufuko wa mwili. Somo hili ni kati ya sehemu chache sana katika Agano la Kale zinazozungumzia moja kwa moja ufufuko wa mwili; ushindi wa milele baada ya madhulumu ya sasa ya waaminifu wa Mungu. Jambo la tatu na la mwisho linalozungumziwa katika somo hili ni hukumu. Katika nyakati hizo za mwisho kutakuwapo pia na hukumu. Katika hukumu hiyo wengine watapatiwa uzima wa milele na wengine dharau ya milele.

Somo la pili (Ebr. 10:11-14,18) somo hili linalinganisha nguvu ya sadaka ya makuhani wa ukuhani wa Haruni na nguvu ya sadaka ya Kristo Kuhani Mkuu. Ni kulinganisha kati ya nguvu ya sadaka ya Agano la Kale na ile ya Agano Jipya. Tunaona kuwa sadaka ya Agano la Kale ambayo makuhani wa ukuhani wa Haruni waliitoa kila siku katika ibada haikuwa na uwezo wa kuondoa dhambi. Ni sadaka iliyokuwa ikiwatakasa watu ili waweze kusimama mbele ya Mungu, kumsikiliza na kushiriki katika ibada. Sadaka ya Kristo, sadaka ya Agano Jipya ambayo Kristo aliitoa mara moja tu inaenda zaidi ya hapo. Inaondoa dhambi. Sasa Kristo ameketi mkono wa kuume wa Mungu kuonesha kuwa sadaka yake moja aliiyoitoa imekamilika na inatosha. Anangoja hata adui zake wawekwe kuwa chini ya miguu yake kwa sababu kupokea matunda ya sadaka hii kunahitaji juhudi binafsi. 

Injili (Mk 13:24-32) Injili ya leo inazungumza juu ya mambo ya nyakati za mwisho, Ujio wa pili wa Mwana wa Adamu. Ujio huo, Yesu mwenyewe anaeleza, utaambatana na mabadiliko mbalimbali: jua kutiwa giza, mwezi kutotoa mwanga, nyota kuanguka na nguvu zilizo mbinguni kutikisika. Yesu anaalika kuwa makini kusoma alama ya nyakati na kuyachunguza mabadiliko ya asili. Mabadiliko haya hata hivyo ni kiashirio tu kwa sababu kuhusu siku na saa hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni wala Mwana ila Baba.

TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tunapoelekea mwisho wa mwaka wa kiliturujia wa Kanisa, Maandiko Matakatifu nayo yanaanza kutupa tafakari kuhusu mambo ya nyakati za mwisho. Mambo haya ya nyakati za mwisho mara nyingi huleta hofu ya namna fulani kwa watu kwa sababu daima huzungumzia mwanadamu kukutana na Mungu na mwanadamu kupata hukumu yake ya mwisho. Lakini tunapoangalia Maandiko Matakatifu katika ujumla wake, karibu mara zote mwanadamu anapokutana na Mungu, Mungu anamwambia “usiogope”.

Mkutano wa mwanadamu na Mungu ni mkutano unaolenga kutakasa, kujalia neema, kuleta amani. Tafakari hii ya mambo ya mwisho wa nyakati na ujio wa pili wa Kristo Kanisa linaileta kwetu kutufunulia siri ya ushindi hata baada ya maisha ya hapa duniani. Pamoja na hayo, tafakari ya mambo ya mwisho ni mwaliko mzito kwetu kudumu; kudumu katika kushika imani, kushika amri za Mungu na maagizo yake, kudumu katika kuvumilia bila kuichafua dhamiri dhidi ya madhulumu na magumu mbalimbali ya imani. Na hapa tunaona kuwa katika tafakari ya mambo ya mwisho wa nyakati hatuangalii zaidi mwisho mbaya wa maadui wa imani, maadui wa Kristo bali hasa ni sisi kuangalia namna tunavyoweza kuingia katika uzima wa milele.

Liturujia J33
17 November 2018, 07:21