Cerca

Vatican News
Upendo kwa Mungu na jirani ni utimilifu wa Torati na Unabii! Upendo kwa Mungu na jirani ni utimilifu wa Torati na Unabii!  (Vatican Media )

Rudini shuleni mkajifunze upendo kwa Mungu na jirani!

Kumbe, kumpenda Mungu na jirani ni kushika Torati na Manabii, ndiyo ufunuo wote katika Maandiko Matakatifu, ni kuoanisha uchaji kwa Mungu na maadili katika maisha na hii ndiyo amri iliyo ya kwanza.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Masomo kwa ufupi: Somo la kwanza (Kum. 6:2-6) somo hili ni sehemu ya hotuba ya Musa aliyoitoa kwa Waisraeli wakiwa wamekaribia kabisa kuingia katika nchi ya ahadi. Katika hotuba hii Musa anawakumbusha Waisraeli mambo yote ya msingi wanayopaswa kufanya; anawakumbusha Agano waliloliweka na Mungu, anawakumbusha amri za Mungu na sheria zake na anawaasa wasizisahau. Na leo anawasisitizia kuwa mafanikio yao wanapoingia katika nchi ya ahadi yatategemeana na namna watakavyozishika amri na sheria hizo za Bwana. Watakapomcha Bwana na kuzishika amri na sheria zake, siku zao zitaongezeka, wao wenyewe wataongezeka kama ilivyokuwa ahadi ya Mungu kwa Abrahamu na pia watafanikiwa. Kwa kutambua pia kuwa nchi wanayongia inakaliwa na watu wanaoabudu miungu wengi, Musa anawakumbusha kuwa wao, Mungu wao ni mmoja tu. Mahusiano waliyo nayo naye yanapaswa kuwa ni yale ya upendo; “mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa nguvu zako zote”

Katika somo hili Musa anaweka mbele ya waisraeli na mbele yetu sisi leo wajibu kwa Mungu na kiini cha kuuishi wajibu huo. Kwa Mungu mwanadamu anao wajibu wa kuzishika sheria na amri zake. Anao pia wajibu wa kumwabudu, wajibu wa kumcha, kumtolea sadaka, kumsifu, kumwomba, kumshukuru na kadhalika. Ni wajibu wa lazima alionao mwanadamu kwa Mungu. Lakini  kiini cha wajibu huu ni kumpenda Mungu. Yote anayofanya mwanadamu kwa Mungu kama wajibu wake usifanywe tu kama wajibu au kama mazoea au kwa hofu bali uwe ni tunda la upendo kwa Mungu.

Somo la pili (Ebr. 7: 23-28) Somo hili linaendeleza dhamira ya ukuhani wa Kristo: ukuhani mmoja na wa milele, ukuhani unaookoa milele na ukuhani ulio mkuu. Waraka huu unauelezea ukuhani wa Kristo ukiulinganisha daima na ule uliozoeleka, ukuhani wa Haruni. Na katika hali hiyo hiyo ya kulinganisha, waraka kwa Waebrania unaonesha kuwa makuhani wa ukuhani wa Haruni walikuwa ni wengi, yaani walirithi daima kutoka kizazi hadi kizazi kwa sababu walikuwa ni binadamu tu. Ukuhani wa Kristo ni mmoja, ni ule ule kwa sababu Kristo ni wa milele. Wale wanaoshiriki ukuhani wa Kristo hufanywa Kristo mwingine (Alter Christus) na kuuendeleza ukuhani ule ule mmoja wa Kristo. Pili ukuhani wa Kristo unao uwezo wa kuokoa milele kwa sababu ni ukuhani usio na hatia kwa sababu Kristo mwenyewe ni kuhani asiye na hatia, hana uovu wala dhambi. Ni mtakatifu. Na tatu ni ukuhani mkuu kwa sababu haukuwekwa na torati kama ulivyowekwa ukuhani wa Haruni bali wenyewe uliwekwa kwa kiapo: “Bwana ameapa wala hataghairi, ndiwe kuhani hata milele kwa mfano wa Melkizedeki” (rej. Zab 110:4).

Injili (Mk 12:28b-34) Katika Injii ya leo, Kristo anafupisha sheria na amri zote za Mungu katika upendo.  Mmoja wa waandishi anapomuuliza “katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza”? Yeye anajibu kumpenda Mungu na kumpenda jirani ndiyo amri iliyo ya kwanza. Kumpenda Mungu kwa moyo, kwa roho, kwa akili na nguvu. Na kumpenda jirani kama nafsi yako. Jibu hili la Yesu linatoa mwangwi wa mambo mawili: mwaliko wa Torati ya Musa kumpenda Mungu kwa moyo wote, kwa roho yote na kwa nguvu zote (Kumb. 6:4) na pia mwaliko usiokoma wa manabii kuunganisha uchaji kwa Mungu na matendo ya uadilifu na haki kwa jirani. Nabii Amosi kwa mfano ni kati ya manabii ambao wamewaonya daima waisraeli dhidi ya hali ya mtu kuwa mstari wa mbele katika ibada ilhali anayoyatenda kwa wenzake nje ya ibada yanapingana moja kwa moja na uchaji wote. Kumbe, kumpenda Mungu na jirani ni kushika Torati na Manabii, ndiyo ufunuo wote katika Maandiko Matakatifu, ni kuoanisha uchaji kwa Mungu  na maadili katika maisha na hii ndiyo amri iliyo ya kwanza.

TAFAKARI Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Maandiko Matakatifu katika dominika ya leo yanaturudisha katika shule ya upendo. Yanatualika kutambua kuwa maisha yetu na mahusiano tuliyonayo na Mungu na wenzetu yanaanza katika msingi wa upendo, yanazunguka katika mhimili wa upendo na yanapimwa katika mzani wa upendo. Na kwa namna ya pekee kabisa leo tunaalikwa kutambua kuwa Mungu hatuiti kutimiza amri zake tu, kufuata maagizo yake tu, tunavyoweza kusema kama roboti! Anatualika tumpende. Uhusiano wetu na Mwenyezi Mungu ni uhusiano wa upendo. Tunapoanzia na upendo, maagizo na amri zake tutazishika. Tunaalikwa pia kuyaangalia mahusiano tuliyonayo na wenzetu ili nayo pia yasitangulizwe tu na wajibu au kitu kingine bali upendo. Upendo huu unayo nguvu kubwa ajabu kiasi kwamba pale unapokuwapo mengine yote mema hufuata tena kwa urahisi ajabu. Na unapokosekana kinyume chake hutokea.

Mtakatifu Agostino aliwahi kusema “anza na upendo na kisha fanya chochote unachotaka”. Aliamini kuwa popote pale upendo unapotangulizwa chochote kile kitakachofuata kitakuwa ni chema. Haiwezekani upendo ukamsukuma mtu kumtendea uovu mwenzake. Upendo na uovu havikai pamoja. Naye Mtakatifu Teresia wa Avila katika upendo anafundisha kuwa “mwisho wa maisha yetu hatutahukumiwa kwa kadiri ya tulichofanya pali kwa kadiri ya upendo tuliouweka katika kile tulichofanya”. Mungu ambaye ndiye upendo wenyewe atujalie nasi kuwa na upendo maishani. Kumpenda Yeye kwa moyo wote, kwa roho yote, kwa akili yote na kwa nguvu zote na kumpenda jirani kama nafsi zetu.

Liturujia J31
03 November 2018, 14:29