Kipindi cha Majilio: Sehemu ya kwanza: Ujio wa Pili wa Kristo Yesu: Kuwahukumu wazima na wafu! Kipindi cha Majilio: Sehemu ya kwanza: Ujio wa Pili wa Kristo Yesu: Kuwahukumu wazima na wafu! 

MAJILIO: Jiandaeni kwa: Sala, makesha, toba na sadaka!

Tukiwa katika sehemu ya kwanza ya majilio, Maandiko Matakatifu katika dominika hii yanaelekeza tafakari yetu katika ujio huo wa pili wa Kristo, atakapokuja kudhihirisha kazi yake ya ukombozi, atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na kuuunda upya ulimwengu. Ni mafundisho ambayo hatuyasikii mara kwa mara na hata katika hizo mara chache tunapata daima picha ya kuogofya.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunaadhimisha dominika ya kwanza ya majilio na kwa dominika hii tunaanza mwaka mpya wa kanisa, mwaka C. Kipindi cha majilio, kama jina lenyewe majilio linavyoashiria “ujio” ni kipindi ambacho tunatazamia ujio wa Masiya; tunautazamia kwa matumaini ujio wake na tunatazamia utimilifu wa ahadi zake kwa ulimwengu na kwa viumbe vyake vyote.

Masomo kwa ufupi: Somo la kwanza (Yer. 33, 14-16) Nabii Yeremia anatoa utabiri wa mambo yajayo kwa taifa la Israeli. Ni utabiri wa kuundwa upya kwa Israeli baada ya kuharibiwa na baada ya wao kupelekwa utumwani Babiloni. Katika kipindi hicho ambayo taifa zima lilikuwa kama limekosa mwelekeo na halikuwa na matumaini. Nabii Yeremia anatoa unabii kuwa Mungu mwenyewe atatimiza ahadi yake na ataiunda upya Israeli. Kiini cha unabii huo ni kuwa Mungu atamchipushia Daudi chipukizi la haki, yaani atawainulia kiongozi mithili ya Daudi. Kiongozi ambaye kama Daudi, atawalinda kutoka maadui wa nje na atairejesha haki katika Israeli. Unabii huu unaisisitiza haki ili kuwakumbusha waisraeli kuwa yote waliyoyapata ni kama adhabu kwa sababu hawakuizingatia haki. Hawakumpa Mungu haki yake kwa maana waliipuzia torati na walilipuuza agano lake na pia jamii nzima haikuenenda kwa haki mbele ya wahitaji. Kumbe katika kuiunda upya Israeli wanawajibishwa kurudi katika haki na mji utakaa salama nao utaitwa kama “Bwana ni haki yetu”.

Somo la pili (1Thes. 3,12-4,2) Mtume Paulo anawaasa waamini wa Thesalonike wadumu katika njia njema hadi wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo pamoja na watakatifu wake wote. Paulo anawaandikia hivyo baada ya kupokea taarifa nzuri kuwa jumuiya ya wakristo aliyoianzisha Thesalonike inaendelea vizuri. Anawaandikia kuonesha furaha yake na matashi yake kwao kwamba upendo wao uzidi kukua na waendelee kuishi maisha yanayompendeza Bwana. Hadi lini? Hadi atakapokuja tena Bwana wetu Yesu Kristo.

Injili (Lk. 21, 25-28. 34-46) Injili ya leo inazungumzia juu ya ujio wa pili wa Mwana wa Adamu na hapohapo kuhimiza juu ya kukesha. Yesu anaonesha kuwa ujio wake wa pili utakuwa ni ujio utakaouunda upya ulimwengu, utakuwa ni ujio utakaobadili mpango wa sasa wa mambo na utaanzisha mpango mpya. Katika lugha ya pekee kabisa Yesu anasema jua, mwezi na nyota vitatiwa ishara, bahari nayo itakuwa na uvumi na misukosuko. Hivi vyote vilikuwa ni vitu vikubwa na visivyoweza kukaribiwa. Bahari kwa mfano ilikuwa ni alama ya hatari na ya maangamizi. Jua, mwezi na nyota viliabudiwa kama miungu na hakuna aliyefikiri kuwa itafika wakati navyo vitaguswa kwa namna yoyote ile. Kristo kwa lugha hiyo anaonesha kuwa ujio wake ni ujio ulio na nguvu kuliko nguvu zozote zilizopo ulimwenguni na kwa nguvu zake hizo ataufanya upya ulimwengu mzima.

Anasema “hapo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika wingu pamoja na nguvu na utukufu mwingi”. Kwa nini ujumbe huu? Kristo anawapa wanafunzi wake ujumbe huu kuwafanya wakumbuke daima kuwa kazi yake ya ukombozi kwa kumwaga damu msalabani, itadhihirika waziwazi pale atakapokuja tena mara ya pili. Na hivyo katika kipindi cha kungojea ujio wake waishi katika kukesha: wasijisahau, wasilemewe na malimwengu, wasilemewe na tamaa za kimwili na vionjo vyake na wala masumbufu ya maisha ya kila siku yasiwafanye wakakata tamaa wakajiona wako peke yao ulimwenguni humu hata siku hiyo ikawajia ghafla. Wakeshe wakijiweka tayari.

TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, kipindi hiki cha majilio tulichokianza kina sehemu mbili, zote zikituandaa kwa ujio wa masiya. Katika sehemu ya kwanza tunajikita kujiandaa kwa ujio wake wa pili na katika sehemu ya pili tunajiandaa kwa ujio wake wa kwanza, kuadhimisha ujio wake wa kwanza katika sikukuu ya Noeli.

Tukiwa katika sehemu ya kwanza ya majilio, Maandiko Matakatifu katika dominika hii yanaelekeza tafakari yetu katika ujio huo wa pili wa Kristo, atakapokuja kudhihirisha kazi yake ya ukombozi, atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na kuuunda upya ulimwengu. Ni mafundisho ambayo hatuyasikii mara kwa mar ana hata katika hizo mara chache tunapata daima picha ya kuogofya. Lakini ni mafundisho ambayo Kristo mwenyewe ameyasisitiza mara nyingi katika injiili kuwa atarudi tena na hili limekuwa ni moja ya mafundisho yanayochukua sehemu kubwa katika nyaraka za Mtume Paulo.

Kipindi hiki cha majilio kinachukua kama mojawapo ya dhamira zake kuu kutukumbusha kuwa Kristo atakuja tena. Na ulimwengu mzima nasi sote tupo katika kipindi hicho cha kusubiri. Atakuja lini? Hatujui. Ila wajibu wetu ni kujiandaa kwa ujio wake. Na katika maandalizi ya ujio wake majilio inatualika kujitwalia fadhila njema na kuzifanya kuwa sehemu ya maisha yetu. Fadhila zinazotajwa katika masomo ya leo ni kukesha, kudumu katika njia njema na kuwa watu wa matumaini. Tunaalikwa kukesha kwa sababu hatujui Kristo atakuja lini. Tunaalikwa kukesha bila kupoteza lengo ili ujio wake usiwe kwetu ujio wa ghafla. Tunaalikwa kudumu katika njia njema, kudumu katika mambo mema tuliyokiwisha yaanza, kama namna ifaayo ya kuungoja ujio wake.

Ujio wake Kristo hatuungoji tukiwa tumekaa tu, tunaungoja tukiwa katika utendaji. Wanafunzi wa Yesu walipoambiwa warudi Yerusalemu kungoja ujio wa Roho Mtakatufu hawakwenda tu kujifungia ndani na kukaa kumsubiri Roho Mtakatifu bali walimngoja wakisali usiku na mchana na hata Roho alipokuja walikuwa katika sala ya pamoja. Ndivyo unavyosubiriwa wakati wa Bwana na ndivyo zinavyosubiriwa ahadi zake Bwana katika maisha yetu. Mwisho tunaalikwa kuwa watu wa matumaini kwa sababu ni Kristo mwenyewe aliyetuhakikishia kuwa atakuja tena na ujio wake ni ujio unaokuja kutimiza ahadi zake za ukombozi wetu na wa ulimwengu mzima. Na tuianze vema majilio ya mwaka huu wa 2018 naye Kristo ayajaze matamanio yetu ya kuwa watu wake hasa na ya kuungana naye kwa furaha atakapokuja tena.

Liturujia: Majilio J1
30 November 2018, 16:45