Tafuta

Vatican News
Upendo kwa Mungu na jirani ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu! Upendo kwa Mungu na jirani ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu!  (ANSA)

Upendo kwa Mungu na jirani ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu!

Amri ya upendo kwa Mwenyezi Mungu na jirani ni muhtasari wa mafundisho makuu yaliyotolewa na Kristo Yesu kwa wafuasi wake, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema ni kuhakikisha kwamba, upendo huu unamwilishwa katika uhalisia wa maisha na kamwe usibaki unaelea katika ombwe!

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma, Tanzania.

Hizi ni baadhi ya sheria zilizokuwepo au bado zipo katika baadhi ya miji huko Marekani: Katika mji wa Pittsburgh, Pennsylvania – ni kinyume cha sheria kulala ndani ya jokofu. Katika mji wa Gary, Indiana – utavunja sheria ukienda sinema ndani ya saa nne baada ya kula kitunguu saumu. Katika mji wa Pocatello, Idaho – ni marufuku kuonekana huna furaha. Katika mji wa Dunn, North Carolina – ukikoroma kiasi cha kusumbua majirani una hatari ya kulala selo siku moja au mbili. Kabila moja la Chippewa – Wahindi Wekundu – nao wana amri kumi na ya kwanza kabisa inasema usiibe isipokuwa kwa adui yako.

Turudi kwenye masomo yetu ya leo. Yule Farisayo anauliza ni ipi amri iliyo kuu. Yesu anajibu ni upendo. Vingine vyote ni muhimu lakini si kama upendo kwa Mungu na jirani.  Sheria za kiyahudi zilikuwa nyingi na watu walitaka toka kwa viongozi wao, muhstasari wa sheria hizo. Ni amri ipi ni kubwa zaidi? Ilionekana kuwa kama zote zingeshikwa, basi kwa ajili ya wokovu, kumbukumbu kubwa ilihitajika.

Rabbi Hillel aliombwa atoe kwa kifupi mno akisimamia mguu mmoja sheria za Kiyahudi na akasema usichokipenda wewe, usimfanyie mwenzako. Kwa hiyo twaona hapa, si tu amri iliyo kuu bali pia inayobeba amri zote. Yesu anataja amri kuu yenye mambo mawili makuu; upendo kwa Mungu kama ya kwanza na ya pili upendo kwa jirani. Kadiri ya fundisho la Yesu amri hii ya upendo ni kamilifu. Kinyume chake ni pungufu. Wengine husisitiza upendo kwa jirani umwonaye kwanza – LIBERATION THEOLOGY na wengine kumpenda Mungu yatosha.

Leo hii Yesu atuambia tofauti kabisa, kwanza Mungu na pili jirani. Upendo kwa Mungu kwa moyo wako, roho, akili na nguvu na ananza akisema – Bwana Mungu wetu ni Mungu pekee. Mungu mkuu na anayeokoa. Mungu ametupenda sisi kwanza, hivyo nasi tunadaiwa upendo kwa sababu tunaweza kupenda.  Kitambulisho cha Ukristo wenu ni mapendano kati yenu – Yoh. 13:34-35 – amri mpya nawapeni; mpendane. Kama mimi nilivyopenda, nanyi pia mpendane. Hivyo watu wote watawatambua kuwa ni wafuasi wangu, mkipendana.  

Kwa maana hii lile swali kwa Yesu ni amri ipi, nia yake haikuwa tu juu ya amri 10 kwamba mimi ndimi Bwana Mungu wako, usiabudu miungu wengine – Kut. 20:2-3, n.k., bali alitaka kusikia Yesu anasema nini. Katika Injili hii ya Marko tunaambiwa kuwa lengo la yule farisayo halikuwa tu kumjaribu Yesu, bali kujifunza. Pengine sheria zilikuwa nyingi katika jamii yake na kuwachanganya watu. Jibu lake kwa Yesu baada ya fundisho, umesema sawa, Mungu ni mmoja na hakuna mwingine ila kumpenda kwa moyo, roho na akili na nguvu na kumpenda jirani ni zaidi ya sadaka za kuteketezwa laonesha kuwa alielewa vizuri kabisa.

Katika Mk. 12:32-33 – tunaona mvutano mkubwa kati ya sheria na utekelezaji wake. Kwa mwanadamu yaonekana ngumu ila kwa Mungu inawezekana. Upo mvutano kati ya kupenda na kutimiza matakwa ya hekalu. Jibu la Yesu linabaki vile vile, kumpenda Mungu kwanza na jirani halafu matoleo yetu   na ibada   zetu. Yesu yu kinyume cha Mafarisayo kwa sababu waligeuza sheria. Anatumia mfano wa uelewa wa sheria zao kama ilivyo katika Torati na kuwapa majibu. Kwa mfano katika Mk. 7;11-12 – bali ninyi husema – mtu akimwambia babaye au mamaye, ni Korbani, yaani wakfu, kitu changu chochote kikupasacho kufaidiwa nacho, huwa basi. Wala hamruhusu baada ya hapo kumtendea neno babaye au mamamye.

Kwa desturi yao mtu akitamka neno hili juu ya mali ina maana kuwa imewekwa wakfu kwa ajili ya hekalu. Hivyo wazazi hata kama wana mahitaji basi hawawezi kufaidika na mali hii tena. Sasa mali inatolewa hekaluni wakati wazazi wana mahitaji ina maana gani? Yesu anawakumbusha na kuwakemea. Wameishia tu kutimiza sheria bila kujali hata faida yake. Pia katika Mt. 23:23 – anasema - ole wenu waandishi na mafarisayo wanafiki, kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mwakurupusha mambo muhimu ya sheria, ambayo ni haki na huruma na uaminifu. Hayo yawapasa kufanya bila kukurupusha mengine. Kwamba wanazingatia kufanya mambo madogo madogo na ya kawaida katika sheria lakini yale ya muhimu na makubwa kama matendo ya huruma na uaminifu wanakurupusha.

Wapo wakristo wengi hata siku hizi ambao huona ibada kama kuabudu sheria na amri tu. Kutimiza wajibu tu kama vile nahudhuria jumuiya, natoa zaka, michango n.k. kwenda kanisani jumapili tu. Kuhudhuria kwaresima au juma kuu tu. Fundisho la Yesu leo lasema  yote tufanyayo yasisukumwe tu na sheria lakini itoke katika pendo kwa Mungu na jirani. Utii siyo wajibu wa kwanza wa mkristo bali upendo. Hatuna budi pia kutafakari leo jinsi tunavyozitimiza sheria mbalimbali ambazo tunazifahamu. Zipo sheria za Mungu, za kanisa, za kijamii, za nchi n.k. Zipo pia sheria nyingi na mbalimbali ambazo tumejiwekea kadiri ya mazingira yetu n.k. Je ni kwa kiasi gani tunazitumia ili zitufae kwa ajili ya maisha na wokovu wa mwili na roho?  Yesu anasema wazi bila upendo, sheria zetu hazitakuwa na faida na maana yo yote kwa maisha yetu ya mwili na roho. Nabii Mika 6:8 anasema – Ee mwanadamu, yeye amekuonesha yaliyo mema, na Bwana anataka nini kwako, ila kutenda haki na kupenda Rehema na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako. Tumsifu Yesu Kristo.

02 November 2018, 08:23