MAJILIO NI KIPINDI CHA KUMBU KUMBU NA MATUMAINI. MAJILIO NI KIPINDI CHA KUMBU KUMBU NA MATUMAINI. 

MAJILIO: Ni kipindi cha kumbu kumbu na matumaini!

Ni kipindi cha kumbukumbu na matumaini. Tunamkumbuka Yesu Kristo aliyejifanya mtu - tunatafakari uwepo wake na maisha yake hapa duniani kama Mungu na mwanadamu akaupa umaana uwepo wetu sisi – hadhi ya kimungu akatuonesha maana ya maisha ya Kimungu. Tumshukuru Mungu. Tunatumaini ujio mtakatifu, jumuiya takatifu na utu uliofungamanishwa na upendo wa Mungu.

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma, Tanzania.

Ndugu wapendwa, leo tunaanza jumapili ya kwanza ya majilio. Katika somo la kwanza, Nabii Yeremia anaongea juu ya kile kitakachotokea – mwisho wa nyakati. Injili ya leo yaongea juu ya ujio mpya wa Kristo, katika utukufu, lakini yaongea juu ya uwepo wa Yesu kati yetu. Wokovu upo, matumaini yapo. Majilio ni juu ya Mungu aliyepo, siyo anayekuja.  Tunakumbushwa kuwa utakatifu hupatikana katika kuwa na kuishi kama wana wa Mungu. Yeye ndiye mtakatifu nasi tunaitwa kuwa watakatifu. Wimbo mpya ni maisha mapya katika Kristo. Uwepo wa Roho Mtakatifu – hutuwezesha kufikia uhuru kamili toka dhambi. Katika 1Thes. 1: 7-8–Mt. Paulo – anawasifia Wathesalonike kwa mfano wao wa imani kwa Mungu na anawaombea kuwa mioyo yao ibaki safi, bila waa na mitakatifu mpaka atakapokuja Bwana na watakatifu wake.

Injili ya leo – yaongelea juu ya ujio mpya wa Kristo, katika utukufu, lakini yaongea juu ya uwepo wa Yesu Kristo kati yetu. Wokovu upo, matumaini yapo. Majilio ni juu ya Mungu aliyepo, siyo anayekuja. Ujio wa pili wa Kristo – wamaanisha ujio wake katika utukufu, mwisho wa nyakati – PAROUSIA.  Huko Thesalonike – Mt. Paulo alirudi mara ya pili kufundisha ili kuondoa mkanganyiko uliojitokeza kuhusu ujio huu wa pili wa Kristo. Shida kubwa toka kwa hao wakristo ilikuwa hii: je hao wakristo wenzao waliokwisha kufariki dunia itakuwaje? Je watarithi pia huu utukufu siku hiyo ya kuja Bwana? Mt. Paulo – anawaondolea hofu hiyo – kwamba kuwa hai au mfu – siyo jambo muhimu. Msisitizo na fundisho ni kwamba – tumaini la Kikristo ni kuwa wote watakuwa na Bwana.

Shida ya pili ya Wathesalonike ilikuwa ni kuwa ujio ungekuja mara moja na hivyo ikatokea hatari ya kukaa hata bila kufanya cho chote, wakakaa tu wakisubiria – inaonekana hivyo pengine katika 1Thes. 1:4;17 – ingawa Mt. Paulo alijua wazi kuwa muda si swala la msingi katika imani. Hata Yesu mwenyewe alisema wazi – hajui siku wala saa – Mk. 13;32. Hivyo ilibidi Mt. Paulo awatulize.

Hata hivyo huku kungojea ujio wa Kristo mara ya pili ikumbukwe si kuja kutusamehe dhambi bali ni ujio wa hukumu na hii inaongeza shauku kubwa ya maisha na imani ya mkristo. Imani yetu katika umwilisho wa Kristo inabaki na tukiamini kuwa atakuja siku ya mwisho. Kama tulifurahia ujio wake wa kwanza, basi hatuna budi kujiandaa ili kushiriki ujio wake wa pili ila tusibaki kama Wathesalonike wakitumaini kushiriki ujio huo mara katika mwili. Sisi tunashiriki katika tumaini la ujio huo. Tukiwa na tumaini hilo basi tuishi mwaliko wetu wa leo toka kwake Yesu na tukizingatia fundisho hilo la Mtume Paulo, yaani kujiandaa, kuwa tayari. Kwa vyo vyote vile sisi tunaoshiriki imani – tukiwa hai au wafu – tunatumaini kukutana na Bwana siku moja. Tuombe kuwa muungano huu uwe wa furaha.

Dante Gabriel Rossetti, Mtaliani mwanamashairi na mchoraji maarufu wa karne ya 19; alifikiwa na mtu mmoja mzee na mchovu akibeba lundo la michoro akitaka toka kwake aseme cho chote au kumtia moyo kwa alichofanya. Rossetti akatazama kwa umakini mkubwa. Akagundua kuwa hazikuwa na alama yo yote ile ya kiufundi. Hakuwa na budi kumweleza ukweli ulivyo kwa utaratibu mkubwa. Yule mzee akakubali matokeo lakini bado akionesha haja ya kupata alama yo yote kwa ile kwa kazi yake, akamwomba msamaha kwa kuchukua muda wake, lakini akamwomba kutazama tena fungu jingine la picha alizokuwa nazo mkononi. Alipozitazama tu Rosetti akamwuliza yule mzee – hizi kachora nani?

Ni mwanafunzi mchoraji? Dante akakubali ufundi uliokuwepo katika fungu hili jingine la picha. Akamwambia kuwa huyu mwanafunzi kijana ana kipaji kikubwa. Huyu inabidi apewe msaada wa pekee ili aendelee mbele. Huyu ana mwelekeo mzuri. Yule mzee akafunguka kwa furaha na uso wake ukang’ara kwa furaha. Rosseti akamwuliza – huyu ni nani na yuko wapi? Ni mtoto wako? Yule mzee akasema – ndimi mchoraji wa michoro hii miaka 40 iliyopita. Lakini kama ningesikia sauti kama hii yenye kutia moyo kama hii toka kwa mtu kama wewe miaka hiyo, leo hii ningekuwa mbali sana.

Hakika tunahitaji mtu au muda au kipindi kinachotupatia tena muda wa kutafakari uhalisia wa ukristo wetu na majukumu yetu hai ya kikristo. Kipindi cha majilio kinachukua jukumu hilo. Majilio ni kipindi cha majuma manne (4) na kipindi hiki huhitimishwa na sikukuu ya Noeli. Katika kipindi hiki: Tunasikia tena sauti za manabii wanaotangaza ujio wa Bwana. Tunasikia tena majilio na matumaini ya watakatifu wa Bwana wa Agano la Kale na imani ya watu walioshiriki tukio hilo moja kwa moja kama Mama Bikira Maria, Mt. Yosefu na Mt. Yohani Mbatizaji n.k. Tunatafakari upendo wa Mungu aliyempeleka mwanae ulimwenguni kwa ajili ya masamaha ya dhambi, kutufanya  wanae kwa kutoa maisha yake na kutupatia neema. Yesu aliyezaliwa Bethlehemu anazaliwa pia kwetu katika mioyo yetu katika familia zetu, katika Jumuiya yetu, katika mtaa wetu na katika Parokia yetu n.k.

Kipindi hiki: Kinatufanya tuwe makini, kukesha. Yesu anagonga, anabisha hodi. Anatualika kwenye karamu tunangoja tukikesha. Yesu pia ni hakimu na hivyo majilio yatukumbusha hali hiyo, uwepo wetu kama mahujaji - tuko safarini tusibanwe na mambo ya dunia. Je tunatambua na kuishi uwepo wa Mungu kati yetu? Liturujia inatuangalisha hivyo: Inahuisha matumaini yetu. Inaimarisha imani yetu. Inakomaza mapendo yetu. Ili ajapo Bwana - atukute tu macho, tukiwa na taa zetu mikono na zikiwaka na kuwa na mioyo iliyo tayari kumpokea mfalme wa Mbingu na dunia.

Ni kipindi cha kumbukumbu na matumaini. Tunakumbuka nini? Tunamkumbuka Yesu Kristo aliyejifanya mtu - tunatafakari uwepo wake na maisha yake hapa duniani kama Mungu na mwanadamu akaupa umaana uwepo wetu sisi – hadhi ya kimungu akatuonesha maana ya maisha ya Kimungu - eti Mungu akawa mwanadamu. Tumshukuru Mungu. Tunatumaini nini? Tunatumaini ujio mtakatifu aliotuahidia, jumuiya takatifu na utu uliofungamanishwa na upendo wa Mungu. Angalia Pope Benedict XVI (Joseph Card Ratzinger) “Seek that what is above” 1986... Memory Awakanes Hope. Kumbukumbu zinaamsha matumaini. Tunakumbuka kuwa Mungu amekuja kwetu, akakaa nasi na tunahusisha matumaini yetu kwamba Kristo atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu wazima na wafu. Katika kipindi cha majilio tunakumbuka matendo makuu ya Mungu na tunatumainia upendo mkuu wa Mungu.

Mtakatifu Ireneo katika maandishi yake karne ya 3 “DHIDI YA UZUSHI” “AGAINST HERESIES” anaandika hivi: akielezea kazi ya Kristo akisema, imani ya Kikristo, inatambua kuwa Mungu ni mmoja na Yesu Kristo mwanae, Bwana wetu, ambaye vitu vyote viko chini yake. Kati ya vitu hivyo yupo mwanadamu, ambaye ni sura na mfano wake Mungu. Hivyo naye mwanadamu ni mali yake naye Mungu asiyeonekana, akaonekana kwetu, tukamfahamu, 3,16,6 Gia’ e Ancora’ (Already and not Yet) CCCXX, 1979, p. 268.

TUMSIFU YESU KRISTO!

28 November 2018, 17:04