Tafakari: Jifunzeni kutoa kwa ukarimu! Tafakari: Jifunzeni kutoa kwa ukarimu! 

Jifunzeni kutoa kwa moyo wa ukarimu na upendo!

Toa kwa moyo wa ukarimu na shukrani, toa katika hali ya ukamilifu hata kama machoni pa watu kinaonekana kuwa kidogo namna gani. Namna hii ya kujitoa inadhihirisha imani thabiti katika Mungu mpaji na kujitegemeza katika fadhila zake.

Na Padre Joseph Peter Mosha, - Vatican.

Katika jamii mamboleo falsafa inayotawala sana ni ile ya “pragmatism”, falsafa ambayo inajikita katika maslahi. Kila mmoja anafanya kitu fulani iwe ni huduma makazini au kwenye jamii au kujitoa kwa tendo fulani la ukarimu akiongozwa na tarajio la kupata faida binafsi. Hii ni sawa na msemo wa katika lugha ya kiswahili usemao: “mkono mtupu haulambwi”. Namna hii ya mwelekeo wa kijamii inaathiri kwa kiasi kikubwa imani yetu sahihi kwa Mungu wetu kama mpaji wa yote, umoja wetu wa kindugu katika jamii na utayari wa kufanya matendo ya huruma kwa wenzetu. Matokeo yake ni uchoyo, ubinafsi na pengine kuona kujitoa kwetu kunaweza kutupunguzia vile tulivyonavyo. Leo tunaalikwa kujikabidhi mikononi mwa Mungu katika imani kuu na kujitoa kwake kikamilifu tukiamini katika ufadhili wake mkuu kwetu na wenye kudumu.

Katika mazingira yoyote yale Mungu ni mfadhili mkubwa kwa wale wanaomtumainia; hivyo tusibanwe na ubinafsi wetu na kuogopa kujitoa kwa ajili ya wenzetu. Mfano mzuri ni mjane wa somo la kwanza aliyekuwa na imani kubwa katika ufadhili wa Mungu hata kuwa tayari kushirikisha kidogo alichokuwa nacho kwa ajili ya mgeni aliyemfikia bila kujali kuwa hatakuwa na kitu cha kula. “Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi”. Mwanadamu anapenda sana kupokea kuliko kutoa. Sala ya Mtakatifu Francisko wa Assis inatuambia kuwa “katika kutoa ndipo tunapokea”. Tujiulize: kama kila mmoja akiwa mchoyo, asiwe tayari kutoa bali kutaka kupokea tu, mwisho wa siku tutapokea nini? Tutambue kuwa mkono unaonyooshwa ili kutoa ndiyo huo huo utakaopokea mema ya Mungu.

Mama huyu mjane hata kama angemnyima mgeni wake bado kiasi kile kingekwisha hivyo akabaki na njaa na pia akakosa kuonesha upendo kwa mwingine. Angekosa chakula na pia kuipoteza nafasi ya kuuhudumia ubinadamu uliohitaji huruma yake. Mara nyingi ubinafsi wetu hutuingiza katika uchoyo; kutokuwa tayari kujitoa nafsi zetu kwa ajili ya wengine, kutokuwa tayari kuona wengine wanapata au kuneemeka zaidi ya wewe. Matokeo yake tunajikuta tunajijengea ukuta na kuishia kufa ndani ya kuta hizo za ubinafsi. Fundisho tunalolipata hapa ni kuona kuwa kinachotakiwa kutolewa kwa jirani yako mwenye uhitaji si kile kinachoshikika kama chakula au mali. Viti hivyo vina ukomo wake. Lakini kama tuwapatia wenzetu upendo, faraja, na mshikamano tutauhudumia ubinadamu na majitoleo yetu hayo yatabaki milele.

“Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe na Eliya na nyumba yake yote, wakala siku nyingi. Lile pipa halikupungua, wala ile chupa ya mafuta haikuisha”. Baraka anayoipata mama mjane pamoja na nyumba yake yote ni ufunuo kwetu kuwa pale mwanadamu atakapokuwa tayari kushirikiana na mwingine, kila mmoja kwa kadiri alivyojaliwa basi wote tutategemezana na kuimarishana na hivyo itakuwa ufanisi kwa jamii yote. Mshikamano wa kijamii na kila mmoja kutenda kwa ufanisi nafasi yake ni mlango wa mafanikio kwa jamii nzima. Kila mmoja wetu anapata wito wa kuitambua nafasi yake na kuitenda vema katika ukamilifu, kuanzia katika ngazi ya familia zetu hadi katika jamii nzima kwa ujumla. Tuepuke vishawishi ama vya kuona tunao uwezo kidogo au kufumba macho na kujitenga na wengine. Tukumbuke kwamba “kidole kimoja hakivunji chawa” na pia “haba na haba hujaza kibaba”.

Leo hii tunaalikwa kutokuona kuwa Mungu anatudai kutoa sana; tunalikwa kutoona uchoyo au ugumu kushirikisha wengine kwa kuangalia kiwango au kiasi ulichonacho. Toa kwa moyo wa ukarimu na shukrani, toa katika hali ya ukamilifu hata kama machoni pa watu kinaonekana kuwa kidogo namna gani. Namna hii ya kujitoa inadhihirisha imani thabiti katika Mungu mpaji na kujitegemeza katika fadhila zake. Mama mjane katika Injili anatuonesha namna hiyo ya kujitoa: kwanza ni kujitoa bila kujibakiza, yaani kujitoa mzima mzima. Pili ni kutoa si sehemu iliyobaki bali kuitoa ile sehemu muhimu kabisa. Maisha yake yote yanapimwa kwa thamani ya senti mbili lakini “katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia”.

Neno la Kristo katika Injili linatufunulia ukweli kwamba Mungu wetu anaangalia zaidi roho ya mtu na madhumuni ya kujitoa na si katika kile kinachoonekana. Tunaonywa kuepa kufanya matendo ya huruma au ya kiibada huku tukichagizwa na kutafuta kuonekana tu. Tabia hiyo ni unafki wa kiroho. Ni nafasi ya kujiuliza ni nini madhumuni ya kujitoa kwetu katika huduma mbalimbali ndani ya jamii? Kama haitaongozwa na kutafuta kumuinua mwanadamu mwenzangu na hivyo kutoa sifa na utukufu kwa Mungu majitoleo hayo huwa yanakosa tija hata kama ni kwa kiwango kikubwa namna gani. Inatosha hata kufanya tendo moja dogo na jema lakini likiwa linatendwa na moyo mwema na ulio tayari kujitoa. Mama mjane si kwamba alitoa ili aendelee kustawi bali alitoa kile ambacho kilikuwa tegemeo lake ili apate kuishi. Kwa maneno mengine aliutoa uhai wake wote sawa na yule mama mjane katika somo la kwanza.

Leo hii tunaona watu wengi wanajitoa katika matendo mbalimbali ya huruma. Kwa namna moja tunafurahia huduma zao ambazo zinahudumia ubinadamu unaosukumwa pembezoni kwa sababu ya uovu wa mwanadamu. Lakini katika namna inayopingana na kujitoa kikamilifu na kuitoa sehemu iliyo bora zaidi wengi wa watu hawa huongozwa na sababu za ubinafsi wao. Mmoja anatafuta kujijenga na kuwa maarufu kiuchumi au kisiasa au kijamii. Hivyo kutoa kwake si kwa ajili ya kuhudumia ubinadamu huo unaoteseka mbele yake bali kwa ajili ya kuhudumia nafsi yake. Watu hawa hawana tofauti na hawa wanaojitoa kwa kuweka vile vya ziada walivyokuwa navyo. Wanatoa kile ambacho akifanyi sehemu muhimu ya nafsi zao bali kile ambacho kitaendelea kuwaneemesha na kuzijenga nafsi zao au kutanua matamvua yao.

Upendo wa Mungu na ufadhili wake kwetu umejifunua katika nafsi ya mwanae Bwana wetu Yesu Kristo. Sadaka yake moja ya Pasaka ni ujumuisho wa ufadhili huo wa Mungu kwetu. Yeye amejitoa kwa ajili yetu mara moja tu. Sadaka hiyo inaendelea kufanywa hai na ya kudumu kwa njia ya Sadaka ya Misa Takatifu, Ukumbusho wa mateso, kifo na ufufuko wake. Sisi nasi tunapata fursa ya kuishiriki sadaka hiyo katika Ekaristi Takatifu, ambamo ndani mwake tunampokea Kristo mzima katika maumbo ya mkate na divai na hivyo kuunganika naye na kuufanya hai uwepo wake kuwa wa kudumu. Tuungane naye kila siku katika Ekaristi Takatifu kusudi kwa njia yake tuendelee kuuonja na kuufanya hai ufadhili wa Mungu na hivyo tujitoe na kuwahudumia ndugu zetu wote katika nafasi yoyote na mahali popote kwa moyo upendo na ukarimu wa kweli na hivyo katika umoja huo tuendelee kutajirishana na kuufurahia ufadhili wa Mungu wakati wote.

J32 Mwaka B

 

07 November 2018, 14:18