Tafuta

Maaskofu wanasali kwa ajili ya waathirika wa moto huko California nchini  Marekani Maaskofu wanasali kwa ajili ya waathirika wa moto huko California nchini Marekani 

Moto California:maaskofu wanawaombea waathirika wa moto mkali!

Ni vifo na uharibifu mkubwa kutokana na moto wa misitu unaoendelea kukumba jimbo la California nchini Marekani. Katika Mkutano Mkuu wa Baraza la Maaskofu Marekani wamewakumbuka kwa sala waathirika wa moto huo wa kihistoria

Sr. Angela Rwezaula- Vatican

Wakati wa sala ya Malaika wa Bwana Jumapili iliyopita, maaskofu wa Marekani wameisali sala wakikumbuka waathirika wa moto, watu wote wanaojikita katika uokoaji na vikosi vya zima moto, kufuatia na vifo na uharibifu mkubwa wa misitu na mali za watu huko California nchini Marekani. Askofu Jamie Soto wa Sakramenti wakati akizungumza juu ya ajali hiyo ya moto mkali, amekumbusha kuwa janga hili halielezeki katika Jimbo lake, mahali ambapo mamia ya watu wamepotea. Katika eneo la Down Paradise ni kuona watu wanakimbia huku na kule kwa maana siyo rahisi kuwahesabu hata wale ambao wamepetea na wanashukiwa  wamekufa.

Kadhalika amesema kuwa nyumba  zaidi ya 6,713 zimeshaharibika  hata viwanda pia. Askofu ameongeza kusema kuwa, katika Parokia ya Mtakatifu Thomas Moro wanaparokia wote wamekimbia na wengine wamepoteza makazi yao. “Tumesitisha misa na shughuli zote za kichungaji na hiyo ni kutokana na  hali mbaya sana".  Aidha ameongeza kusema:"Parokia na shule zimeokoka kwa namna ya kiajabu. Wakati huo huo wazima moto bado wanaendelea kwa ujasiri kupambana na hali hii mbaya ya kihistoria". Askofu Soto amethibitisha.

Bwana Antonio Guterres amesikitishwa sana kufuatia taarifa za vifo na uharibifu mkubwa

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres ameelezea kusikitishwa kwake kufuatia taarifa za vifo na uharibifu mkubwa kutokana na moto wa misitu unaoendelea kukumba jimbo la California nchini Marekani. Ripoti zinanukuu vyombo vya habari vikisema kuwa hadi sasa idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na moto huo imefikia 31, huku wengine zaidi ya 200 hawajulikani waliko kutokana na moto huo utokonao na joto kali na kusambazwa kwa upepo. Kupitia taarifa ya Naibu msemaji wake, Bwana Guteress ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya wahanga na kwa serikali na watu wa Marekani. Bwana Guterres ameelezea mshikamano wake na serikali ya Marekani wakati huu ambapo ripoti za vyombo vya habari zinasema moto huo umesababisha watu wapatao 250,000 kukimbia makazi yao na kuwaacha watu wengi bila makazi.

Taarifa inasema kuwa idadi ya waliofariki kutokana na moto wa misituni katika maeneo mawili ya jimbo la California, magharibi ya Marekani imeongezeka na hivyo kufikia kiwango cha historia cha vifo kutokana na moto katika jimbo hilo. Karibu watu robo milioni walilazimika kukimbia makazi yao na gavana wa jimbo akisema sababu moja ya moto huo mkali ni mabadiliko ya hali ya hewa.

Moto wa kihistoria

Moto uliosababisha maafa makubwa zaidi katika historia ya jimbo hilo la California ulianza kaskazini ya jimbo hilo na kuteketeza kabisa mji wa Paradise ambako watu wengi walipoteza maisha na wazimamoto wameripoti kuwa wamegundua maiti nyingine siku ya Jumatatu 12 Novemba. Moto huo mkali uliopewa jina la Camp Fires unateketeza misitu ya sehemu za chini ya milima ya Sierra Nevada ambako karibu watu laki mbili na nusu wamekimbia makazi yao na zaidi ya nyumba na majengo 6400 kuteketezwa kabisa . Gavana wa jimbo la California Jerry Brown anasema wako katika zama zisizo za kawaida za hali ya hewa.  “Hatujui sababu za moto huo. Mji wa Paradaise ulijitayarisha vya kutosha kukabiliana na hali mbaya ya hewa kutokana na ukame na kukauka kwa mimeya lakini upepo mkali umesababisha hali hii mbaya kutokea na inatubidi kufahamu mabadiliko haya kwani tunaishi katika mazingira yasiyo ya kawaida.

Gavana Brown amemuomba Rais Donald Trump kutangaza kuwa moto huu ni janga kuu ili kuongeza msaada wa dharura na kuwasaidia wakazi kupata fidia.Hata hivyo  taarifa nyingine zinasema kuwa Rais Trump wiki iliyopita alikosoa usimamizi mbaya wa misitu ya California kuwa ni sababu ya moto ya mara kwa mara, lakini maafisa wa jimbo wanasema moto unatokea zaidi katika misitu inayosimamiwa na serikali kuu.

Wakazi wapoteza kila kitu

Wakazi walioweza kurudi katika mji wa paradise kutazama hasara waliopata wanalia kwa masikitiko kupoteza kila kitu. Mmoja wa wakazi hao amesema: "Tulilazimika kukimbia jana usiku hadi mji wa Topanga ili kutafuta maeneo ya usalama na nimerudi kutokana na habari kwamba kuna nyumba moja ilinusurika. Na hivyo niko hapa kutizama jinsi majirani zetu walivyoppoteza mali yao". Maafisa wa vikosi vya kuokoa na na wazima moto wanasema hawana hakika lini wataweza kudhibiti moto huo kwa hivi sasa.

14 November 2018, 11:01