Tafuta

Madhabahu mpya ya Bikira Maria Afya ya wagonjwa huko Buhabhugali- Kigoma, Tanzania Madhabahu mpya ya Bikira Maria Afya ya wagonjwa huko Buhabhugali- Kigoma, Tanzania 

Kigoma,Tanzania:madhabahu ya Bikira Maria afya ya wagonjwa!

Historia fupi ya madhabahu ya Mama Bikira Maria, Afya ya Wagonjwa, Buhabhugali na Kituo cha Ushauri cha Mtakatifu Teresa wa Calcuta, wakati wa ufunguzi wake tarehe 27 Oktoba 2018 iliyoandaliwa na Askofu wa Jimbo la Kigoma Tanzania

+Joseph R. Mlola, ALCP/OSS. Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma.

Tarehe 27 Oktoba 2018 yamefunguliwa Madhabahu na Kituo cha Ushauri cha Mtakatifu Teresa wa Calcuta huko Buhabhugali Kigoma Tanzania. Misa iliongozwa na Askofu Mkuu Paulo Ruzoka wa Tabora, ambaye pia alitabaruku Kanisa la kituo hicho cha Hija. Kabla ya kuanza Misa Takatifu ya Kutabaruku Kanisa, kwanza ilisomwa historia ya kituo hicho, kama ilivyoandaliwa na Askofu wa Jimbo la Kigoma, Mhashamu Askofu Mlola na historia hiyo ilisomwa na Padre Christopher Ndizeye.

Historia ya kituo cha hija

Katika historia ya kituo hicho Askofu Joseph R. Mlola, ALCP/OSS wa Jimbo la Kigoma kwa kutumia Barua ya Kichungaji ya Askofu Mkuu Paul R. Ruzoka ya tarehe 5 Januari 2001 kwa wakristo wa kigoma iliyokuwa na jina “Kristo Tumaini letu”, ili kuweza kuelezea vema juu ya mahali pale pa tukio ambapo alikuwa amesema kwamba,“ hapa Buhabhugali ni mahali pazuri penye kuvutia”. Askofu Mlola anathibitisha kuwa: Maneno haya ni ya kweli kwa sababu Mwenyezi Mungu alipaumba na akapapamba namna hii ya kupendeza machoni petu. Hakuna mikono ya mwanadamu iliyotumika kukiumba kilima hiki cha Kitwe. Hakuna mikono au akili za binadamu zilizotumika kuliumba ziwa Tanganyika. Hayo yote yanatuthibitishia kuwa Mwenyezi Mungu alipapamba mahali hapa na sasa panavutia na kupendeza machoni petu.

Sababu ya pili ya Buhabhugali kuwa mahali pazuri penye kuvutia

Maneno ya Mhashamu Askofu Mkuu Paul R. Ruzoka yanaendelea kuonesha kweli kwa sababu nyingine ya pili, kwamba, wana Kanisa la Buha wamepafanya papendeze na paonekane kama palivyo. Buhabhugali haikuwa na sura kabla ya mwaka 2000. Kama kuna watu waliokuwa wanakuja kutembelea mahali pale, hawakuwa wanakuja kwa malengo kama yaliyowaleta siku ile. Baada ya kutimiza matakwa ya kuweka eneo hili kuwa chini ya umiliki wa Jimbo Katoliki Kigoma, mwaka 2000 ofisi ya utawala wa Jimbo Katoliki Kigoma ilijenga msalaba eneo hilo. Ikumbukwe kuwa mwaka 2000 kama kumbukumbu ya Jubilei Kuu ya miaka 2000 ya Ukristo kila parokia ilijenga msalaba unaofahamika kama msalaba wa Jubilei. Ndiyo maana ukienda Nyaronga utaona msalaba uliojengwa mlimani Nyamayoka, Amethibitisha.

Kwa maana hiyo nia ni hiyo hiyo, ya mlima wa Kabhulankwi huko katika parokia ya Kakonko umekuzwa na kupewa hadhi ya kubeba msalaba wa Jubilei Kuu. Kiyungwe na Kitunda ni milima katika parokia za Makere na Janda ambako ilijengwa na kusimikwa misalaba ya Jubilei Kuu ya miaka 2000 ya Ukristo. Baada ya kuwa shughuli za ujenzi wa Msalaba huo wa Jubilei Kuu zimekamilika, mlima huo wa Kitwe uliendelea kupambwa na matakatifu.

Matukio mawili yatakayobaki katika historia

Askofu Mlola anasema, “Tarehe 25 Desemba 2000 yalitendeka matukio mawili ambayo yatabaki kuwa sehemu ya historia ya Buhabhugali, kwanza jina la Nyamayoka lilibadilishwa na Mhashamu Ask. Mkuu Paul Ruzoka aliyetangaza kuwa mlima huo utaitwa Nyabhitebhe badala ya Nyamayoka. Ilihimizwa kila parokia ijenge msalaba wa Jubilei, na ndivyo ilivyofanyika. Parokia ziliyotajwa hapa ni mfano tu wa kile kilichofanyika katika parokia nyingine. Pili: Askofu Mkuu  Ruzoka wa Jimbo Kuu la Tabora ambaye kwa wakati huo alikuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Kigoma, alizika masalia ya Mt. Maria Goreti chini ya Msalaba huo wa Jubilei Kuu. Pamoja na masalia hayo ya Mt. Maria Goreti tarehe hiyo hiyo ilizikwa pia Skapulari na Medali ya Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili.

Huo ulikuwa mwanzo wa safari nyingi za waamini kutoka sehemu mbalimbali kuja Buhabhugali mahali pazuri panapovutia kwani mwaka huo huo, siku tatu baada ya kuzika masalia ya Mt. Maria Goreti na skapulari na Medali ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, yaani tarehe 28 Desemba 2000, Buhabhugali ilipata wageni, wakubwa kwa wadogo. Mahali hapo pa kuvutia, kulifanyika Ibada ya Misa Takatifu na ni siku hiyo ambayo katika Jimbo lao Katoliki Kigoma, lilizinduliwa rasmi Shirika la Utoto Mtakatifu wa Yesu na likawekwa chini ya Ulinzi na Usimamizi wa Mt. Maria Goreti.

Bila shaka matukio haya yalikuwa yamebeba ujumbe mzito. Buhabhugali palikuwa panaandaliwa kuwa mahali pa wote: kwa uwepo wa masalia ya Mtakatifu Maria Goreti, Buhabhugali ilikuwa inaandaliwa  kuwa nyumbani kwa vijana. Kwa kitendo cha uzinduzi wa Shirika la Utoto Mtakatifu wa Yesu kijimbo kufanyika hapo, Buhabhugali, palikuwa panaandaliwa  kuwa nyumbani kwa watoto. “Kwa uwepo wa alama hizi muhimu za Mama yetu Bikira Maria, Buhabhugali palikuwa panaandaliwa kuwa nyumbani kwa wazazi. Sasa Buhabhugali kweli panavutia, ni nyumbani kwetu sote”. Ni mahali pa kukutana na Mungu na kujitajirisha kiroho kwa matakatifu yatakayokuwa yanaadhimishwa hapa”.

Uzuri wa Buhabhugali uneendelea kuongezwa na matakatifu

Akiendelea katika maandishi ya historia kuhusu eneo hilo , Askofu Mlola amesema: “Uzuri wa Buhabhugali umeendelea kuongezwa na matakatifu ambayo yamefanyika na yataendelea kufanyika hapa. Kazi ya ujenzi wa madhabahu haya  ambayo yanatabarukiwa leo, ulizinduliwa siku ya kufunga maadhimisho ya Jubilei Kuu ya miaka 2000 ya Ukristo, tukio ambalo lilifanyika katika kilele cha mlima Kitwe – hapa Buhabhugali- tarehe 6 ya mwezi Januari 2001”. Baada ya uzinduzi wa ujenzi kufanyika, kazi ya ujenzi ilianza. Ilikwenda pole pole ila hakuna hata mmoja ambaye alikuwa na mashaka kuwa siku moja kazi ya ujenzi itafikia sehemu nzuri ambapo Kanisa linaweza kuanza kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Askofu Mlola amesema: Kunako mwaka 2014 wakati wa uongozi wetu, ndipo ambapo ujenzi wa mahali hapa ulifanyika kwa kasi kubwa. Julai 2016 ndipo ambapo kazi ya mwendelezo wa kujenga Kanisa litakalotumika kama madhababu (shrine) ilianza rasmi. Mwaka huo huo tulipata wazo la kuweka kitu kingine ambacho kitawasaidia mahujaji na watu wengine pia, kupatumia mahali hapa ambapo ni pazuri na panapendeza kweli. Julai 2016, ulianza pia ujenzi wa Kituo kikubwa cha Ushauri ambacho nacho ujenzi wake umekamilika kwa kiasi kikubwa katika siku hii ya leo muhimu sana na ya kihistoria katika Jimbo letu Katoliki Kigoma; Kituo hiki kinabarikiwa na kuwekwa chini ya ulinzi na usimamizi wa Mt. Mama Teresa wa Kalkutta.

Shughuli hii ya kumalizia ujenzi wa Madhabahu haya na Kituo cha Ushauri imekuwa ya kuchosha kwa kuwa imefanywa ndani ya muda mfupi. Pamoja na uchovu huu, shughuli imekuwa yenye kutia faraja na furaha kwa kuwa baada ya kukamilisha kazi hii, wana wa Mungu wa ndani na nje ya Buha watapata huduma za kiroho na za kimwili kupitia vituo hivi: Madhabahu ya Bikira Maria, Afya ya Wagonjwa na cha Mtakatifu Mama Teresa wa Kalkutta.

Pongezi kwa waliofanikisha eneno hilo

Askofu Mlola anatoa, pongezi kwa Askofu Mkuu Paul Ruzoka aliyezaa wazo la kumiliki eneo hili na kupafanya kuwa mahali pa kukutana na Mungu. Pongezi kwa Mhashamu Askofu Mkuu Protase Rugambwa ambaye naye aliweka mipango ya uendelezaji wa ujenzi wa eneo hili pamoja na kwamba, alihama shughuli zikiwa bado hazijaanza kama ilivyokuwa imepangwa. Askofu Mlola anathibitisha:  “Nasi tunamshukuru Mungu kwa kuwa alitupa ujasiri wa kutokuogopa mradi mkubwa huu tulioukuta. Tulimkimbilia Bwana na kumwomba afanikishe shughuli hii. Ikiwa wengi wanashangaa namna ambavyo imewezekana kwa muda mfupi tena katika kiwango hiki, wafarijike kwa kutambua kuwa na sisi ni miongoni mwa wanaoshangaa. Ukweli ni kwamba yule yule aliyependa mambo haya yatendeke hapa na yakamilike, alitupa hamu ya kusali kwa ajili ya shughuli hii; na kwa kuwa aombaye hupata, ndiyo maana Mungu mtoaji wa mapaji yote alijibu sala na maombi yetu kwa ajili ya Taifa la Mungu la Kigoma na nje ya Kigoma. Shukrani za pekee ziwaendee wafadhili na wote wenye mapenzi mema waliotusaidia kwa hali na mali katika ujenzi huu.

Shukrani kwa mafundi wote waliohusika katika ujenzi huu

Askofu Mlola anasema: Tunawashukuru hata wale ambao walitoa ushauri au hata kukosoa namna ya ujenzi ilivyofanywa. Shukrani kwa Mungu kwa ajili ya wale wote ambao, kupitia vituo hivi viwili vilivyoko hapa Buhabhugali, watazitajirisha roho na maisha yao ya safarini kuelekea mbinguni. Kwa unyenyekevu twazidi kusema asante kwa Mungu kwa ajili ya wale wote ambao watarudishiwa amani, furaha na upya wa maisha moyoni, katika familia na jumuiya zao wanakoishi na kufanya kazi, kupitia mafundisho, semina, mafungo, ushauri na matakatifu yatakayoadhimishwa hapa. Furaha yetu ni kubwa kwa kuwa Madhabahu haya pamoja na kituo cha Ushauri vimezinduliwa mbele ya Maaskofu wa majimbo ya Metropolitani ya Tabora na mbele ya Abate wa Abasia ya Mvimwa.

Tunawakaribisha tena na tena ninyi pamoja na Taifa la Mungu katika Majimbo yenu na maeneo yenu ya uchungaji. Mahali hapa pameitwa jina la Buhabhugali yaani “Buha ni pana”; si kwa waha tu bali hata kwa kaka na dada zetu katika Kristo watakaotufikia wakiwa na nia ya kutumia huduma zinazotolewa hapa Buhabhugali.  Mama Maria Afya ya Wagonjwa pamoja na watakatifu wote ambao majina yao yametajwa katika historia hii na wale ambao picha zao zimepamba kuta za Madhabahu haya, watuombee. Amina

05 November 2018, 09:18