Maaskofu ni madaraja ya umoja na mshikamano kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa! Maaskofu ni madaraja ya umoja na mshikamano kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa! 

Jubilei ya Miaka 50 ya CEAST: Utume wa Maaskofu mahalia!

Maaskofu wanapaswa kujikita zaidi na zaidi katika wongofu wa kimisionari, ili kukuza na kudumisha ari, wito, maisha na utume wa kimisionari ndani ya Kanisa; kwa kuhamasisha miito ya kipadre na kitawa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya pamoja na kuhakikisha kwamba, vyama na mashirika ya kitume yanachangia kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa linahitaji viongozi wakweli na waadilifu; watu wanaoweza kujitosa kimasomaso kwa ajili ya watu wa Mungu waliokabidhiwa kwao. Kanisa halihitaji mameneja, bali Askofu ambaye ni shahidi wa ufufuko wa Kristo; mtu mnyenyekevu na jasiri. Kanisa halihitaji wapambanaji, bali viongozi wanyenyekevu watakaopandikiza mbegu ya haki, ukweli na amani. Maaskofu mahalia wawe kweli ni watu walioteuliwa na Kristo Yesu kwa njia ya Roho Mtakatifu, kwa ajili ya Kanisa lake. Maaskofu mahalia ni watu ambao wanapaswa kuzingatia mahitaji ya Makanisa kwa kusoma alama za nyakati. Askofu awe ni mtu mwenye uwezo wa kuunganisha nguvu na rasilimali iliyopo kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Jimbo husika. Ustawi na maendeleo ya Kanisa yanategemea kwa kiasi kikubwa ni ubunifu wa Askofu mahalia katika maisha na utume wa Kanisa!

Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu wakati wa ziara yake ya kichungaji nchini Angola kuanzia tarehe 10 - 20 Novemba 2018 kama sehemu ya kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tome na Principe, CEAST, Jumapili, tarehe 18 Novemba 2018 wakati wa maadhimisho ya Siku ya II ya Maskini Duniani sanjari na kilele cha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tome na Principe, amekazia dhamana na utume wa Maaskofu mahalia nchini Angola.

Ibada hii imeadhimishwa kwenye Parokia ya Bikira Maria wa Fatima, Jimbo kuu la Luanda, Angola. Kardinali Filoni anasema, katika kipindi cha miaka 50 ya maisha na utume wa CEAST kumekuwepo na uwajibikaji wa pamoja katika urika wa Maaskofu Katoliki nchini Angola, Sao Tome na Principe. Maaskofu wanapaswa kujikita zaidi na zaidi katika wongofu wa kimisionari, ili kukuza na kudumisha ari, wito, maisha na utume wa kimisionari ndani ya Kanisa; kwa kuhamasisha miito ya kipadre na kitawa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya pamoja na kuhakikisha kwamba, vyama na mashirika ya kitume yanachangia kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu.

Kardinali Filoni anakaza kusema, Ili kufikia lengo hili: Mashauri ya Kiinjili yaani: Ufukara, Utii na Useja; nidhamu, kanuni maadili na utu wema vinapaswa kuzingatiwa bila kusahau haki msingi za binadamu. Kardinali Filoni ameonya kuhusu haki binafsi na uhuru usiokuwa na mipaka ni hatari kwa umoja na mafungamano ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Maaskofu washikamane na kusaidiana katika urika wao, ili kwa pamoja waweze kuwatakatifuza, kuwaongoza na kuwafundisha watu wa Mungu nchini Angola, Sao Tome na Principe.

Familia ya Mungu inapaswa kujenga na kudumisha mahusiano mema na Kristo Yesu kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na Maadhimisho mbali mbali ya Mafumbo ya Kanisa. Maaskofu wajenge na kuimaarisha umoja na mshikamano na wakleri, watawa, makatekista na waamini walei katika ujumla wao, ili wote kwa pamoja waweze kujisikia kuwa ni sehemu ya familia ya Mungu inayowajibika na kutaabikiana. Malezi awali, endelevu na fungamani ni muhimu sana kwa familia ya Mungu, dhamana inayopaswa kutekelezwa kwa dhati kabisa na Maaskofu mahalia!

Kardinali Fernando Filoni, amekazia pia ushirikiano wa dhati kati ya Maaskofu mahalia na watawa wa mashirika mbali mbali ya kitawa na kazi za kitume, kwa kutambua kwamba, wanao mchango mkubwa katika masuala ya: elimu, afya, katekesi, ustawi na maendeleo endelevu na fungamani katika jamii. Amewataka Maaskofu kushirikiana kwa karibu na waamini walei, ili waweze kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Waamini walei wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya familia inayofumbatwa katika ndoa kati ya mwanaume na mwanamke na kamwe wasikubali kumezwa na ukoloni wa kiitikadi unaokumbatia pamoja na mambo mengine, utamaduni wa kifo. Maaskofu waimarishe utume wa familia za Kikristo kama shule ya imani, tunu msingi za maisha ya Kikristo na kiutu. Maaskofu wajenge sanaa na utamaduni wa kuwasikiliza waamini walei, ili hatimaye, kujibu kwa busara matamanio yao halali katika maisha na utume wa Kanisa!

Angola: CEAST 50 YRS
20 November 2018, 11:09