Tafuta

Vatican News
Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji ni wakati muafaka wa kurithisha na kushuhudia imani katika matendo. Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji ni wakati muafaka wa kurithisha na kushuhudia imani katika matendo. 

Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania: Ushuhuda wa imani

Askofu mkuu mstaafu Josaphat Louis Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha, wakati huu wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya uinjilishaji nchini Tanzania anao ujumbe maalum kwa familia ya Mungu nchini Tanzania. Anaitaka familia ya Mungu kukuza, kudumisha na kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo kwa kutambua kwamba, hii ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji nchini Tanzania yanaongozwa na kauli mbiu “Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji furaha ya Injili na kilele cha maadhimisho haya ni Jumapili, tarehe 4 Novemba 2018. Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, ametumia fursa hii kuwakaribisha waamini kuhudhuria katika kilele cha maadhimisho haya, ili kwa pamoja waweze kumshukuru Mungu kwa zawadi ya imani.

Tarehe Mosi, Novemba 2018, Askofu Telesphory Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro, ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea waamini marehemu, lakini zaidi, wamisionari waliojisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili nchini Tanzania. Baadaye, walikwenda kubariki makaburi ya waamini Parokia ya Bagamoyo, ambamo, wamezikwa wamisionari wengi!

Maadhimisho haya yamekuwa ni fursa ya kutafakari kwa kina na mapana matendo makuu ya Mungu katika maisha na utume wa Kanisa nchini Tanzania pamoja na kuendelea kujenga mahusiano ya dhati na Kristo Yesu kwa njia ya Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, ili Kristo Yesu aendelee kumimina neema na baraka zake kwa familia ya Mungu nchini Tanzania.

Miaka 150 ya uinjilishaji Tanzania Bara ni mada ambayo imechambuliwa kwa kina na mapana na Askofu Msaidizi Methodius Kilaini wa Jimbo Katoliki Bukoba. Elimu Katoliki kwa ajili ya malezi fungamano katika kipindi cha miaka 150 ya uinjilishaji imedadavuliwa na Padre Charles Kitima, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Katika maadhimisho haya kumekuwepo na semina za makundi. Askofu mkuu mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwaichi amechambua maeneo makuu matatu yanayohitaji uinjilishaji mpya nchini Tanzania.

Mada kuhusu Mlei Mkatoliki katika kuyatakatifuza malimwengu imetolewa na Padre Raymond Saba, kutoka Jimbo Katoliki la Kigoma, ambaye amewahi kuwa pia Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Nafasi ya vijana katika mchakato wa uinjilishaji mpya ni mada ambayo inachambuliwa na Askofu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Mada nyingine zilizopewa uzito wa juu ni watoto na uinjilishaji!

Askofu mkuu mstaafu Josaphat Louis Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha, wakati huu wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya uinjilishaji nchini Tanzania anao ujumbe maalum kwa familia ya Mungu nchini Tanzania. Anaitaka familia ya Mungu kukuza, kudumisha na kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo kwa kutambua kwamba, hii ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambaye kwa njia ya ubatizo, amewawezesha kuwa ni watoto wake wapendwa na ndugu zake Kristo Yesu, licha ya mapungufu yao kama binadamu! Wakristo wanapaswa kukuza na kuimarisha imani katika medani mbali mbali za maisha; daima wakikumbuka kwamba, wao wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake!

Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara, waamini wamekirimiwa neema na baraka zinazowataka kuwa ni washiriki wa kazi ya uumbaji na ukombozi. Kwa njia ya Mafumbo ya Kanisa waamini wamekirimiwa fadhila ya: imani, matumaini na mapendo; karama na mapaji ya Roho Mtakatifu wanayopaswa kuyatumia katika maisha na utume wao hapa duniani.

Askofu mkuu Lebulu

 

 

02 November 2018, 16:49