Tafuta

Vatican News
Askofu Gervas Nyaisonga: Risala ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika kilele cha Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji. Askofu Gervas Nyaisonga: Risala ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika kilele cha Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji. 

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Risala, kilele cha Jubilei ya miaka 150 ya Uinjilishaji

Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania, amesema ni sherehe za ukombozi na ushindi katika Kristo dhidi ya utumwa, pamoja na kufurahia kazi ya Mungu inayoonekana nchini Tanzania. Kutokana na zawadi ya imani inayofumbatwa katika tunu msingi za kiinjili, waamini wameweza kuwa ni chumvi na mwanga kwa watanzania wenzao.

Na Askofu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, TEC. – Bagamoyo, Pwani.

Askofu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika risala ya Baraza wakati wa kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania, amesema, Jubilei hii ni sherehe za ukombozi na ushindi katika Kristo dhidi ya utumwa, pamoja na kufurahia kazi ya Mungu inayoonekana nchini Tanzania. Kutokana na zawadi ya imani inayofumbatwa katika tunu msingi za kiinjili, waamini wameweza kuwa ni chumvi na mwanga kwa watanzania wenzao.

Kanisa liko katika mchakato wa kuwatangaza watumishi wa Mungu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sr. Bernadeta Mbawala kuwa wenyeheri na hatimaye watakatifu. Uhuru wa kuabudu kikatiba umeliwezesha Kanisa Katoliki nchini Tanzania kuchangia kwa dhati kabisa katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya watanzania wote!  Askofu Nyaisonga amesema, Rais Magufuli pia ni tunda la Jubilei ya Miaka 150 ya uinjilishaji nchini Tanzania. Kanisa lina mpongeza kwa kazi kubwa anayoifanya katika kujenga na kudumisha dhamiri na hofu ya Mungu; nidhamu ya kodi na kazi, ujenzi na uimarishaji wa miundo mbinu pamoja na dhana ya uongozi kama huduma kwa watanzania!

Askofu Nyaisonga amekaza kusema, kuna matukio ya watu kutekwa nyara, kutozingatiwa kwa kanuni za utawala wa sheria kwa baadhi ya watendaji, rushwa, uonevu, migogoro kati ya wakulima na wafugaji; uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji. Haya ni mambo yasiyopendeza na ambayo yanahitaji kuvaliwa njuga na wadau mbali mbali. Kanisa linapania kuendelea kujielekeza katika mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii na kwamba, tofauti ya karama, hadhi sawa, umoja wa amani katika Mungu ni mwongozo ambao Kanisa linapenda kuufanyia kazi kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji nchini Tanzania.

IFUATAYO NI RISALA YENYEWE KWA KIREFU!

Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Daktari John Pombe Joseph Magufuli. Mwadhama John Kardinali Njue, mwakilishi wa Baba Mtakatifu kwenye sherehe hizi,  Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, wahashamu maaskofu wakuu, wahashamu maaskofu, waheshimiwa mapadre Valentin Bayo na Francis Kangwa mliotumwa na Baba Mtakatifu kumsindikiza Kardinali mwakilishi wake, waheshimiwa viongozi wa serikali mliopo hapa, waheshimiwa viongozi wa vyama vya siasa, waheshimiwa viongozi wa madhehebu ya dini na dini mbalimbali, waheshimiwa mabalozi wa nchi mbalimbali, waheshimiwa mapadre na watawa, waheshimiwa waamini  na wageni wetu wote, amani ya Mungu iwe nanyi.

Tuko kwenye sherehe hizi za kikatoliki kitaifa za Jubilee ya Miaka 150 tangu wamisionari wa kwanza Wakatoliki walipoingia Tanzania Bara. Ni sherehe za ukombozi na ushindi  katika Kristu dhidi ya utumwa wa kila aina. Tunafurahia na kushangilia kazi ya Mungu inayoonekana hapa Tanzania. Wamisionari wa kwanza kutuletea dini Katoliki walikuwa watawa wa Shirika la Roho Mtakatifu wakiongozwa na Padri Athony Honer mwaka 1868. Na shirika bado linaendelea  na utume wao hapa Bagamoyo na sehemu mbalimbali nchini. Mwaka 1878 Shirika la Wamisionari wa Afrika (White Fathers)waliwasili  hapa na kuelekea magharibi hadi Uganda. Wabenediktini waliwasili mwaka 1889.

Tukio la leo ni kilele cha kipindi cha sala na neema tulichokuwa tunakiadhimisha tangu mwaka jana. Tunamshukuru Mungu kwa kutupa fursa ya kumfahamu na kumwamini Yesu Kristo, Mkombozi wa Binadamu wote.  Kutokana na imani hii katika Kristo, Kanisa Katoliki kwa njia ya tunu za Injili tumeweza kuwa chumvi na mwanga kwa watanzania wenzetu katika nyanja mbalimbali za maisha, hususani nyanja za kiroho na kijamii. Wakatoliki tumeshiriki kujenga ufalme wa Mungu hapa Tanzania.

Kutokana na ustawi wa imani yetu Kanisa Katoliki Tanzania limeweza kutoa matunda ya kulifaa Bara la Afrika na dunia. Mwadhama Laurian Kardinali Rugambwa, mtanzania, ndiye Kardinali wa kwanza mwafrika.  Aidha, ndani ya miaka hii 150, Kanisa katoliki bado  halijatangaza mtakatifu wa mfano mtanzania. Hata hivyo tuna matumaini juu ya  waamini wawili, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyejifunza tunu za Injili za kuheshimu utu na maendeleo ya wote, na Mtawa Sista Bernadeta Mbawala, OSB ambao wametajwa kuwa watumishi wa Mungu, yaani wameingia kwenye mchakato utakaothibitishwa siku moja kuwa wao ni wenye heri na hatimaye watakatifu.

Tunaamini wapo waamini marehemu waliothibitisha kwa dhati imani yao kwa Mungu wakati wa uhai wao na wako mbinguni. Tunaendelea kusali ili Mwenyezi Mungu awathibitishe kuwa wenye heri na hatimaye watakatifu. Pamoja na kukiri mchango huo wa wamisionari katika kutufanya tutoe mchango unaoonekana wazi kwa jamii yetu, tunatambua kuwa mafanikio yetu hayakuletwa na wamisionari tu. Uwepo Kikatiba kwa Uhuru wa kuabudu na kueneza dini tangu enzi za mababu wa nchi hii uliwafanya watawala na viongozi wa serikali kuwapokea na kuwawezesha wa misionari kuanzisha na kuendeleza kazi za unjilishaji. Mfano mzuri ni wa Sultan Seyyeid Majid wa Zanzibar, mtemi Bushiri na maliwali wa Bagamoyo 1868 waliwapokea wamisionari na kuwapa misaada waliyohitaji ili waweze kufanya kazi zao za kueneza dini ikiwepo kuwakomboa watumwa, kuwajengea makazi na kuanzisha mfumo wa elimu rasmi wa shule(formal education). Tunashukuru Kanisa Katoliki kwa kuwa waanzilishi wa elimu rasmi hapa nchini  na kujenga shule ya Kwanza Tanzania Bara mwaka 1868.

Mafanikio yetu yalichangiwa pia na ushirikiano mzuri kati ya wakatoliki na viongozi wa kiraia, waamini wa dini na madhehebu mengine na hata washirika walio nje ya nchi yetu zikiwepo serikali za nchi za Ulaya. Katika fursa hii hatuna budi kuwashukuru wote kwa michango ya hali na mali katika kustawisha na kudumisha utume wa Kanisa Katoliki. Aidha, tunawashukuru wote mliotusaidia katika maandalizi ya sherehe hizi hasa Mapadre wa Shirika la Roho Mtakatifu akiwepo Pd.Valentin Bayo. Mungu abariki juhudi zenu za maendeleo.

Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , tunapenda kukupongeza kwa jitihada zako za kustawisha amani katika nchi yetu. Tunapenda kukiri mafanikio makubwa ya taifa letu unayoyachagiza. Wewe pia leo uko kwenye “jubilee ya miaka mitatu” kwani kazi ulizofanya hasa kupambana dhidi ya rushwa na uhalifu matokeo yake ni kama kazi ya miaka ya kijubilei. Tangu umeingia madarakani tunashuhudia kuchukuliwa kwa hatua kubwa za kiutendaji ambazo hazitasahaulika katika historia ya maendeleo ya taifa letu. Udumifu wake kwa vizazi vijavyo unahitaji Taifa liyaunganishe matokeo haya na mitaala ya elimu na malezi ya maadili kitaifa. Lengo ni watu wawe na dhamiri za kujali na kuwa na hofu ya Mungu. Kwani mendeleo ya watu huenda sambamba na maendeleo ya vitu.

Umeweza kusimamia kwa dhati nidhamu ya kodi na kazi, kuendeleza miundo mbinu ya maji na umeme, kuchochea ujenzi wa viwanda, kufufua shirika la ndege la taifa (ATC), kuboresha huduma na biashara ya bandari zetu na ujenzi wa reli ya kisasa. Hii ni mifano michache ya mafanikio yako makubwa ya kitaifa ndani ya kipindi cha miaka mitatu. Mheshimiwa Rais, tunaamini kuwa mafanikio yako yanatokana na uongozi wako  unaowahamasisha watendaji uliowateua. Tumeshuhudia ukiwahimiza watanzania wawe na utamaduni wa kuwatumikia watu wote kwa kuongozwa na ukweli na haki. Kwa mantiki hiyo tunawapongeza watendaji wote wanaokusaidia kazi. Tunathamini kwa dhati utendaji mzuri sana wa Mheshimiwa Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan na utendaji thabiti na makini wa Waziri wetu Mkuu, Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa na watendaji wengine wanaojituma katika ngazi mbalimbali. Mheshimiwa Rais, tunajua kuwa ustawi wa Taifa letu  haujakamilika kwa asilimia mia moja. Bado kuna vikwazo vinavyohujumu jitihada zako za kujenga nchi yenye maendeleo na mshikamano kwa wote.

Mpaka sasa bado kuna matukio yasiyopendeza. Baadhi ya matukio hayo ni kutekwa nyara kwa watu, kushambuliwa kwa watu wasio na hatia, kutozingatiwa kanuni za utawala wa sheria na baadhi ya watendaji, rushwa na uonevu kwenye sekta ya huduma za kijamii, migogoro ya ardhi kwa wafugaji na wakulima ambao wengi wako vijijini, ukosefu wa ajira kwa vijana kutokana na sekta binafsi ya kiuchumi kutowekewa mikakati makini, kutotabirika kwa baadhi ya sera zetu, uharibifu wa mazingira hasa misitu na vyanzo vya maji, matumizi mabaya ya madaraka, ucheleweshaji mkubwa wa utoaji wa vibali kama vile leseni na hati, uhaba wa wataalamu wa afya na uhaba wa maji kwa watanzania wengi hasa walioko vijijini. Tunapendekeza uwepo ufuatiliaji wa utendaji wa ngazi zote na kuboresha mazungumzano(dialogue) na wadau wa maendeleo. Udhaifu katika ngazi za chini na kukosekana mazungumzano kati ya serikali na wadau wa kiraia unaweza kukwamisha umahiri na ufanisi wa ngazi za juu.

Mheshimiwa Rais, Baraza la Maaskofu Tanzania linatambua kuwa ni jukumu lake kuendeleza kazi nzuri iliyofanywa na wamisionari na watangulizi wetu. Baraza linakusudia kutimiza utume wake ili dini yetu iendelee kuwahudumia watanzania wote kwa kila hali ili  wapate kujikomboa  kiroho na kijamii. Tunakusudia kutoa mchango wa pekee kwa watanzania  na ulimwengu ili baada ya miaka 150 ijayo utume wa Kanisa Katoliki katika nchi yetu uwe na matokeo chanya mengi zaidi ya hayo tunayoyashuhudia  katika maadhimisho haya. Kitabu cha historia ya miaka 150 ya Ukatoliki Tanzania kinaonyesha  taasisi katoliki za elimu 777(228 chekechea, 165 msingi, 262 sekondari na 110 VETA), vyuo vikuu vinne vyenye matawi saba. Taasisi za afya ziko 519. Taasisi zetu nyingi ziko vijijini wanakoishi watanzania wengi.

Mheshimiwa Rais, azma yetu ya ukombozi wa watu wote Tanzania inakabiliana na vikwazo vingi vya kisera na kijamii. Hata hivyo, tunajipa moyo kuwa tutashinda vikwazo hivyo kwa msaada wa Mungu. Tunawaomba watanzania wenzetu watuombee na kutuunga mkono ili dhamira yetu ya kumpa kila mtanzania fursa ya elimu bora itimie; kusudio letu la kumpa  mtanzania huduma bora za afya litekelezwe na wajibu wetu wa kuwasaidia kiroho viongozi wa umma kutimiza vizuri wajibu wao kwa Mungu, kwa taifa na nafsi zao wenyewe utimizwe.

Mheshimiwa Rais, dhamira ya Mkutano Mkuu wa Maaskofu wa Umoja wa Mabaraza ya Maaskofu wa nchi 9 za Mashariki mwa Afrika: Association of Member Episcopal Conferences of Eastern Africa (AMECEA) uliofanyika Agosti 2018 huko Addis Ababa, Ethiopia,ilihusu heshima kwa “Tofauti ya karama zetu, hadhi sawa, umoja wa amani katika Mungu kwenye kanda yetu ya AMECEA”: Vibrant Diversity, Equal Dignity, Peaceful Unity in God in the AMECEA Region. Dhamira hii inadokeza vipaumbele vya utume wetu ujao.  Tunatambua na kuheshimu kuwa tofauti zetu katika karama na vipaji ni utajiri wa jamii, ni bora kipekee na zinastahili kuheshimiwa tunapostawisha tunu za usawa wa hadhi ya mwanadamu, umoja na amani na hivi ndivyo atakavyo Mungu katika nchi yetu.

Tunahimiza dhamira hii itafakariwe katika nchi yetu ili kuzidi kujenga taifa la watu wanaodhihirisha kwa uhuru karama zao mbalimbali huku wakiheshimu usawa wa hadhi, amani na umoja. Kwa miaka 150 iliyopita Kanisa liliweka kipaumbele cha kujenga uheshimu wa utu, maendeleo kwa wote, amani na umoja. Haya tutaendelea kuyaeneza na kuyafundisha kwa mwanga wa Kristu kwani imani ya kweli lazima ithibitishwe na matendo yenye upendo kwa wengine.

Mwisho, Mheshimiwa Rais, tunapenda kukushukuru tena kwa kupokea mwaliko wetu na kuja kushiriki nasi tendo hili la kumshukuru Mungu na kuendeleza uinjilishaji. Tunakupongeza kwa utendaji wako wa miaka mitatu tangu uchukue majukumu ya kuingoza Tanzania. Tunakuombea baraka za Mungu katika shughuli zako. Maneno ya Mtume Yohane kwa watu wote yatupe nguvu, Katika hili tumelifahamu pendo, kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu” (1Yoh. 3:16).

Washangwera asanteni sana kwa kushiriki kwa moyo maadhimisho haya.

Askofu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga.

Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania.

Askofu Nyaisonga
05 November 2018, 10:30