IMBISA: Caritas Africa inapania kuboresha huduma ya upendo kwani ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa! IMBISA: Caritas Africa inapania kuboresha huduma ya upendo kwani ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa! 

IMBISA: Mchakato wa maboresho ya huduma ya upendo kwa maskini Kusini mwa Afrika!

Caritas Africa inataka kuratibu kikamilifu huduma yake kwa Bara la Afrika kwa kushirikiana na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Majimbo katika ujumla wake ili kujenga umoja wa Kikanisa na huduma ya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu; kuimarisha umoja na mshikamano na wadau mbali mbali wa maendeleo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Misaada ya Kanisa Katoliki Barani Afrika, Caritas Africa katika Tamko la Dakar la Mwaka 2017 linasema, Caritas Afrika itaendelea kujikita katika mchakato wa kumwilisha upendo wa Mungu katika huduma makini ya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu, kwa kutambua kwamba, upendo wa Mungu ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa. Kanisa linafundisha kwamba, upendo wa binadamu unapata utimilifu katika upendo wa Mungu, ulioshuhudiwa kwa namna ya pekee na Kristo Yesu kwa njia ya maisha yake.

Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Barani Afrika, “Caritas Africa” kwa kushirikiana na Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, kuanzia tarehe 29 Oktoba hadi tarehe 3 Novemba 2018 wanafanya mkutano wa kimataifa unaoziunganisha nchi wanachama wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, IMBISA.

Caritas Africa inataka kuratibu kikamilifu huduma yake kwa Bara la Afrika kwa kushirikiana na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Majimbo katika ujumla wake ili kujenga umoja wa Kikanisa na huduma ya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu; kuimarisha umoja na mshikamano na wadau mbali mbali wa maendeleo ili kujenga utamaduni wa amani na maendeleo ya kweli yanayofumbatwa katika utambulisho wa Kanisa Katoliki kwamba, huduma ya upendo ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia.

Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki yanayojihusisha na matendo ya huruma, yasijikite tu katika kutafuta na kugawa fedha kwa ajili ya huduma, bali yaguswe na mahitaji ya watu kwa kuwamasisha waamini kutambua umuhimu wa kushirikishana, kuheshimiana na kupendana mintarafu moyo wa Injili ya Kristo. Mashirika yajitofautishe na mashirika mengine ya misaada ya kijamii kwa kuwa makini na huduma yanazotoa kwa wahitaji na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Huduma hizi zinaweza kuwa ni katika ngazi mbali mbali!

Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki, Caritas ni mali ya Kanisa na limepata mafanikio makubwa, linaheshimiwa na kuthaminiwa na waamini pamoja na watu wengine sehemu mbali mbali za dunia kutokana na ukarimu kama kielelezo makini cha imani kwa kujibu kwa wakati muafaka mahitaji ya maskini. Kutokana na mwelekeo kama huu, waamini wengi wameanzisha Mashirika ya misaada ambayo ni kielelezo cha huduma ya upendo kwa wahitaji. Mashirika haya yanatofautiana katika asili na sharia, ingawa yanaoneshwa jinsi ambavyo yanahitaji kujibu kilio cha huduma ya upendo kwa wahitaji.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI  katika barua yake binafsi “Intima Ecclesia Natura” yaani “Huduma ya upendo ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa” anasema, Mama Kanisa anatekeleza wajibu na utume wake kwa kuzingatia misingi mikuu mitatu: Kutangaza Neno la Mungu; kuadhimisha Sakramenti za Kanisa na kutoa huduma. Mambo haya matatu yanakwenda pamoja na kamwe hayawezi kutenganishwa”. Huduma yaanasema Mashirika haya hayana budi kuratibiwa na Kanisa kama kielelezo cha viongozi wa Kanisa kutambua na kuthamini mchango wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa; kwa kuheshimu sheria na kanuni husika, uongozi uliopo kama kielelezo cha uhuru wa Wabatizwa. Itakumbukwa kwamba, Kanisa Katoliki lina taasisi zake linaloratibu misaada inayokusanywa kutoka kwa waamini mbali mbali; taasisi hizi zinafuata sheria na uongozi unaoziwezesha kujibu kwa uhakika mahitaji ya watu.

Caritas Africa

 

01 November 2018, 17:57