Tafuta

Haki msingi za Watoto Duniani 2018: Watoto ni matumaini ya leo na kesho ya binadamu! Haki msingi za Watoto Duniani 2018: Watoto ni matumaini ya leo na kesho ya binadamu! 

Haki ya Mtoto Duniani kwa Mwaka 2018: Watoto ni leo na kesho ya binadamu!

Kutokana na umuhimu wa kuwalinda watoto, mwaka 2017 ulitangazwa na Patriaki Bartolomeo kuwa ni “Mwaka wa Kulinda na Kudumisha Utakatifu wa Watoto”. Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema Vita, kinzani, migogoro na mipasuko ya kijamii, matokeo yake ni maafa na majanga makubwa katika utu na heshima ya binadamu; ukosefu wa usawa na haki jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

 

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1989 lilipitisha makubaliano ya haki msingi za watoto duniani. Haki hizo ni pamoja na kutobaguliwa, haki ya kuzaliwa na kuishi, haki ya kukua, na haki ya kusikilizwa. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kubainisha: sera na mikakati itakayotumika kuwalinda, kuwatetea na kuwaendeleza watoto, ili kupunguza vifo vya watoto wadogo pamoja na kuwakinga dhidi ya nyanyaso mbali mbali wanazokabiliana nazo katika maisha, malezi na makuzi yao! Ili kufikia lengo hili kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kuwekeza zaidi katika lishe bora, maji safi na salama pamoja na uhakika wa elimu bora na wala si bora elimu pamoja na kuwaandalia mazingira bora yatakayosaidia malezi na makuzi yao endelevu na fungamani!

Jumuiya ya Kimataifa iendelee kusimama kidete kulinda, kutetea na kuendeleza haki msingi za watoto; utu na heshima yao kama binadamu. Watoto wajengewe mazingira mazuri ya maisha, kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao kiroho na kimwili! Hizi ni changamoto zilizotolewa hivi karibuni na Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli wakati wa kuadhimisha Siku ya Haki za Mtoto Duniani kwa mwaka 2018. Ikumbukwe kwamba, watoto ni matumaini ya leo na kesho ya binadamu!

Kutokana na umuhimu wa kuwalinda watoto, mwaka 2017 ulitangazwa na Patriaki Bartolomeo wa kwanza kuwa ni “Mwaka wa Kulinda na Kudumisha Utakatifu wa Watoto”. Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema Vita, kinzani, migogoro na mipasuko ya kijamii, matokeo yake ni maafa na majanga makubwa katika utu na heshima ya binadamu; ukosefu wa usawa na haki jamii. Watoto sehemu mbali mbali za dunia wanajikuta wakiwa wamezungukwa na madhara ya vita, dhuluma, nyanyaso, ubaguzi, magonjwa, njaa na umaskini wa kutupwa.

Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni, aliwataka wadau mbali mbali katika Jumuiya ya Kimataifa yaani familia na taasisi mbali mbali kuhakikisha kwamba watoto wanalindwa na kuendelezwa ili kamwe wasitumbukie wala kutumbukizwa katika nyanyaso na utumwa mamboleo. Ni matumaini yake kwamba, Jumuiya ya Kimataifa italinda haki msingi za watoto ikiwa ni pamoja na uhai wao, elimu, afya na malezi bora, ili kuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Siku ya mtoto duniani huadhimishwa kila mwaka iifikapo tarehe 20 ya mwezi Novemba ili: kukuza uelewa na kudumisha haki za msingi za mtoto ambazo ni kuishi, kuendelezwa, kushirikishwa na kulindwa.

Wakati huo huo, Baraza la Makanisa Ulimwenguni limempongeza na kumshukuru Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli kwa kusimama kidete: kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote! Hayo yamesemwa na Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Haki ya Mtoto Duniani. Ameendelea kufafanua kwamba, kuna uhusiano mkubwa katika athari za mabadiliko ya tabianchi, ustawi, maendeleo na makuzi ya watoto sehemu mbali mbali za dunia, kwani kimsingi watoto ndio waathirika wakuu wa mabadiliko ya tabianchi. Ukosefu wa maji safi na salama una madhara makubwa kwa afya ya watoto wengi duniani, kama ilivyo pia kwa ukame wa kutisha na baa la njaa inayosababisha utapiamlo wa kutisha kwa mamilioni ya watoto duniani.

 

Inakadiriwa kwamba, kuna watoto zaidi milioni 500 wanaoishi katika maeneo yaliyokumbwa na mafuriko sehemu mbali mbali za dunia; watoto wengine milioni 160 wanaishi katika maeneo yaliyokumbwa na ukame wa kutisha na wengine zaidi ya milioni 115 wanaishi katika mazingira hatarishi yanayoweza kukumbwa na tufani. Takwimu zinaonesha kwamba, kila mwaka athari za mabadiliko ya tabianchi zinatishia usalama na maisha ya watoto zaidi ya milioni 1.7. Ikumbukwe kwamba, athari za mabadiliko ya tabianchi ni kati ya sababu kubwa zinazochangia uwepo wa idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi!

Viongozi wa Makanisa wanathubutu kusema, maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ni hatari sana kwa utu na heshima ya watoto wadogo, kiasi cha watoto hata katika umri mdogo kuanza kujisikia kuwa wamekomaa na wanaweza kubeba dhamana na wajibu wa watu wazima! Wazazi na walezi wengi wameacha dhamana na wajibu wa malezi kwa watoto wao kwa computer na simu za viganjani. Watoto wamepokwa na utamaduni wa teknolojia ya mawasiliano, hatari sana kwa malezi na makuzi yao! Tangu mwanzo, watoto hawa wanaanza kuingizwa kwenye tabia ya ulaji wa kupindukia, ubabe wa kutisha na mashindano yasiyokuwa na tija wala mashiko kwa ustawi na maendeleo yao: kiroho na kimwili.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza analipongeza Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwa kuendelea kushirikiana na Kanisa Katoliki pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF ili kulinda na kudumisha haki msingi za watoto sehemu mbali mbali za dunia. Inasikitisha kuona jinsi ambavyo watoto wananyanyaswa na kudhulumiwa haki zao msingi, kuwalinda na kuwaendeleza watoto ni ujumbe unaopaswa kuvaliwa njuga na Wakristo wote duniani, sanjari na kuhakikisha kwamba, watoto hawa pia wanalindwa katika jamii na maeneo ya Makanisa!

Haki ya Mtoto Duniani

 

27 November 2018, 08:45