Tafuta

Vatican News
Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana: Utakatifu wa maisha! Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana: Utakatifu wa maisha!  (AFP or licensors)

Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana: Utakatifu wa maisha!

Utakatifu wa maisha hauna budi kumwilishwa katika medani mbali mbali za maisha kama sehemu ya kuyatakatifuza malimwengu, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi kwa kusimamia: utu, heshima na haki msingi za binadamu kama kielelezo makini cha imani katika matendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” (Mt. 5:12) anawaalika waamini kutambua vizingiti, changamoto na fursa ambazo wanaweza kuzitumia kufikia utakatifu wa maisha. Kristo Yesu anawaalika waja wake ili wawe watakatifu, watu wasiokuwa na hatia mbele zake katika upendo. Baba Mtakatifu anasema, maisha ya kikristo ni mapambano endelevu yanayohitaji nguvu na ujasiri, ili kumpatia nafasi Kristo aweze kushinda na hatimaye, waamini kufurahia maisha. Waamini watambue kwamba, shetani, Ibilisi yupo na wala si dhana ya kufikirika tu!

Waamini wawe macho na waendelee kukesha na kusali kwa kutambua kwamba, ushindi wao unafumbatwa katika Msalaba wa Kristo. Utakatifu ni chemchemi ya furaha na amani ya ndani. Huu ni mwaliko wa kupambana na “giza la maisha ya kiroho” kwa kujikita katika mang’amuzi ya maisha ya kiroho kwa kutafakari kwa kina na mapana matamanio halali ya maisha, uchungu na fadhaa katika maisha yao; hofu na mashaka ili kutambua njia zinazowaelekeza katika uhuru wa kweli, daima wakijitahidi kusoma alama za nyakati kadiri ya mwanga wa Kristo Mfufuka. Mang’amuzi ya maisha ya kiroho, yawasaidie waamini kutambua Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Hii ndiyo tema iliyoongoza mkutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana uliohitimishwa hivi karibuni, kwa kuchambua vizingiti, changamoto na fursa ambazo familia ya Mungu nchini Ghana itaweza kuzitumia kufikia utakatifu wa maisha sanjari na kuendelea kujenga Ufalme wa Mungu unaojikita katika utakatifu, kweli na haki pamoja na ushiriki mkamilifu wa Fumbo la maisha ya Kristo Yesu. Utakatifu wa maisha hauna budi kumwilishwa katika medani mbali mbali za maisha kama sehemu ya kuyatakatifuza malimwengu, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi kwa kusimamia: utu, heshima na haki msingi za binadamu kama kielelezo makini cha imani katika matendo!

Maaskofu Katoliki Ghana wanasema, “Heri za Mlimani” ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu, chemchemi ya utakatifu wa maisha. Hii ni changamoto kwa familia ya Mungu nchini Ghana kupambana na vitendo vya rushwa, ufisadi na wizi wa mali ya umma kwa kujikita katika ukweli, uwazi, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Serikali ya Ghana inapaswa kuonesha nia hii njema kwa vitendo, kwa kuwawajibisha wale wote wanaojihusisha na vitendo hivi viovu ndani ya jamii! Wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi kutoka Ghana ni changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi, kwani hawa ni watu wanaoteseka kwa utupu, kiu, njaa na kifo jangwani na baharini! Ghana inapoteza nguvu kazi yake, kumbe, kuna haja kwa Serikali kuhakikisha kwamba, sheria, kanuni na taratibu za uhamiaji zinafuatwa kikamilifu, ili kuokoa maisha ya watu.

Maaskofu wanasema, utunzaji bora wa mazingira ni kielelezo makini cha utakatifu. Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kuhakikisha kwamba, wanalinda misitu, vyanzo vya maji na kutunza mazingira nyumba ya wote kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Uchafuzi wa mazingira ni chanzo kikuu cha umaskini, magonjwa na majanga asilia. Familia ya Mungu nchini Ghana iwe makini na changamoto inayoendelea kujitokeza kwa baadhi ya watu na makampuni makubwa kujitwalia maeneo makubwa ya ardhi kwa mafao yao binafsi, kwa kutambua kwamba, ardhi ni mtaji wa maskini wengi nchini Ghana.

Ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana nchini Ghana, marekebisho ya mfumo wa utawala katika serikali za mitaa; umuhimu wa maboresho ya huduma za kijamii nchini Ghana kwa kuendelea kukazia Bima ya Afya; Ukweli na uwazi katika masuala ya mfumo wa huduma za Benki nchini Ghana; Maboresho ya huduma ya elimu, malezi na makuzi yanayofumbatwa katika kanuni maadili, utu wema ni kati ya mambo yaliyopewa mkazo na Maaskofu wa Ghana katika mkutano wao. Maaskofu wanawataka wanasiasa na wapambe wao kukazia demokrasia shirikishi kwa kutambua kwamba, uongozi ni huduma na wala si kichaka cha ubinafsi na uchoyo; kinzani na malumbano yasiyokuwa na tija wala mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wa Ghana. Maaskofu wa Ghana katika tamko lao wanasema, utakatifu ni chachu muhimu katika kudumisha: utu, heshima, haki msingi, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Maaskofu Katoliki Ghana
27 November 2018, 08:29