Tafuta

Vatican News
Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma hivi karibuni ametoa Sakramenti ya Kipaimara kwa Wakristo 75 kwenye Parokia ya Mt. Petro, Swaswa kwa "Wasomi" Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma hivi karibuni ametoa Sakramenti ya Kipaimara kwa Wakristo 75 kwenye Parokia ya Mt. Petro, Swaswa kwa "Wasomi" 

Askofu mkuu Kinyaiya awataka vijana kuenzi mila na tamaduni njema

Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo Kuu la Dodoma, Tanzania, hivi karibuni ametoa Sakramenti ya Kipaimara kwa waamini 75 wa Parokia Mtakatifu Petro, Swaswa, maarufu kama “Swaswa kwa wasomi”. Katika mahubiri yake, baada ya kufafanua kuhusu Sakramenti ya Kipaimara, amewataka vijana kuzingatia: tamaduni na maadili ya Kitanzania.

Na Rodirck Minja, Dodoma & Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Sakramenti ya Kipaimara ni zawadi ya umoja wa Kanisa; upendo na mshikamano katika kutangaza, kushuhudia; kulinda na kutetea imani ya Kanisa. Ni zawadi inayowawezesha waamini kuwa alama ya upendo, mashuhuda na vyombo vya amani katika jamii inayowazunguka! Kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara muungano wa wabatizwa na Kanisa hufanywa kuwa mkamilifu zaidi, kwani wanatajirishwa kwa nguvu ya pekee ya Roho Mtakatifu na hivi hulazimika kwa nguvu zaidi kuineza na kuitetea imani kwa maneno na matendo, kama mashuhuda wa kweli wa Kristo Yesu.

Kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara waamini wanampokea Roho Mtakatifu anayewawezeshwa kufanywa waana wa Mungu; kwa kuunganishwa zaidi na nguvu za Kristo pamoja na kupata mapaji ya Roho Mtakatifu na hivyo, kuwasaidia kukamilika zaidi kama viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Kwa njia hii, waamini wanajitoa sadaka na kuwa ni zawadi kwa ajili ya jirani zao! Waamini wanapopakwa mafuta ya Krisma wanapokea mhuri wa Paji la Roho Mtakatifu kutoka kwa Askofu mahalia.

Huyu ni Roho wa hekima na akili; Roho wa shauri na nguvu; Roho wa elimu na ibada na ni Roho wa uchaji mtakatifu. Mapaji yote haya yanapaswa kukua na kuzaa matunda kwa ajili ya jirani zao. Haya ndiyo maisha ya Kikristo, anayewawezesha waamini kujisadaka kwa ajili ya jirani zao kwa kuondokana na ubinafsi; ili hatimaye, kufungua njia katika maisha ya jumuiya inayopokea na kutoa. Waamini wakumbuke kwamba, wao ni vyombo vya Roho Mtakatifu kwa ajili ya jirani zao.

Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo Kuu la Dodoma, Tanzania, hivi karibuni ametoa Sakramenti ya Kipaimara kwa waamini 75 wa Parokia Mtakatifu Petro, Swaswa, maarufu kama “Swaswa kwa wasomi”. Katika mahubiri yake, baada ya kufafanua kuhusu Sakramenti ya Kipaimara, amewataka vijana kuzingatia: tamaduni na maadili ya Kitanzania na kamwe wasikubali kumezwa na utandawazi usiokuwa na mashiko wala mvuto kwa kuiga “mambo yanayoichefua jamii”. Amewataka vijana kuendelea kujiimarisha katika katekesi, Neno la Mungu na Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili waweze kuwa tayari kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha imani yao! Vijana wasikubali kuyumbishwa katika imani kama “daladala zilizokatika usukani”.

Mwenyezi Mungu apewe kipaumbele cha kwanza na kamwe wasikubali kudanganywa na manabii wa uwongo wanaotishia imani na maisha yao kwa mambo ya mwisho wa nyakati. Hivi karibuni Papa Francisko amesema, Yesu katika ufafanuzi wa Mambo ya Nyakati za Mwisho, anawarejesha wanafunzi wake kuhusu kazi ya uumbaji kadiri ya mpango wa Mungu; alama ya uhai, lakini jua kutiwa giza, mwezi kushindwa kutoa mwanga, nyota za mbinguni kuanguka na nguvu za mbinguni kutikisika ni alama ya mwisho wa nyakati, Kristo Yesu atakapokuja katika utukufu wake pamoja na watakatifu wote kuwahukumu wazima na wafu. Hii ndiyo siku ile ambayo wafuasi wake wataweza kuuona Uso wake uking’ara utukufu wa Fumbo la Utatu Mtakatifu; Uso wa upendo na ukweli. Jambo la msingi kwa waamini ni kujiandaa huku wakiwa wanakesha kwa kutenda matendo mema na yenye adili!

Jimbo Kuu la Dodoma
22 November 2018, 10:36