Vatican News
Askofu Evaristo Marcus Chengula aliyefariki dunia tarehe 21 Novemba 2018 atazikwa Jimboni Mbeya, tarehe 27 Novemba 2018 Askofu Evaristo Marcus Chengula aliyefariki dunia tarehe 21 Novemba 2018 atazikwa Jimboni Mbeya, tarehe 27 Novemba 2018  (AFP or licensors)

Marehemu Askofu Chengula: Ombolezeni kwa imani, matumaini, mapendo bila woga wala kukata tamaa!

Marehemu Askofu Evaristo Marcus Chengula alijisadaka bila ya kujibakiza: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kama sehemu ya utume wake kama Askofu; akavumilia yote, kwani alitambua wajibu na dhamana yake katika kazi nzima ya ukombozi, changamoto kwa familia ya Mungu Jimbo Katoliki Mbeya kuendeleza kazi ya ukombozi na utume wa Kanisa.

Na Thompson Mpanji, Mbeya & Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Alhamisi, tarehe 22 Novemba 2018 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Marehemu Askofu Evaristo Marcus Chengula wa jimbo Katoliki la Mbeya aliyefariki dunia tarehe 21 Novemba 2018 na anatarajiwa kuzikwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Anthony wa Padua, Jimbo Katoliki Mbeya, tarehe 27 Novemba 2018 baada ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa kwenye Kanisa la Hija, Mwanjelwa. Familia ya Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam, Jumatatu tarehe 26 Novemba 2018 itaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Kurasini na baadaye mwili wa Marehemu Askofu Chengula utasafirishwa kwenda Jimboni Mbeya kwa maziko.

Askofu Nyaisonga katika mahubiri yake yaliyochota utajiri wa Liturujia ya Neno la Mungu kadiri ya Kalenda ya Kanisa kwa siku hiyo aliitaka familia ya Mungu Jimboni Mbeya kuendeleza kazi ya ukombozi kwa kutangaza na kushuhudia Injili; kwa kusimama kidete pasi na woga; kwa kujiandaa kikamilifu, huku wakitimiza nyajibu zao kuelekea mwisho wa nyakati na kamwe wasikate tamaa, bali wawe ni watu wa imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani!

Askofu Nyaisonga alifafanu kwa ufundi mkubwa lugha ya picha iliyotumika katika Kitabu cha Ufunuo wa Yohane mintarafu mazingira ya majonzi na masikitiko kwa familia ya Mungu Jimboni Mbeya. Amesema, Simba wa Yuda na Mwanakondoo aliyechinjwa amemnunulia Mungu watu kutoka katika kila lugha, taifa na jamaa. Mwanakondoo ana uwezo na mamlaka; ufahamu, maarifa na ujuzi wote. Mwanakondoo ni chemchemi ya furaha na ujasiri pasi na kukata tamaa, kwani anawahakikishia usalama, amani na utulivu wa ndani.

Askofu Nyaisonga ameitaka familia ya Mungu Jimboni Mbeya kuomboleza kwa imani, matumaini na mapendo, kwani wamenunuliwa kwa thamani kubwa ya Damu Azizi ya Mwanakondoo wa Mungu. Marehemu Askofu Evaristo Marcus Chengula alijisadaka bila ya kujibakiza: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kama sehemu ya utume wake kama Askofu; akavumilia yote, kwani alitambua wajibu na dhamana yake katika kazi nzima ya ukombozi, changamoto kwa familia ya Mungu Jimbo Katoliki Mbeya kuendeleza kazi ya ukombozi na utume wa Kanisa. Amewataka waamini kamwe wasiogope kwani kuna Simba wa Yuda, Mwanakondoo wa Mungu anayewapigania.

Askofu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga ameendelea kufafanua kwamba, Injili inamwonesha Kristo Yesu akulilia Mji wa Yerusalemu! Amewakumbusha kwamba, siri ya fumbo la kifo imefichwa machoni pao, lakini kifo ni hakika, jambo la msingi ni kujiandaa vyema! Waendelee kushiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi, kwa kutimiza vyema wajibu wao kama waamini. Waendelee kumwombea Askofu Chengula ili aweze kuonana na rafiki yake mpendwa Kristo Yesu na Mwenyezi Mungu ambaye alikuwa ni dira ya maisha yake. Lakini kama kuna vikwazo vinavyokwamisha mchakato huu, basi sala na sadaka zao, zimsaidie kufika haraka kwenye lengo la maisha yake, yaani furaha ya maisha ya uzima wa milele.

Itakumbukwa kwamba, Askofu Evaristo Marcus Chengula alizaliwa tarehe Mosi Januari 1941, huko Mdabulo, Mufindi, Mkoani Iringa. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa na kipadre, tarehe 15 Oktoba 1970 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 8 Novemba 1996, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Mbeya na kuwekwa wakfu kama Askofu tarehe 2 Februari 1997. Askofu Evaristo Marcus Chengula Amefariki dunia tarehe 21 Novemba 2018 kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam. Jitihada za Madaktari kutaka kuokoa maisha yake, zikagonga mwamba na Askofu Evaristo Marcus Chengula akaaga dunia katika usingizi wa amani, akiwa na tumaini la ufufuko na maisha ya uzima wa milele! Alisimamia Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; akakazia uzuri na utakatifu wa Daraja Takatifu ya Upadre na Maisha ya wakfu; Elimu na malezi endelevu na fungamani kwa vijana wa kizazi kipya!

Aliwataka watanzania kukuza na kudumisha demokrasia shirikishi kwa kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, huku umoja, upendo na mshikamano kati ya watanzania ukipewa kipaumbele cha kwanza! Haya ni kati ya mambo ambayo wengi wataendelea kuyakumbuka katika maisha na utume wa Askofu Evaristo Marcus Chengula, bila kusahau Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa!

Marehemu Chengula

 

 

 

24 November 2018, 13:36